Friday, August 25, 2017

BALOZI WA CHINA AFIKA OFISINI KWA SPIKA NDUGAI KUMUAGA

Na Lawrence Raphaely - Bunge.

Balozi wa China nchini LU Youqing amefika Ofisini kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai  Jijini Dar es Salaam mapema leo kumuaga baada ya muda wake wa kukaa Tanzania kwisha.

Akizungumza na Spika Ndugai, Balozi huyo alisema kuwa muda wake wa kutumikia kama Balozi wa China hapa nchini umekwisha hivyo hana budi kuondoka ingawa angetamani kuendelea kubaki.Balozi huyo aliongeza kuwa amefurahi kuona kuwa katika kipindi chake chote akiwa hapa nchini uhusiano baina ya Tanzania na China umezidi kukua.

“Ninafuraha kubwa wakati ninaporejea China kuona kuwa uhusiano wetu wa kihistoria umezidi kukua na kwamba kuna ongezeko kubwa la uwekezaji wa China hapa Tanzania na pia tumesaidia katika utekelezaji wa miradi mingi,” alieleza Balozi huyo.

Balozi huyo ambaye amesema kuwa Tanzania ni nchi yake ya mwisho kuhudumu kama Balozi aliongeza kuwa kwa sasa anarejea nchini China na akiwa huko ataendelea kujitikita katika shughuli za kudumisha uhusiano baina ya Tanzania na China.

“Tanzania ndiyo nchi yangu ya mwisho  kuhudumu kama Balozi na nitakaporejea nyumbani (China) nitaendelea kufanya shughuli nyingine ambazo zinalenga kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na China,”  alisema Balozi Youqing.

Kutokana na hilo Balozi Youqing alisema kuwa ingawa  anarejea nchini China lakini yupo tayari kwa Tanzania kuendelea kumtumia kama Balozi wake katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali zitakozosaidia katika kudumisha ushirikiano baina wa nchi zote mbili.

“Nipo tayari kwa Tanzania kuendelea kunitumia kama Balozi wake aliyepo Nchini China, ninawakaribisha kwa mikono yote miwili tuendelee kufanya kazi kwa pamoja,” alisema Balozi huyo.

Kwa upande wake Spika Ndugai alimshukuru  Balozi huyo kwa kazi kubwa ambayo ameifanya akiwa hapa nchini na kumueleza kuwa daima Watanzania wataendelea kumkumbuka kwa kazi nzuri aliyoifanya.

“Mimi binafsi katika kipindi chako ukiwa kama Balozi nimeshuhudia ongezeko kubwa la watanzania wengi tena wa hali ya chini wakisaifiri kwenda China kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibiashara,” alisema Spika Ndugai na kuonegeza kuwa; kupitia fursa hiyo Watanzania wengi wameweza kujiajiri kupitia biashara ya kununua bidhaa toka China na kuja kuuza hapa nchini.

Mhe Spika pia alimshukuru Balozi Youqing kwa uchakapakazi wake katika kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia wataalamu kutoka nchini China.

“Unaondoka lakini utakapojisikia kurudi, sisi kama Bunge na Serikali kwa ujumla tupo tayari kukupokea kwa mikono miwili na kuendelea kufanya kazi na wewe,” alisema Spika Ndugai.

Mbali na hayo Spika Ndugai pia alimuomba Balozi Youqing kuendelea kuwa Balozi wa Tanzania atakaporejea nchini China kwa kuendelea kufanya shughuli ambazo zitasaidia katika kuimarisha ushirikiano baina ya pande zote mbili.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai (kulia) akizungumza na Balozi wa China nchini LU Youqing  anayemaliza muda wake alipofika kumuaga  mapema leo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa masuala ya  Diplomasia na Vyombo ya Habari- Ubalozi wa China Bi. Wang Fang.
Balozi wa China nchini LU Youqing  anayemaliza muda wake akimueleza jambo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai alipofika kumuaga  mapema leo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa masuala ya  Diplomasia na Vyombo ya Habari- Ubalozi wa China Bi. Wang Fang.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai (kulia) akimkabidhi zawadi  Balozi wa China nchini LU Youqing  anayemaliza muda wake alipofika kumuaga  mapema leo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China nchini LU Youqing  anayemaliza muda wake akimkabidhi  zawadi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai alipofika kumuaga  mapema leo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu wa Spika Bw. Said Yakubu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai (kulia) katika picha ya pamoja  na Balozi wa China nchini LU Youqing  anayemaliza muda wake alipofika kumuaga  mapema leo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai akiagana  na Balozi wa China nchini LU Youqing  anayemaliza muda wake mara baada ya kuzungumza nae  mapema leo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam. Picha na Ofisi ya Bunge

No comments: