JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA
Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngorongoro, kwa kushirikisha Hifadhi
ya Taifa Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, inaendesha zoezi
la kuondoa mifugo na makazi ndani ya hifadhi ya Taifa Serengeti na
kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo.
Zoezi
hilo lililoanza tarehe 10 Agosti 2017 litadumu kwa siku kumi na nne
na linashirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngorongoro,
Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro,
Hifadhi ya Taifa Serengeti na Hifadhi ya eneo la Ngorongoro.
Zoezi
hilo linalenga kunusuru uhifadhi ndani ya hifadhi, ndani ya Pori
Tengefu Loliondo, na ndani ya mfumo ikolojia wa Serengeti na pia
kunusuru utalii katika mfumo ikolojia huo.
Aidha,
hatua hii ya kuondoa makazi na mifugo kutoka katika maeneo ya mipaka ya
Pori Tengefu Loliondo kutaongeza uhakika wa kupatikana malisho ya
mifugo wakati wa kiangazi kwa kuwa hakutakuwepo na makazi ndani ya
Hifadhi na ufugaji holela.
kimsingi zoezi hili linaendana na wito wa Serikali wa kuondoa mifugo ndani ya maeneo yote yaliyohifadhiwa nchini.
Katika
kutekeleza zoezi hili, Mkuu wa Wilaya Ngorongoro, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngorongoro Bwana
Rashidi Taka, alitoa maelekezo yafuatayo:
1.
Zoezi litafanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na kwenye mpaka
wa Pori Tengefu Loliondo. Kwa upande wa mpaka wa Pori Tengefu Loliondo
zoezi litaanzia kaskazini hadi kusini urefu wa kilometa 90, na upana
wake utakuwa kilometa 5. Kwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti
litafanyika upande wa mashariki kuanzia milima ya Kuka (kaskazini) hadi
kigingi na. SNP 9 (kusini);
2. Maboma
yatakayokutwa ndani ya hifadhi yatateketezwa kwa moto na watu
watakaokutwa na mifugo watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo
kupelekwa mahakamani;
3. Maboma
yaliyoko ndani ya mpaka wa Pori Tengefu Loliondo - kwenye mpaka na
ndani ya kilometa tano - wataondolewa ili warudi vijijini. Eneo hilo
litabaki kwa ajili ya malisho na si kwa ajili ya makazi. Uwepo wa
makazi kwenye mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti umekuwa kichocheo
kikubwa cha mifugo kuingizwa hifadhini.
Zoezi
hili linalenga kuondoa changamoto kubwa ya mifugo kuingizwa Hifadhi ya
Taifa Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo, kupambana na
uvamizi mkubwa uliofanywa na wahamiaji haramu kutoka nchi jirani na
kunusuru vyanzo vya maji kutokana na mifugo kulishwa kwenye vyanzo vya
maji na hivyo kusababisha vyanzo hivyo kuharibika na kukosekana kwa maji
kwa ajili ya mifugo na wanyamapori.
Hadi
sasa zoezi hili la kuondoa mifugo na makazi ndani ya Hifadhi ya Taifa
Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo linaendelea vizuri
likihusisha kuchoma moto maboma yote yaliyoachwa na wafugaji walioondoka
wakati wa zoezi.
Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuufahamisha umma kuwa hakuna watu wanaopigwa katika zoezi hili.
Pia,
Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuutaarifu umma kuwa habari
zinazosambazwa mitandaoni ni upotoshaji wa ukweli wenye nia ovu ya
kujenga chuki dhidi ya Serikali kwa wananchi wa Loliondo na maeneo
yanayopitiwa na zoezi hilo.
Aidha,
Wizara ya Maliasili na Utalii, inapenda kuweka bayana kuwa, taarifa za
kupigwa risasi Pormoson Losso mwenye umri wa miaka 23, mkazi wa
Ololosokwan zilitolewa tarehe 8 Agosti 2017 na hazihusiani na zoezi
tajwa kwani tukio hilo lilitokea siku tano kabla ya kuanza zoezi la
kuondoa mifugo na makazi ndani ya hifadhi wakati zoezi hili lilianza
kutekelezwa Jumapili tarehe 13 Agosti 2017.
Hata hivyo Serikali inawapongeza wananchi wengi miongoni mwa wafugaji kwa kuunga mkono zoezi hili na kwa ushirikiano wanaotoa.
Serikali
inatoa onyo kwa yeyote anayejihusisha na upotoshaji wa ukweli kuhusu
zoezi hili lenye nia njema linalolenga kunusuru hifadhi, kuacha mara
moja ili kujiepusha na hatua za kisheria zitakazochukuliwa pindi
atakapobainika.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
17/08/2017
No comments:
Post a Comment