Sunday, August 20, 2017

WAKINA BABA WATAKIWA KUTOA TAARIFA ZA MAENDELEO YA WATOTO KWA WENZA WAO

  Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu akitoa elimu juu ya wajibu wa wazazi wa kiume katika malezi ya mtoto katika kikao cha wazazi kilichofanyika jana kwenye shule ya Saint Monica iliyopo jijini Arusha (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
 Mwalimu Mkuu wa shule ya Saint Monica Sister Pauline Etyang Nasike akitoa shukrani zake kwa Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mara baada ya Mkuu wa kitengo hicho kutoa elimu kwa wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo juu ya malezi ya watoto wao. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Wazazi wa wanafunzi wa shule ya Saint Monica waliohudhuria kikao hicho wakionekana wakimsikiliza kwa umakini mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu alipokuwa akitoa elimu juu ya umuhimu wa wazazi wa kiume kuwa karibu na watoto wao. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)


WAKINA BABA WATAKIWA KUTOA TAARIFA ZA MAENDELEO YA WATOTO KWA WENZA WAO


Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Kumekuwa na tabia iliyojengeka kwa baadhi ya jamii zetu kwamba taarifa za maendeleo ya masomo au ukatili na unyanyasaji wa watoto lazima zitoke kwa mzazi wa kike kwenda kwa mzazi wa kiume.

kufuatia hali hiyo Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoani hapa kimetoa ushauri kwa wazazi wa kiume kurudi nyumbani mapema pia kuwa na muda wa kuongea au kukaa na watoto wao na kuwa wa kwanza kutoa taarifa za maendeleo ya watoto kwa wake zao badala ya hali hiyo kufanywa na wenza wao pekee kama ilivyo sasa.

Akizungumza jana Jumamosi katika kikao cha wazazi wa wanafunzi ya Saint Monica iliyopo maeneo ya Moshono jijini hapa, Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu alisema kwamba, imekuwa kawaida kwa baadhi ya wazazi wa kiume kutokuwa na muda wa kukaa na watoto kwa kile tunachokiita uwajibikaji katika utafutaji na kushindwa kujua matatizo ya watoto wao.

Alisema mara nyingi wazazi wengi wa kiume wamekuwa wakijiweka pembeni katika kuwasikiliza watoto wao kwa masuala madogo madogo na kudhani kwamba wenzi wao pekee ndio wanapaswa kujua masuala hayo na kufikiri wao huwa wanatatua shida kubwa kama vile chakula, mavazi na ulipaji wa ada.

Alisema vitendo vya ukatili na unyanyasaji hasa ubakaji na ulawiti vinavyowakumba watoto vinatokana na wazazi kutokuwa na muda wa kuongea na watoto wao na hivyo kusababisha watoto hao kushindwa kutoa duku duku lao kwa watu wao wa karibu katika wakati sahihi.

Alisema wakati umefika sasa kwa baadhi ya wazazi wa kiume pamoja na kutimiza mahitaji mbalimbali ya nyumbani lakini wanatakiwa kutenga muda wa kukaa na watoto, kuwadadisi mambo mbalimbali, kuwasikiliza lakini pia kufuatilia nyendo zao badala ya kuwaachia wazazi wa kike pekee.

Alisema kama wazazi wote watasaidiana katika malezi ya watoto hasa kuwa nao karibu na kuwasikiliza itasaidia kwa kiasi kikubwa kugundua maendeleo yao lakini pia matatizo yao ambayo pengine walishindwa kuyaeleza kwa watu wengine.

Wakichangia katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na wazazi 580 miongoni mwa wazazi waliohudhuria kikao hicho Bw. Felix Mwetha alisema amevutiwa na elimu hiyo iliyotolewa na kitengo hicho lakini pia aliwataka wazazi wenzake wawe wanafanya maombi ili watoto wao wasikumbwe na vitendo hivyo.

Huku Bw. Mhando Bamara alisema kutokana na umuhimu wa elimu hiyo alilishauri jeshi la Polisi kuandaa programu maalum ambayo itatengeneza vipindi vya uelimishaji kupitia kitengo hicho ili watu wengi wafahamu badala ya kuishia kwenye vikao pekee.

Naye Sister Pauline Etyang Nasike ambaye ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, ambayo inamilikiwa na Augustinian Missionary Sisters alilishukuru Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto kwa kutoa elimu kwa wazazi pamoja na walezi lakini pia aliahidi kuandaa kikao kingine kitakachotoa fursa kwa kitengo hicho kutoa elimu kwa wanafunzi.

Imekuwa kawaida wanafunzi hasa wa shule za msingi kujitokeza kwa wingi na kuelezea matatizo yao mara baada ya Kitengo hicho cha Dawati la Jinsia na Watoto kutembelea shule hizo na kutoa elimu juu ya masuala ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji, hali inayojidhihirisha baadhi ya wazazi hawatoi nafasi ya kuwasikiliza watoto wao mara kwa mara.

No comments: