Wednesday, July 12, 2017

WANANCHI WAIOMBA SERIKALI IONGEZE MUDA ZAIDI WA KULIPA KODI YA MAJENGO

Benny Mwaipaja, WFM-Dar es Salaam
Zikiwa zimebaki siku tatu kati ya siku 15 zilizoongezwa na Serikali kwa wananchi kulipa kodi ya majengo bila adhabu, baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameiomba Serikali iongeze muda mwingine zaidi ili watu wote waweze kulipa kodi hiyo bila adhabu kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa zoezi hilo.
Wananchi hao wamemweleza Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alipofanya ziara za kushitukiza katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA-Mtaa wa Kipata-eneo la Mnazi Mmoja na Mbagala mkoani Dar es Salaam
Wamesema kuwa mwamko wa wananchi kulipa kodi ni mkubwa hali iliyosababisha foleni kubwa kila mahali nchini kutokana na uhaba wa watumishi wa TRA pamoja na vitendeakazi muhimu kama vile kompyuta na mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFDs).
Waziri wa Fedha na Mipango Dokta Philip Mpango amewataka Watanzania kuwa watulivu na kuendelea kulipa kodi hiyo huku akiahidi kutatua changamoto ya uhaba wa watumishi pamoja na vitendeakazi ili kuwaondolea adha wananchi waliojitokeza kwa moyo kulipa kodi mbalimbali ikiwemo ya majengo.
Ameahidi pia kwamba Serikali itayafanyiakazi maombi ya wananchi ya kutaka kuongezewa muda wa kulipa kodi hiyo na kwamba watajulishwa wakati muafaka  uamuzi wa Serikali kuhusu suala hilo.
Dokta Philip Mpango amesema kuwa Serikali inafarijika kwa kiasi kikubwa na namna wananchi walivyoitikia wito wa Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Joseph Magufuli unao wataka wananchi walipe kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Amebainisha kuwa watu wanapolipa kodi wanaipa nguvu Serikali ya kuboresha huduma za jamii kwa wananchi ikiwemo elimu, barabara, maji, afya na kuboresha huduma ya umeme hususan vijijini na kulifanya Taifa kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje ya nchi.
Majuma mawili yaliyopita Serikali iliongeza muda kwa wananchi kulipa kodi ya majengo bila adhabu kwa muda wa majuma mawili hadi Julai 15 mwaka huu ambapo siku hizo zitaisha siku ya Jumamosi huku idadi kubwa ya watu ikiwa bado wanahitaji kulipa kodi hiyo.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akiongea na wananchi waliojitokeza kulipa kodi ya majengo katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)-Ilala Mtaa wa Kipata, na kuwapongeza kwa kuitikia wito huo kwa wingi na kuwaeleza kuwa kwa kulipa kodi kutasaidia upatikanaji wa huduma muhimu kama maji, barabara, umeme  na dawa hospitalini.
 Wananchi waliofika katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ilala Mtaa wa Kipata, wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kulia) akiwaelezea namna atakavyoboresha huduma kwa walipa kodi za majengo kwa kuwapa kipaumbele walemavu, wazee, wagonjwa na wasiojiweza. Tukio hili litaenda sambamba na kuwawekea sehemu maalumu ya kukaa wakati wakisubiri huduma.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kushoto) akipokea shukrani na pongezi kutoka kwa Bi. Rose Muyalo, kwa utendaji makini wa Serikali ya Awamu ya Tano na kwa kupatiwa huduma bora kutoka kwa wafanyakazi wa TRA.
  Bw. Obedi Hezron Misoji (kulia) ambaye ni mstaafu akimuomba Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto), kuongeza muda wa zoezi hili la ulipaji kodi ya majengo kwani watu bado ni wengi na Watanzania wameonesha nia yakujitokeza kwa wingi kulipia kodi hiyo.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kulia) akiongea na wananchi waliofika katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ilala Mtaa wa Kipata kulipa kodi za majengo na kuelezea furaha yake namna walivyoitikia wito huo.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto), akiwasikiliza viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ilala Mtaa wa Kipata namna ambavyo wanaweza kukabiliana na changamoto wanazokabiliana nazo katika zoezi hili la ulipaji kodi wa Majengo.  Kutoka kulia ni Meneja Msaidizi Kanda ya Ilala kwa upande wa madeni Bw. Nuhu Ramadhani, Meneja wa Kanda ya Ilala Bw. Abdul Mapembe na Bw. Revelian Kajuna.

 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto), akisalimiana na mmoja wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)- Mbagala, alipotembelea ofisi hizo kujionea namna zoezi la ulipaji kodi ya majengo unavyoendelea.

 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwa katika moja ya ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)- Mbagala na kukutana na Mtoto Salma (aliyembeba) ambaye aliambatana na mama yake (hayuko pichani) kwenda ofisini hapo kulipa kodi ya majengo.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kushoto) akiongea na baadhi ya wazee waliojitokeza kulipa kodi za majengo katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)- Mbagala jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kushoto) akiwapongeza vijana waliojitokeza kulipa kodi ya majengo katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) - Mbagala jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)

No comments: