Tuesday, August 29, 2017

KAMISHNA WA MADINI AANZA ZIARA KANDA YA ZIWA

Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (kulia), akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Samwel Sweda (wa pili kutoka kushoto), alipofika ofisini kwake akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Eliud Mwaiteleke. Wengine ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria-Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba (kushoto kwa Mkuu wa Wilaya) na Mhandisi Rayson Nkya (wa kwanza kulia).
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (katikati), akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Mradi wa Uchimbaji wa Kati wa Madini ya Dhahabu uliopo Ishokelahela wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza, Mrisho Masebu, kuhusu utendaji kazi wa Mradi huo.
Mmoja wa Viongozi wa Mradi wa Uchimbaji wa Kati wa Madini ya Dhahabu uliopo Ishokelahela wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza, Baraka Ezekiel (wa pili kutoka kulia), akifafanua jambo kwa Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (katikati) na Ujumbe wake. Kamishna Mchwampaka alitembelea Mradi huo Agosti 28 mwaka huu akiwa katika ziara ya kazi Kanda ya Ziwa.
Viongozi wa Mradi wa Uchimbaji wa Kati wa Madini ya Dhahabu uliopo Ishokelahela wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza, wakimwongoza Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (katikati), kukagua shughuli mbalimbali zinazofanyika katika mgodi huo. 
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (katikati), akiwa ameambatana na baadhi ya maafisa wa Wizara ya Nishati na Madini na wafanyakazi wa Mradi wa Uchimbaji wa Kati wa Madini ya Dhahabu uliopo Ishokelahela wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza, wakikagua sehemu mbalimbali za Mgodi huo.
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (mwenye koti), akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mradi wa Uchimbaji wa Kati wa Madini ya Dhahabu uliopo Ishokelahela wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza na Maafisa wa Wizara ya Nishati na Madini, mara baada ya kukagua Mgodi huo.
Shughuli za uchimbaji madini zikiendelea katika Mradi wa Uchimbaji wa Kati wa Madini ya Dhahabu uliopo Ishokelahela wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza.

Na Veronica Simba – Mwanza
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka, ameanza ziara ya kazi ya takriban juma moja katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali za sekta hiyo.
Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, Agosti 28 mwaka huu, Kamishna Mchwampaka alikutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Ofisi ya Madini, Kanda ya Ziwa Viktoria-Magharibi pamoja na wafanyakazi wa Ofisi Ndogo ya Ukaguzi wa Madini Kanda ya Mwanza, iliyokuwa ikijulikana kama Wakala wa Ukaguzi Madini Tanzania (TMAA).
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi hizo mbili, Kamishna Mchwampaka aliwataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii na kwa ushirikiano ili kufanikisha malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwaletea wananchi wake maendeleo ya dhati.
Katika hatua nyingine, akizuru Mradi wa Uchimbaji wa Kati wa Madini ya Dhahabu uliopo Ishokelahela wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza, Kamishna Mchwampaka, alipongeza jitihada za watendaji wa Mradi huo unaomilikiwa na wazawa wazalendo kwa asilimia mia moja, kwa ubia kati ya Isinka Federation 2014 Mining Cooperative Society Limited na Kampuni ya kitanzania ya Busolwa Mining Limited.
Alisema kuwa, jitihada zinazooneshwa na wajasiriamali hao wazalendo zinapaswa kuigwa na watanzania wengine kote nchini kwani Mradi huo una maendeleo ya kuridhisha na kujivunia japokuwa bado haujaanza uzalishaji.
“Sisi kama Serikali tunafarijika sana tunaposhuhudia wananchi wazalendo wakiweka jitihada na kufanikiwa katika biashara za madini kama hivi mnavyofanya ninyi. Tunaahidi kuendelea kuwasaidia kadri iwezekanavyo ili muweze kufikia malengo yenu na kuchangia katika kuinua uchumi wa nchi.”
Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa Mradi huo, Baraka Ezekiel na Mrisho Masebu, waliahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu ili mafanikio yao yaweze kuwahamasisha watanzania wengine.
Aidha, waliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kadri ipasavyo ikiwa ni pamoja na kulipa kodi zote stahiki pamoja na kufuata kanuni na sheria za madini zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.
Kamishna Mchwampaka pia alipata fursa ya kuwatembelea na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Samwel Sweda ambapo walikubaliana kushirikiana katika majukumu mbalimbali yanayohusu sekta ya madini kwa manufaa ya wananchi.
Hii ni ziara ya kwanza rasmi ya kikazi kwa Kamishna wa Madini, Mhandisi Mchwampaka tangu alipoteuliwa na Rais John Pombe Magufuli, kushika wadhifa huo, takribani miezi minne iliyopita.
Kamishna Mchwampaka anaendelea na ziara yake, ambapo katika siku ya pili atazuru Mkoa wa Geita.

No comments: