Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga,Kadama Malunde anayeandikia gazeti la Mtanzania na Mmiliki wa Mtandao wa Malunde1 blog amekamatwa na jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga wakati akipiga picha baada ya wananchi kuziba barabara ya Magadula mjini Shinyanga.Waandishi wetu wanaripoti.
Tukio hilo limetokea leo Jumatano Agosti 16,2017 majira ya saa tano asubuhi katika eneo hilo la barabara hiyo baada ya wananchi kuziba barabara hiyo kwa mawe na matofali wakidai wamechoshwa na vumbi kali linatokana na mchanga na simenti/saruji baada ya magari kupita eneo hilo.
Malunde alifika katika eneo hilo kutekeleza majukumu ya uandishi wa habari baada ya kupata taarifa kuwa wananchi wameziba barabara hiyo ili kuzuia magari yasipite katika barabara hiyo.
Baada ya kuwahoji wananchi hao ghafla askari wa jeshi la polisi walifika katika eneo hilo na kuwataka wananchi waliokuwepo eneo hilo kuondoa mawe na matofali huku mwandishi huyo akiendelea kupiga picha.
Wakati anaendelea kupiga picha askari mmoja alihoji kwanini anapiga picha ndipo Malunde aliposema ni mwandishi wa habari lakini askari huyo alimtaka atoe kitambulisho cha kazi na wakati anataka kuonesha kitambulisho alitokea askari mwingine (Mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Shinyanga) akihoji kwanini anapiga picha na kumwamuru apande kwenye gari la polisi.
Hali hiyo ilileta mvutano baina ya mwandishi huyo wa habari na askari polisi hao na hata alipoonesha kitambulisho mkuu huyo wa kituo cha polisi alisisitiza apandishwe tu kwenye gari,naye akatii amri hiyo.
Baada ya kufikishwa katika kituo cha polisi,Malunde alitakiwa kutoa maelezo ya tuhuma ya kosa la uchochozi akidaiwa kuwahamasisha wananchi kuziba barabara.
Baada ya kuandika maelezo hayo askari polisi kitengo cha upelelezi aliyekuwa anamchukua maelezo kwa agizo la mkuu wa kituo cha polisi alimruhusu mwandishi huyo kutoka kituo cha polisi na kwamba kama watamhitaji wamuita kituoni.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka kituo cha polisi,Malunde alisema anatuhumiwa kwa kosa la uchochezi wakati wananchi wakiwa wameziba barabara.
“Nimeandika maelezo baada kuambiwa natuhumiwa na kesi ya uchochezi,kwamba nimehamasisha wananchi waweke mawe na matofali wakati mimi nimefika eneo la tukio kutekeleza majukumu yangu ya uandishi wa habari”,alisema Malunde.
“Nimefika eneo la tukio kuandika habari juu ya tukio lililokuwa linaendelea,nimekuta wananchi wanaendelea kufunga barabara wakiongozwa na mwenyekiti wa mtaa wa Magadula kata ya Ngokolo Diana Ezekiel nikaanza kuwahoji wakasema wamefunga barabara kwa sababu ya vumbi katika barabara hiyo”,alieleza Malunde.
“Wananchi hao walieleza kuwa makubaliano ya mkataba wakati Kampuni ya ukandarasi JASCO anayesimamiwa na halmashauri ya manispaa ya Shinyanga ni kwamba anatakiwa kuwa anamwaga maji asubuhi,mchana na jioni lakini hali imekuwa tofauti kabisa kwa muda wa zaidi ya miezi sita sasa”,alieleza.
Malunde alisema baada ya kumaliza kufanya mahojiano na wananchi alikaa pembeni ili kujua kitakachoendelea na baada ya takribani dakika 10 askari polisi walifika eneo hilo na kuwataka wananchi waliokuwa eneo hilo kuondoa mawe na matofali hayo.
Wakati polisi wakiwa eneo hilo huku wananchi wakiendelea kuondoa mawe hayo,ghafla askari polisi mmoja alihoji kwanini anapiga picha,alipojibu ni mwandishi wa habari aliombwa aoneshe kitambulisho wakati anajiandaa kuonesha ndipo alitokea askari mwingine (OCD) akimtaka apande kwenye gari la polisi anafanya uchochezi.
“Pamoja na kwamba nilieleza kuwa ni mwandishi wa habari na kutaka kuwaonesha kitambulisho cha kazi askari hao waliendelea kunizonga,huku mkuu wa kituo cha polisi ambaye sikuwahi kumuona aliyejulikana kwa jina la Cloud Kanyolota akiamuru nipandishwe kwenye gari la polisi kwamba kwanini nakuwa mbishi,nikauliza kwanini akasema mimi mchochezi,nikaamua kupanda na kuelekea kituo cha polisi wilaya”,aliongeza Malunde.
Mwandishi huyo wa habari baada ya kushikiliwa kituoni hapo kwa takribani masaa mawili kisha kuandika maelezo yake aliruhusiwa kutoka polisi bila dhamana na kuelezwa kuwa endapo watamhitaji watamwambia.
Akizungumza kabla ya kukamatwa na polisi kwa tuhuma ya uchochezi kwa kuwaongoza wananchi kuziba barabara,Mwenyekiti wa mtaa wa Magadula Diana Ezekiel alisema barabara hiyo imekuwa kero kwa wananchi wa eneo hilo hali iliyowafanya wachukue uamuzi wa kufunga barabara hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ngokolo Emmanuel Ntobi alisema mkandarasi anayejenga barabara hiyo hamwagi maji tatizo linalotokana na halmashauri ya manispaa ya Shinyanga kutomsimamia ipasavyo
“Ujenzi wa barabara unaotokana na pesa za benki ya dunia ulianza Tarehe 1 Julai,2016,ulitakiwa ukamilike ndani ya miezi 6 lakini mpaka sasa haujakamilika,mbaya zaidi mkandarasi kamwaga simenti hali ambayo inasababisha vumbi kali na kuhatarisha afya za watumiaji wa barabara hii na wananchi wanaoishi jirani na barabara hii”,alieleza Ntobi.
“Tunalaani kitendo cha jeshi la polisi kumkamata mwandsihi wa habari ambaye akikuwa anatekeleza majukumu yake,lakini pia tunataka jeshi la polisi limwachie huru mwenyekiti wa mtaa wa Magadula,Diana Ezekiel bali wamkamate mkandarasi,lakini pia tunatoa siku tano maji yaanze kumwagwa la sivyo tutaandamana kata nzima”,aliongeza Ntobi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,Simon Haule alisema wamemuachia huru mwandishi huyo wa habari bila masharti.
Hivi karibuni baraza la madiwani la manispaa ya Shinyanga lilitoa azimio kumtaka mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga afuatilie mkataba wa mkandarasi JASCO Investment kumwagilia maji mara tatu kwa siku kwani fedha kwa ajili ya kumwagili barabara ilishatengwa na amekuwa akilipwa.
Ikumbukwe pi kuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro aliwahi kuagiza Mkandarasi JASCO akamatwe kwa kutotekeleza majukumu yake ipasavyo.
ANGALIA HAPA VIDEO
ANGALIA HAPA VIDEO
ANGALIA MATUKIO HAPA CHINI JINSI WALIVYOFUNGA BARABARA
Barabara ya Magadula/Mohamed Trans inayotenganisha kata ya Ngokolo na Ndembezi mjini Shinyanga ikiwa imefungwa kwa mawe na matofali.Hapa ni karibu na ukuta wa kanisa Katoliki la Ngokolo na shule ya msingi Bugoyi B.-Picha zote na Kadama Malunde na Isack Luhende - Malunde1 blog
Muonekano wa barabara
Hili ni eneo jingine ambapo wananchi walifunga barabara hiyo
Baadhi ya wananchi wakiwa katika barabara hiyo wakiwa na mwenyekiti wa mtaa wa Magadula Diana Ezekiel (aliyesimama karibu na bajaji).
Mwenyekiti wa mtaa wa Magadula Diana Ezekiel akitoa maelezo kwa mwandishi wa habari aliyewahi kufika katika eneo hilo,Kadama Malunde kwanini wameamua kufunga barabara.
Mwandishi wa habari Kadama Malunde akichukua maelezo kutoka kwa mwenyekiti wa mtaa wa Magadula Diana Ezekiel
Askari polisi baada ya kufika katika barabara hiyo.
Askari polisi wakiwaita wananchi waje waondoe mawe na matofali hayo
Wananchi waliokuwa karibu na barabara hiyo wakiondoa mawe na matofali baada ya kuitwa na polisi.
Zoezi la kuondoa mawe likiendelea
Askari polisi wakizozana na mwenyekiti wa mtaa wa Magadula Diana Ezekiel kabla ya kumkamata na kumpandisha kwenye gari la polisi,baada ya kumkamata ndipo walimwamuru pia mwandishi wa habari Kadama Malunde apande kwenye gari la polisi.
Kadama Malunde akiwa na kitambulisho chake cha kazi baada ya kutoka kituo cha polisi.
Picha na Kadama Malunde
na Isack Luhende - Malunde1 blog
na Isack Luhende - Malunde1 blog
No comments:
Post a Comment