Wednesday, July 12, 2017

UKISTAAJABU YA GAGA, NJOO UYAONE YA KIZOTA

Na  Haji Sunday  Manara

Ehhh!! Haya! Na leo naandika tena? Mazoea mengine bana!!  

Ndio, nimeona niandike ujinga wangu ila safari hi naandika kuhusu suala jepesi la wachezaji kuhama timu kubwa moja kwenda timu kubwa nyingine. Hapa nazungumzia Simba na Yanga, aka mapacha Kulwa na Dotto.

Kiuhalisia hili jambo halikuanza leo,limeanza miaka Dahal. Na ukienda katika historia, zamani lilikuwa linakera zaid pengine kupita zama zetu, sababu miaka ya nyuma kabisa, wachezaji walikuwa wakihama upande mmoja kwenda mwingine sababu za kishabiki zaid kuliko sasa, ambapo sababu za kimaslahi zmechukua nafasi kubwa.

Kihistoria mchezaji wa kwanza maarufu kuhama katika  timu hizi ni wajina wangu Haji Omari....Huyu alikuwa sentahafu mahiri sana wa Yanga, lakini akaja kuhamia Sunderland (Simba). Inaarifiwa kwa kitendo chake cha kuhama jinsi kilivyowakera wanayanga,wakaamua kuhakikisha hachezi Simba. Haji akaishia kuuza soda pale Ilala Stadium (Karume).

Baada ya hapo kulikuwa na mtikisiko mkubwa katika  medani ya kabumbu nchini, baada ya anaetajwa kuwa kiungo bora nchini kuwahi kutokea miaka ya 19960  na mwanzoni mwa 1970 ,Gilbert Mahinya kuihama klabu ya Simba na kujiunga na Yanga. Kiungo huyo inatajwa kuwa alinyan'ganywa hadi fenicha alizonunuliwa na Simba,hali iliopelekea kuacha gumzo kubwa nchini. Gilbert anatajwa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Pan, Pamba na timu ya Taifa,Mohamed Rishard Adoph, kuwa ndie half back six bora kuwahi kumuona nchini.

Miaka ya 70 suala la kuhama halikuziacha salama klabu hizi. Kwanza kwa kiungo Adam Juma akihama kutoka Simba kwenda Yanga. Huyu alidhihakiwa kuwa alihama Simba kufuata safari ya Yanga iliolikwa kwenda Romania, ingawa baadae nayo Simba ilikwenda nchini Poland kupitia Italy miaka hyo.

Miaka hii pia ilishuhudia kipa bora kupita wote nchini kuwah kutokea Athumani Mambosasa nae akienda Yanga kwa kipindi kifupi, sambamba na namba ten ya Afrika Maulid Dilunga "Eusebio" nae akihamia Simba toka Yanga - ingwa hawa hawakudumu sana na klabu zao mpya.

Mtikisiko kwa miaka hyo ni kwa Ezekiel Greyson "Jujuman",mzaramo wa Kisarawe na baba wa muigizaji mahiri wa filamu Aunt Ezikiel, huyu alihama Yanga kuja Simba. Kiungo huyo aliye mbele ya haki kwa sasa,alichezea Yanga wakati ikipokea kipigo cha kihistoria cha goli Sita kwa bila mwaka 1977. Jujuman alikuwa akicheza kiungo wa ushambuliaji.

Miaka ya themanini haikuwa na vbweka hivyo sana. Zaidi ya Omary Hussein "Kevin Keegan wa Yanga,kama walivyokuwa wakimwita washabiki wao,kuja kucheza Simba mwishoni mwa miaka hiyo. Simba wakambatiza jina la One Ten - aina ya gari zilizokuwa kwenye chati miaka hiyo.

Ila kwa faida ya wasomaji, mwanzoni mwa miaka hyo almanusura katibu mkuu wa sasa wa Yanga,Charles Boniface Mkwasa kujiunga na Simba. Mkwasa au Master kama alivyokuwa akiitwa na wafuasi wake,alishasajili Simba, ila mwenyekiti wa FAT (TFF )wakati huo Mzee Said El-Maamry akampa fursa ya kuchagua timu gani anayotaka kuichezea. Ndipo kiungo huyo mtaratibu akaichagua timu yake anayoishabikia ya Yanga.

Pia full back kutoka Pamba Yusuf Bana nae aliingia katika  mtego kama huo, wakati akihama huko kuja Dar, Bana alijisajili timu zote mbili, ila FAT ikamuidhinisha kuchezea Yanga, hali iliyopelekea kubadilisha jina kwa kuongeza jina Ismail. Akaitwa Yusuf Ismail Bana.

Vurugu hasa zilianza miaka ya 90. Kwanza zikianzishwa na marehemu Syllesaid Mziray kocha msaidizi wa Simba,ambae alijiunga na Yanga katikati ya msimu wa 1990. Tena mara baada ya mechi kali ya mwezi May,ambapo Simba iliibwaga Yanga kwa goli moja kwa sifuri, kwa shuti la yadi 45,toka kwa beki Mavumbi Omari.
Mziray alikuwa kocha wa kwanza rasmi kuhama toka kwa watani hao wa jadi,ambao baadhi ya wasiojua huwaita mahasimu,

Mziray akiwa kocha aliifunga Simba alivyotaka, huku ikichagizwa na mfadhili bepari Abbas Gulamali, ambapo waliifunga Simba mara tano mfululizo, ikianzia kipigo cha 3-1 mwaka huo, kabla ya kuwafunga mara nne tena katika  msimu wa 1991, hadi pale Simba walipoifunga Yanga kule Zanzibar kwenye fainali ya Ubingwa wa Afrika mashariki na kati katika michuano ambayo leo ni Kagame Cup.

Mziray aliweka historia kubwa sana kipindi hicho,ingawa kwa maneno yake mwenyew kwangu miaka ya baadae aliwahi kunitamkia kuwa yeye ni mnazi wa Simba, na kwamba pale alikuwa kazini tu. Super coach Mziray mtaalam wa soka ya matumizi ya nguvu, baadae alirejea kufundisha klabu yake aliokuwa anaishabikia.

Hapa nimtaje Mkuu wa mkoa wa Manyara, kocha Joel Bendera ambae naye aliwahi kuzifundisha timu hizi mbili, lakini yeye akifundisha zaid pale zilipokuwa zikiwakilisha nchi katika mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na CAF.


Hapa niwajuze Kocha Bendera akisaidiana na marehemu Ayoub Mohamed,waliiwezesha Simba kuweka rekodi pekee duniani,ya kushinda goli tano bila ugenini,baada ya kufungwa nyumbani goli nne kwa bila,dhidi ya klabu ya Mufurila Wonderes ya Zambia, Kiukweli hii ni rekodi ya dunia. Ingawa sijui kwa nini haijawekwa katika  vitabu vya Guinnes book. Mechi hii ilikuwa ni ya klabu bingwa barani Afrika, na ilichezwa mbele ya Rais wa Zambia wakati huo Dokta Kenneth kaunda aka KK.

Tukiachana na makocha hao,mwaka huo beki mwenye umbile dogo lakini mahiri Deo Njohole au OCD,alivaa jezi ya Yanga huku akiwa mchezaji wa Simba. Deo alivaa jezi hyo siku Yanga ikicheza na Kikwajuni ya Zbar, na alifungiwa kucheza soka baada ya kusajiliwa na timu zote hizo mapacha.

Kivumbi na jasho kilikuwa mwaka uliofata,1991. Simba ilipoteza nyota wake watatu kwa mpigo. Narudia 'NYOTA', Zamoyoni Mogella, Method Mogella, na Hamis Thobias Gaga. Hawa walianza kuichezea Yanga kule Zanzibar kwenye klabu bingwa Afrika mashariki na kati 1992, na katika hali ya kawaida ungedhani Simba ingeyumba. Lakini ajabu haikuwa hvyo. Ikiwatumia nyota wapya kama Hussein Marsha,George Masatu,Mohamed Mwameja, Kasongo Athmani, Fikiri magoso, Damian kimti, Michael Paul, George Lucas, Mnyama aliweza kumfunga Yanga kule Visiwani na kuchukua kombe hilo tena,ambalo walilitwaa mwaka 1991.

Na hapa ndio ule msemo wa watu wa Soka....klabu ni kubwa kuliko mchezaji unapotimia.

Yanga pia ilishawahi kutimua timu nzima mwaka 1976, wakiwemo wazee wangu, Kitwana na Sunday Manara, Maulid Dilunga, Kilambo,Chitete na wengine wengi. Ingawa uamuzi ule uliacha doa na historia mbaya kwao,kwani ndipo walikula 6-0 na kuifanya Simba ichukue ubingwa kwa miaka mitano mfululizo.

Kikosi cha kina Masha na Masatu ndio kilifika fainali ya Caf, medali pekee kubwa katika soka nchini kuwahi kuvaliwa. Wachezaji hao wanaungana na Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu kuwahi kuvaa medali zinazotolewa na Shirikisho la soka Afrika, CAF. Kina Samata wao walivaa medali za ubingwa wakiwa na TP Mazembe ya Congo DRC.

Sina hakika msomaji hadithi yangu kama unajua kukosa huruma ya Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ally Hassan Mwinyi, wachezaji Kenneth Mkapa wa Yanga, Mwameja na Michael Paul almanusura wafungiwe baada ya kujisajili timu zote mbili!! Hiyo ilikuwa 1993. Lakini mzee Ruksa aliwaombea msamaha kwa waziri wa michezo wakati huo Profesa Philemon Sarungi,ambae aliwaagiza FAT  wawafungulie nyota hao wakubwa kwa kipindi hcho.

Godwin Aswile na Thomas Kipese nao walihama Yanga kuja Simba msimu huo,na walivaa medali hzo za CAF,ambazo ziliwawezesha kujipatia magari aina ya Toyota Corolla toka kwa mfadhili wa Simba wakati huo,Azim Dewji. Simba ni timu pekee nchini kuwahi kuwapa wachezaji wake wote magari kwa mpigo,,jambo ambalo halijawahi kufanywa na klabu yoyote nchini kwa miaka 56 ya uhai wa Taifa hili liliojaa wapiga domo.

Ninazo pia kumbukumbu za kiungo mnyumbufu Athaman China ambae alikuwa nyota wa Yanga,lakini baadae akajiunga na Simba 1994,akitokea Ughaibuni alipokuwa akicheza soka ,

Sololist Dally Kimoko ndio jina la utani alilokuwa akitumia Mwanamtwa Kihwelo, ambae nae kuhama hakukumuacha salama. Yeye alihama msimu wa 1994, Mtwa ni ndugu wa beki mahiri wa zamani wa Simba Mussa kihwelo, na pia Julio au Jamhuri kihwelo, Muhesa na Muhehe ambao nao walikuwa wachezaji walioacha alama nchini. Dally Kimoko yeye alihama Yanga kuja Simba.

Steven Casmir Nemes na Said Mwamba Kizota nao katika msimu wa 1995 wakajiunga na Simba kutokea Yanga. Nimewah kuwapenda nyota wengi kiuchezaji nchini,,ila Kizota na Gaga niliwazimia sana. Miguu yao ilikuwa ni kuliko almasi. Wakati fulani hivi nilikuwa naamini Kizota alikuwa anacheza huku anaweka nta miguuni,ukizingatia anatokea mkoa wenye kuzalisha Asali kwa wingi.

Siku moja miaka ya nyuma kdogo nilikuwa naongea na Charles Boniface Mkwasa kuhusu masuala mbalimbali ya mpira, akaniambia wachanganye Gaga na Kizota, basi hawajamfikia baba yako Sunday hata nusu. Hapo niliogopa kdogo,,lakini majuzi tu Waziri Mwakyembe alimuita Messi wa zama hizo. Nasikitika macho yangu hayakujaaliwa kumuona mzee wangu katika  ubora wake uwanjani. Nilikuwa mdogo mno, ingawa ni mpekepeke wa kuuliza historia na kusoma majarida ya zamani.

Hebu turejee katika  mada kuu. Jina la kocha Nzoyisaba Tauzani walikumbuka? Mrundi huyu nae anaingia kwenye historia ya kuhama, ingawa yeye hakutokea Yanga moja kwa moja kuja Simba, lakini nae hakuachwa salama katika  mkumbo huu maarufu kama iba uibiwe.

Unadhani ntawasahau Edibiy Jonas Lunyamila na Mohamed Hussein Mmachinga? La, Hasha! Hawa nao mwanzoni mwanzoni mwa karne hii nao waliasi toka Yanga kuja Simba. Eddy kwa vigezo vyovyote vile ndio winga bora niliowahi kumuona nchini kwa macho yangu...achana na hao niliohadithiwa, sijui kina Leonard Chitete na Willy Mwaijibe. Lunya kwa macho yangu nimeshuhudia akiwakalisha chini kwa chenga kali mabeki wafuatao,David Mwakalebela, Kassongo, Aziz Nyoni, Said korongo, Deo mkuki, Mohd Mtono na ukitaka hilo nenda kamuulize nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Uganda, Paul Hassule jinsi alivyompindua pindua kama chapati pale Nakivubo Stadium 1993,wakati Yanga ilipotwaa ubingwa wa Kagame cup (ndio linavyoitwa kwa sasa).

Ikumbukwe Yanga walikabidhiwa na mfadhili wao Seti ya TV inch 18, toka kwa marehemu Gulamali, mwaka ambao Simba ilikabidhiwa ndinga mpya toka Toyota.

Ohhh kichwa kimechoka nini? Akida Makunda nae hakubaki salama na iba uibiwe. Huyu bwana alihama Simba kwenda Yanga pia.

Mwaka 1998,Yanga ilipata fursa ya kucheza fainali za ligi ya mabingwa, ikawaazima nyota watatu kutoka Simba, Beki bora wa kushoto nchini Alphonce Modest,  kando ya Mohamed Kajole,Mohamed Chuma, Ahmed Amasha na Kenneth Mkapa, Kiungo mtundu Shaban Ramadhan na mshambulizi aliyecheza miaka mingi zaid ligi ya Tanzania kando ya Kitwana Manara na Madaraka Selemani, Monja liseki.

Kitendo hiki kilichofanywa na Simba ni uungwana bora michezoni kupita kitendo chochote kufanywa katika  historia ya mapacha hao watukutu. Mimi nnaloamini mwakani wakati Simba ikirudi kwenye caf.com, Yanga itawaazima wachezaji Simba, nikiamini Simba itafuzu kwa hatua za makundi, huku wenzetu kama kawaida yao.

Nikimrejea Lunyamila nae ana historia kubwa ya pengine mchezaji pekee nchini kucheza hatua za makundi mara mbili za ligi ya Mabingwa Afrika, akianzia na Yanga 1998, kisha Simba 2003.

Jembe Ulaya na Yusuf Macho iba uibiwe nao haikuwacha,ingawa uhamaji wao ni tofauti kdogo. Huku wote wakija Simba baada ya kutokea nje walikoenda kujaribu kucheza soka la kulipwa,awali walikuwa wakiitumikia Yanga.

Jina kamili la Jembe Ulaya ni Bakari Malima, ambaye ni mpwa wa sentahaf wa kimataifa wa zamani nchini na klabu za Simba na Cosmopolittan Mohammed Bakari Tall. Timu ya pili kuchukua ubingwa baada ya Sunderland (Simba) Cosmo walichukua ubingwa 1967,huku Simba ikiitangulia mwaka 1966.

Kipa bora nchini kwa wakati wake Tanzania one Juma Kaseja au Juma K Juma unamuachaje katika mkumbo huu wa kuwatumikia mafahari hawa wawili nchini,  tena yeye alitoka unyamani kwenda bondeni , au Kiggi Makassi na Amiri Maftah unadhani walibaki salama? au Ephrahim Makoye? hawa nao iba uibiwe iliwakumba. Wote hao walikuwa Yanga baadae wakaja Unyamani.

Au mkumbo huo wa iba uibiwe utawaacha vipi, watu kama, kipa Yaw Berko , Rashid Gumbo, Nurdin Bakar, ambao kwa nyakati tofauti walitoka timu moja kwenda upande wa pili kwa mapacha hawa wawili nchini - Simba na Yanga

Loooh masikini  Athman Iddi 'Chuji' ni kweli anastahili kutokuwemo kwenye ligi kuu nchini kwa sasa? Hebu zifikirie zile pasi zake kama rula zinazogawa uwanja!! ahh yote maisha, ila nae alihama Simba kwenda Yanga na kuna kipindi alirudi Simba kabla ya kurudi alipopapenda zaid,Yanga. Doyi Moki,nae aliwah kuhama Yanga kwenda kudakia Simba.

Wasso Ramadhani, Mrundi aliyekuwa namba tatu mahiri wa Simba nae alihamia Yanga pia, ingawa tunajua ni mnazi mkubwa wa unyamani. Deogratius Munishi Dida, Ally Mustafa Barthez, Kevin Yondan na Kessi nao wote kwa vipindi tofauti waliwah kukipiga na Simba na kwa sasa wapo Yanga.

Kuna na yule Diego wa kiganda, mwe mwe mweh!! Hamis Kiiza!! nae alikuja kucheza Simba akitokea Yanga, ingawa ni dhambi ya kuhitaji utubu kwake kutumia jina hili la Aramando, Sambamba na mwanasoka bora wa kigeni kuwah kucheza nchini Emmanue Okwi. Hawa wote washawahi kuvaa jezi za mapacha hawa, na hapa nimpe heko Okwi aliondoka kwa heshma Simba na anarejea kwa heshma ile ile.

Niliwasahau hata hao??......

Na safari hii Ibrahim Ajibu ambae sijawah kukosa kuamini kuwa ana kipaji halisi cha soka nae kajiunga na Yanga. Ndio binafsi imeniuma kwa kuwa naamini angepata fursa zaidi akiwa Simba, ila mwisho wa siku uamuzi wa maisha ya mtu hufanya yeye mwenyewe, na kwa kuwa Ibra ni mtoto wa mjini sijui kama msomaji umemsikia kasema lolote baya au zuri kuhusu Simba. Hii inampa fursa ya kutochukiwa na wanazi wetu, tofauti na vjana wengine wanaohama huku midomo ikiwa wazi, wanaoshindwa kuweka akiba ya maneno, wakisahau vilabu hivi ni vikubwa na vina rasilimali watu kila pembe ya nchi.

Rai yangu kwa wachezaji ni kuwa binadam kuhama huzuiwi ila uweke akiba. Yasije kukuta kama marehemu Haji Omari. mcheza mpira hupaswi kuwa msemaji, zaidimpira uwe miguuni mwako na sio kinywani. Kazi ya usemaji mtuachie wenyewe, hii ni taaluma kama zilivyo taaluma zenu.

Mwisho
Niwaombe wanazi wenzangu, nimejaribu kuwapa historia hii fupi ili mjue suala la mchezaji kuhama ni jambo la kawaida,limeanza miaka Dahal nyuma,na halitaisha kamwe. Muhimu sisi washabiki tuwe na uvumilivu...Ikitokea kwa Yanga kama ilivyokuwa kwa Simba mvumilie tu, ndio *IBA UIBIWE HYO*,

De la Boss

No comments: