Monday, July 31, 2017

VIONGOZI TUMSAIDIE RAIS KUTATUA KERO - WARIOBA


Na Judith Mhina – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, anahitaji kupata usaidizi wa kutosha kutoka kwa viongozi na hasa wasaidizi  kuanzia ngazi ya nyumba kumi hadi taifa.
Maneno hayo yametamkwa na Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba alipofanya mahojiano na Idara ya Habari – MAELEZO - ofisini kwake Oysterbay Jijini Dar-es-Salaam.
Jaji Warioba ameona kuna udhaifu mkubwa wa kiutendaji ambapo wananchi hawatoi changamoto zinazowakabili mpaka wamuone Rais amefika katika eneo lao, au wanaeleza changamoto zinazowakabili kwa viongozi husika ila, viongozi hawazifanyii kazi, ambapo wananchi wanaamua kuziwasilisha kwa Rais mara wanapomuona.
 “Rais hawezi kufanya kazi peke yake naomba tuimarishe utendaji wetu wa kazi, kama utendaji ungekuwa mzuri suala la makontena kufika hadi bandarini lisingekuwepo, na hata kugundulika kwake kusingefanywa na Rais,” amesema Jaji Warioba.
“Nampongeza sana Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan na  Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa, kwa utendaji wao wa kazi. Viongozi hawa ni wasikivu na wanatekeleza kazi zao bila mihemko kwa kutoa maagizo na maelekezo kwa wahusika ili wayatekeleze”, aliongeza  Mhe. Warioba.
Hivi karibuni, Rais ameona tatizo hilo, la kuachiwa kila jambo ili afanye  wakati kuna uongozi wa serikali, kuanzia ngazi ya nyumba kumi hadi taifa.  Rais amelisema hilo, alipokuwa kwenye ziara katika Mkoa wa Tabora, ambapo mabango mengi yaliyoandikwa na wananchi yakiwa na changamoto mbalimbali na kugundua kuwa viongozi walio wengi hawatatui changamoto hizo. Matokeo yake, Rais anapofika eneo husika, kila mwananchi anataka atatuliwe changamoto yake kitu ambacho hakiwezekani na wala sio sahihi.
Tabia hii haikumpendeza Rais Magufuli, ambapo alipotoa kauli kuwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na watendaji wengine ambao hawatatui matatizo ya wananchi atawaondoa katika nafasi hizo mara moja.
“Endapo nitarudi na kuelezwa kero ambazo mnaweza kuzitatua lakini mkashindwa kufanya hivyo, nitajua kuwa mmeshindwa kufanya kazi yenu kwa ufanisi” alisema Rais Magufuli.
Warioba ameongeza kwa kusema; “Sisi wote tulikuwa viongozi lakini hatukuwahi kuachiwa tufanye kila kitu bila usaidizi wa viongozi katika ngazi zote.
Tanzania ni kati ya nchi zilizojizatiti kwa kuwa na uongozi kuanzia ngazi ya nyumba kumi, shina, kata, tarafa, Wilaya, Mkoa hadi taifa. Kama kweli uongozi wa kila ngazi utajituma kutatua changamoto za wananchi itamrahisishia Rais kufanya majukumu yake.  
Mtakumbuka kuwa enzi za awamu ya kwanza na ya pili, sio kweli kwamba hali ilivyo sasa ni mbaya kuliko awamu hizo. Lakini wakati ule kilichotusaidia ni umoja wetu na mshikamano wa kutatua matatizo yetu kwa pamoja, hatukuachiwa kama viongozi tutatue changamoto za wananchi sisi wenyewe. Amesema Warioba.
Akisisitiza, Warioba amesema; “Iweje leo tumuachie Rais afanye kila kitu mwenyewe naomba sana tumsaidie na kumuunga mkono, hakika ana nia njema na rasilimali za nchi hii. Ni vema kilichofanyika kikaangalia rasilimali zote za nchini na sio wawekezaji wa nje tu hata wa ndani”.
Aidha, kiongozi mwingine aliyeliona tatizo hili ni Waziri Mkuu Msataafu Dkt. Salim Ahmed Salim, ambaye amesema Vijana ni lazima wajue siasa za nchi yao na nini muelekeo wa uongozi wa nchi kwa ujumla. Uongozi ni dhamana unayopewa kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, hivyo ni lazima uwatumikie ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili.
 “Bila kujua historia na siasa ya nchi yako utashindwa kuwatumikia wananchi badala yake utafanya kazi kwa matakwa yako, ambapo itakuwa sio sahihi. Wito wangu viongozi wote msaidieni Rais katika kutimiza wajibu wa Watanzania, msimuache afanye kazi peke yake, sisi sote tumuunge mkono”Amesema Dkt. Salim.
Tangu Rais ateue viongozi mbalimbali ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa, kila kiongozi anajua utendaji wa Rais na nini anataka wafanye. Viongozi wameapa na kupewa miongozo ya utendaji wa kazi zao. Kutokana na Rais kuwa wazi katika hilo nadhani sasa kila mhusika atafanya ipasavyo ili kutatua changamoto kadhaa zinazowakabili wananchi.
Mfano mzuri ni ule uliotolewa na Kamati ya maridhiano ya viongozi wa madhehebu ya dini Tanzania ya kuomba viongozi wengine kuiga utendaji wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, ambaye walimpongeza kwa kutatua kero za ardhi kila mahala hapa nchini. Kiongozi huyo amejitahidi kupunguza kero za watumishi wa ardhi wasio waaminifu kwa kudai rushwa, katika suala zima la kupata viwanja, kupima na kupata hati miliki.   
Hivyo, kila mhusika katika Mkoa, Wilaya, Tarafa, Kata, shina na nyumba kumi anawajibu wa kutatua kero na changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo lake. Iwapo kero ipo nje ya uwezo wa uongozi wako, utashirikiana na ngazi iliyokuzidi kuhakikisha unaipeleka mbele zaidi itatuliwe na kuchukuliwa hatua zinazofaa.
Kiongozi hutumia busara, badala ya kusubiri Rais afike katika eneo lake na wananchi waanze kulalamika, tafsiri yake ni kwamba  hufai kuwepo kwenye nafasi husika, hivyo ni vema ukatafuta kazi nyingine ya kufanya.
Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliliona tatizo hili la wananchi na viongozi wote kuwa ni sehemu ya kulalamika badala ya kutafuta jinsi ya kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili kwa wakati huo baada ya uhuru.
Mwalimu akaliona kama donda ndugu ambalo likiachwa litaambukiza kizazi na kizazi,  hivyo alitafuta dawa na kuja na waraka wa serikali wa kusema “Toa Hoja usipige kelele” akiwa na maana hoja yako itaangaliwa, litafanyiwa kazi na kutolewa majibu , lakini kwa kupiga kelele watu wanaweza kudhani wewe ni mwendawazimu tu na wakakupuuza na tatizo litabaki palepale.       

Mpaka sasa Waraka huu wa Mwalimu Nyerere alioutoa mwaka 1964 una umuhimu na mantiki ya hali ya juu. Watanzania tutoe hoja tusipige kelele.

No comments: