Serikali imeziasa taasisi za umma zinazoshughulikia viwango nchini kufanya kazi kwa ushirikiano ili kupunguza urasimu na kujiruidia kwa majukumu vitu ambavyo vinapelekea kukuza gharama za uwekezaji nchini.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano uliowakutanisha watendaji wakuu wa mashirika ya viwango nchini jana Jijini Dar es Salaam kujadili uboreshaji wa namna ya kufikia viwango vya bidhaa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof Adolf Mkenda amesema kuboresha na kurahisisha mazingira ya uwekezaji ndio kipaumbele cha sertiukali.
Mkutano huo ambao uliandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) unatokana na mikutano ya wadau iliyofanyika awali kwenye mikoa ya Arusha, Mtwara na Dar es Salaam chini ya ufadhili wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ambapo wadau mbalimbali walipata fursa ya kutoa maoni juu ya uboreshaji wa sekta ya viwango nchini.
“Taasisi za serikali za viwango zinafanya kazi nzuri, lakini kuna urudiwaji wa majukumu ambao unafanya mazingira ya uwekezaji kua magumu,” alisema Prof Mkenda.
Alisema ipo haja ya kuweka pamoja miundombinu ya kudhibitisha viwango na kwamba TBS iongoze mchakato huo kwa kuwa wao ndio chombo kikuu cha udhibiti wa viwango nchini.
“Katika utekelezaji wa jambo hili, taasisi zetu lazima zihakikishe kwamba tozo zao haziwi mzigo kwa wawekezaji na wajasiriamali na suala la kukusanya mapato kamwe lisiwe lengo la mashirika ya viwango nchini,” aliwaasa watendaji hao.
Pia alionya kwamba taasisi hizo zisijisikie ufahari kutoza faini kwa makampuni yanayofanya makosa kuhusiana na viwango na badala yake wajikite katika kuwapa wawekezaji ushauri wa namna ya kuhakikisha kwamba wakaiti wote wanazingatia viwango.
“Hatutaki kucheza na suala la ubora na suala hili halina mjadala lazima lizingatiwe, lakini tusijikite kwenye kuweka mazingira magumu na badala yake tuboreshe mazingira ya uwekezaji,” alisema.
Prof Mkenda pia alirudia kusema kwamba serikali haitabishana na wataalamu katika masuala ya viwango vya bidhaa zinazozalishwa ndani na nje ya nchi.
“Naendelea kusisitiza kwamba serikali haitaingilia mamlaka ya taasisi za viwango, lakini pia taasisi zinalojukumu la kufanya kazi kwa uadilifu na uhuru bila kumuonea au kumkomoa mtu,” alisema.
Mkurugenzi wa TBS wa Upimaji na Ugenzi, Bi. Agnes Mneney alisema kwamba TBS na taasisi nyingine zitahakikisha kwamba maagizo ya Katibu Mkuu huyo yanafanyiwa kazi ili kuhakikisha kwamba nia njema ya serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini inafanikiwa.
“Napenda kuwaomba wawekezaji na wajasiriamali wabadilishe mtizamo wao juu yetu, wajue kwamba sisi tuko hapa kwa ajili ya kuwasaidia na kamwe wasijishauri wanapokua na tatizo lolote waje kwetu sisi tupo tayari na tunajisikia fahari kuawahudumia,” alisema.
Bi. Mneney alisema kwamba wadau mbalimbali waliohojiwa kwenye mikoa ya Tanga, Arusha, Mtwara na Dar es Salaam wamesema kwamba kukosekana kwa sera ya viwango nchini ni kikwazo katika kuimarisha na kurahisisha mchakato wa kupata ithibati ya taasisi za viwango.
“Habari njema ni kwamba tayari serikali ipo kwenye mchakato wa kuitengeneza sera ya viwango nchini na kukamilika kwake kutaboresha kwa kiasi kikubwa mazingira uwekezaji na kurahisisha mchakato wa kupata ithibati ya viwango,” alisema.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Huduma za Mikoa wa Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO), Bi. Joyce Meru alisema kwamba taasisi yake tayari imeanza kufanya kazi kwa kushirikiana na TBS pamoja na taaisi nyingine za viwango nchini katika kurahisisha mchakato wa wajasiriamali kubata ithibati ya viwango vya bidhaa zao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini, Bw. Godfrey Simbeye aliipongeza serikali kwa nia yake nyema ya kuboresha na kuimarisha sekta binafsi nchini.
Alisema kwamba adhima hiyo ya serikali ni lazima iungwe mkono na taaisi zinazohusika na viwango nchini ili kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kukuza sekta binafsi.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo kwenye mkutano uliowakutanisha watendaji na wakuu wa mashirika ya viwango nchini ambapo aliwataka kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuchochea uwekezaji. Kushoto ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ugenzi wa TBS na kulia ni Meneja wa Viwango wa TBS, Bi Mary Meela. Mkutano huo ulifanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya watendaji wakuu wa mashirika ya viwango nchini wakiwa kwenye mkutano uliofanyika jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (wa pili kushoto)akibadilishana mawazo baadhi ya wakurugenzi mara baada ya kufungua mkutano uliowakutanisha watendaji na wakuu wa mashirika ya viwango nchini ambapo aliwataka kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuchochea uwekezaji. Kushoto ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ugenzi wa TBS na wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye. Mkutano huo ulifanyika jana Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment