Tuesday, July 11, 2017

WATUMISHI WA UMMA WALIOGHUSHI VYETI KUCHUKULIWA HATUA ZA KINIDHAMU

Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Bibi. Theresia Mbando akizungumza na watumishi wa umma Tarafa ya Mbagala kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Angellah J. Kairuki (kulia) leo wakati wa ziara yake katika tarafa hiyo  Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam.
------------------------------------------
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) amesema Watumishi wa  Umma walioghushi vyeti watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Mhe. Kairuki alisema hayo katika kikao kazi na watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke,Tarafa ya Mbagala mapema leo.
Mhe. Kairuki alisisitiza kuwa wote  walioghushi vyeti hawapo kazini na wameshafutwa katika orodha ya malipo ya Serikali (payroll) na kuelekeza waajiri kuwafuta wote wasiostahili kuwepo katika orodha ya malipo na wasimsubiri hadi afike katika maeneo ya kazi ili kutekekeza hilo.
“Baada ya zoezi la uhakiki kukamilika, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa walioghushi vyeti kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma” Kairuki alisema.
Aidha, aliwataka waajiri kuhakikisha wanahakiki taarifa za watumishi wapya wanapoajiriwa na wale wanaohamia ili kujiridhisha kama wana vyeti safi.
“Ni wajibu wa kila Mwajiri kuhakikisha kuwa Vyeti vya kila mwajiriwa mpya vinathibitishwa na Mamlaka husika kabla ya kumwajiri na hatimaye kumuingiza kwenye Orodha za Malipo ya Mishahara (Payroll) kupitia kwenye Mfumo wa HCMIS na Mifumo mingine ya mishahara ya kitaasisi.”
Akiongelea watumishi wa umma walioajiriwa na sifa za darasa la saba Mhe. Kairuki alisema kuwa endapo mtumishi aliajiriwa kabla ya tarehe 20 Mei 2004 anastahili kuendelea kuwa katika Utumishi wa Umma, na endapo kajiendeleza abadilishiwe muundo kuendana na sifa za elimu aliyopata, lakini endapo mtumishi aliajiriwa baada ya tarehe 20 Mei 2004 anatakiwa kuwa na sifa ya elimu ya kidato cha nne.
Sanjari na hilo, Mhe. Kairuki alitoa ufafanuzi wa zoezi linaloendelea linahusu kuoanisha taarifa za watumishi na zile za usajili wa Taifa  uliofanywa na NIDA.
“Uhakiki huu utaongeza usahihi wa taarifa za Watumishi nchini, kudhibiti watumishi hewa, udanganyifu wa taarifa mbalimbali zinazomhusu mtumishi, na kutekeleza azma ya Serikali ya kuunganisha mifumo ya kimakakati ya TEHAMA ili ibadilishane taarifa” Mhe. Kairuki alisema.
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar e Salaam Bi. Theresia Mbando alimshukuru Waziri Kairuki kwa kuuboresha Utumishi wa Umma .
“ Nikupongeze kwa namna ulivyoweza kuuboresha Utumishi wa Umma kwa kuwa tunafanya kazi katika mazingira mazuri”  Bi. Mbando alisema na kuongeza kuwa kwa sasa watumishi wa Umma waliobaki kazini wameweza kuziba pengo la watumishi waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi ambao wameondolewa katika Utumishi wa Umma.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais-UTUMISHI

11.07.2017

No comments: