Wednesday, July 12, 2017

DKT. KALEMANI AZINDUA REA AWAMU YA TATU MKOANI GEITA

Na Greyson Mwase, Geita
Naibu  Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, ametoa siku 13 kwa mameneja wote wa Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO) kuhakikisha wananchi wote waliolipa ada kwa ajili ya kuunganishiwa huduma ya umeme wanaunganishiwa mapema na kuondokana na adha ya kuwepo gizani.
Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo katika kijiji cha Nyijundu wilayani Nyang’hwale mkoani Geita wakati akizindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa mkoa wa Geita pamoja na kumtambulisha mkandarasi atakayetekeleza mradi kwa mkoa huo.
Alisema kuwa, ni haki ya mwananchi  aliyelipia gharama za kuunganishiwa umeme kupatiwa huduma ndani  ya siku saba kama sheria inavyofafanua na kuwataka mameneja kuhakikisha wananchi wote waliokuwa wamelipia huduma za kuunganishiwa  umeme kupata huduma hiyo kabla ya  Julai 25, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani aliwataka mameneja  wa TANESCO  kusogeza huduma karibu na wananchi badala ya wananchi kusafiri  umbali mrefu  kwa gharama kubwa kufuata  huduma za umeme.
Alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuinua  uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha nishati ya umeme ya uhakika inapatikana hususan katika maeneo ya vijijini ili wananchi waweze kujiajiri kupitia viwanda vidogo  vidogo kama mashine za kusaga na kukoboa nafaka, kuchomelea vyuma na kusindika matunda.
Waziri Kalemani alimtaka mkandarasi atakayetekeleza mradi kabambe wa kusambaza umeme  vijijini awamu ya tatu katika mkoa wa Geita kufanya kazi  usiku na mchana ili kukamilisha kazi kwa miezi 16 badala ya kipindi cha miezi 24, na kuwa na nafasi ya kutosha ya kufanya marekebisho madogo kabla ya kukabidhi rasmi mradi kwa Serikali.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Gissima Nyamo- Hanga akielezea Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Tatu, alisema utekelezaji wake katika mkoa wa Geita utahusisha upelekaji  umeme katika vijiji 220 kwa gharama ya shilingi bilioni 78.56 na kuongeza kuwa sehemu ya kwanza ya mradi itatekelezwa na muunganiko wa kampuni mbili  za White City International Contractors Ltd ya Tanzaia na Guangdong Ltd ya  China.
Mhandisi Nyamo-Hanga aliwataka wananchi watakaounganishiwa umeme kukamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao mapema ili wakati mkandarasi atakapofika katika maeneo yao wawe tayari kulipia na kuunganishiwa umeme
Aidha, alihimiza wananchi kutoa maeneo yao kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya kusambaza umeme bila kudai fidia kama mnchango wao kwenye miradi hii ya maendeleo.
 Sehemu ya wananchi kutoka katika kijiji cha Nyijundu wilayani  Nyang’hwale mkoani Geita wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini  Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) alipokuwa akizindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa mkoa wa Geita mapema Julai 12, 2017.
Mbunge wa Nyang’hwale, Hussein Kasu akielezea hali ya  upatikanaji wa umeme katika wilaya ya Nyang’hwale kwenye uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa mkoa wa Geita uliofanyika katika kijiji cha  Nyijundu wilayani humo mapema  Julai 12, 2017.
 Kutoka kulia waliokaa mbele, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati  Vijijini (REA) Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mbunge wa Bukombe,  Dotto Biteko, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga,  Naibu  Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, Mbunge wa Nyang’hwale, Hussein Kasu, wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watendaji kutoka  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati  Vijijini (REA), Wizara ya Nishati na Madini mara  baada ya kumalizika kwa uzinduzi huo.
 Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga akielezea  hali ya upatikanaji wa umeme katika mkoa huo  mbele ya Naibu  Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kwenye uzinduzi huo.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mbunge wa Bukombe,  Dotto Biteko akifafanua jambo kwenye uzinduzi huo.
 Naibu  Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akitoa maelekezo  kwa wakandarasi na watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) (hawapo pichani) kwenye uzinduzi huo.
 Sehemu ya wakandarasi na watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakipokea maelekezo kutoka kwa Naibu  Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kwenye uzinduzi huo.
 Naibu  Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akitoa sehemu ya  vifaa maalum vya Umeme Tayari (UMETA) kama zawadi kwa  sehemu ya wazee wa kijiji cha Nyijundu wilayani Nyang’hwale kwenye uzinduzi huo.
  
Naibu  Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kama ishara ya uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa mkoa wa Geita kwenye uzinduzi huo.
 Naibu  Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akibonyeza kitufe  kama ishara ya  uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa mkoa wa Geita kwenye uzinduzi huo.
 Sehemu ya wananchi na wanafunzi kutoka katika kijiji cha Nyijundu wilayani  Nyang’hwale mkoani Geita wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini  Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) alipokuwa akizindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa mkoa wa Geita mapema Julai 12, 2017.

No comments: