Tuesday, August 29, 2017

ZABUNI YA MRADI WA UMEME WA STIEGLER’S KUTANGAZWA AGOSTI 30


Asteria Muhozya na Zuena Msuya, DSM
Serikali imesema kuwa ifikapo tarehe 30 Agosti, mwaka huu itatangaza Zabuni ya kuanza ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 2,100 katika Maporomoko ya Maji ya Mto Rufiji. (Stiegler’s Gorge).
Hayo yalielezwa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani wakati akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kalemani alitoa wito kwa Watanzania, Taasisi Binafsi na Kampuni zenye uwezo kutoka ndani na nje ya nchi kujitokeza kuomba zabuni hiyo mara baada ya kutangazwa na kuongeza kuwa, Serikali inazo fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi husika.
Aliongeza kuwa, tayari taratibu za awali za utekelezaji wa mradi huo zimekwisha anza ambapo Wataalam kutoka ndani na nje ya nchi wamekwishakutana na kupitia nyaraka za mradi ikiwemo kuchagua eneo ambalo mradi husika utajengwa.
Aidha, alieleza kazi ambazo tayari zimekwishaanza kutekelezwa ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu wa kujengwa miundombinu ya umeme jukumu ambalo limefanywa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakati Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza maandalizi ya ujenzi wa barabara katika eneo husika.
Dkt. Kalemani amesema kuwa, Mkandarasi atakayepewa kazi ya kujenga mradi huo ni yule atakayeridhia kujenga mradi husika kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi wa mwaka mmoja na nusu zaidi ya ule uliowekwa wa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwezi Oktoba au Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Dkt. Kalemani mradi huo unatarajiwa kuzalisha umeme wa kiasi cha Megawati 2,100 baada ya kukamilka kwake na utagharimu kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 2 ambazo zitatolewa na Serikali ya Tanzania.
Pia, Dkt. Kalemani alieleza kuwa, kukamilika kwa mradi husika kutasaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme nchini na kwamba Serikali haitarajii kuongeza bei ya umeme, vilevile, imeanza kuachana na uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta mazito.
“ Kwanza nipende tu kueleza hapa kuwa ndani ya kipindi cha miezi miwili tayari tumeanza kuachana na uzalishaji Umeme wa kutumia mafuta,” Aliongeza Dkt. Kalemani.
Dkt. Kalemani alisema kuwa, malengo ya Serikali ni kuzalisha umeme kiasi cha megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 kama Sera ya Nishati ya mwaka 2015 inavyoelekeza.
“Tunataka kujenga Tanzania ya Viwanda. Tunataka ifikapo mwaka 2019-20 tufike megawati 5,000. Tanzania ya Viwanda inahitaji umeme, mradi kama huu na pia ya Kinyerezi I Extension, MW 185 Kinyerezi II MW 240 na miradi mingine itawezesha kufikia lengo letu,” alisisitiza Dkt.  Kalemani.
Tanzania inatekeleza miradi ya Nishati nchini kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 ambayo inasisitiza uwepo wa nishati ya bei nafuu rahisi na yenye uhakika itakayowezesha mapinduzi ya viwanda nchini.

Tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini zimeonesha kuwa, Tanzania inaweza kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 4,700 kutokana na vyanzo vyake vya maji.

No comments: