Sunday, July 9, 2017

NDOTO YA MWALIMU YATIMIA, LUGHA YA KISWAHILI LULU YA AFRIKA

Na Judith Mhina - MAELEZO

Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muasisi aliyeenzi lugha adhimu na tamu ya Kiswahili na anastahili tuzo maalum kwa kutambua umuhimu wa lugha  hiyo katika kuleta umoja, mshikamano, na maendeleo barani Afrika.

Mwalimu kwa kutambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili, alianza kuweka mfumo wa matumizi ya lugha hiyo katika utendaji wa serikali, jamii nzima ya Tanzania na Umoja wa Afrika. Aidha, sera za Tanzania za kushiriki katika kupigania Uhuru wa nchi kadhaa za Afrika na uwepo wa wakimbizi nchini kwa idadi kubwa imewezesha lugha hii kuvuka mipaka na kuenea kote kusini mwa Afrika.

Mwalimu amepata wapiganaji mahiri wa lugha ya Kiswahili ambao wapo wengi, lakini kwa uchache makala yangu itaangazia viongozi yaani, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, na Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chissano, Marais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, Rwanda, Paul Kagame, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila na Jemedari wa kuenzi lugha ya Kiswahili anayeifanya lugha hii kuwa Lulu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli. 

Mtakubaliana nami mchango wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi katika kutumia lugha ya Kiswahili fasaha, katika shughuli zote za Serikali na za kijamii zilisukuma mwamko wa gurudumu la kiswahili kusonga mbele haswa kwa wale wanaodhani lugha za kigeni ni bora kuliko lugha yao.

Mwinyi, alipata ushirikiano wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kutoka kwa Marais walio wengi wa Afrika Mashariki ambao kwa njia moja au nyingine walikaa Tanzania wakati wa kupigania uhuru wa nchi zao au kama wakimbizi wakati wa machafuko katika nchi husika.

Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhesimiwa Joachim Arbeto Chisano ni kati ya wapigania uhuru ambao waliishi nchini Tanzania kwa miaka kadhaa na kufanikiwa kufahamu Kiswahili, alithibitisha hili alipohutubia Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika kwa Kiswahili kwa mara ya kwanza alipokuwa akifunga mkutano huo na kumaliza muda wake wa kuwa mwenyekiti wa Umoja huo Julai 2004 jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Amini usiamini huu ukawa ni mwanzo wa lugha za kiafrika kutumika katika mkutano mkubwa wa viongozi wa Umoja wa Afrika yaani Kiswahili ambapo Mwalimu Nyerere alilitamani siku zote kwa kusema: “Sio kama lugha za kigeni ni nzuri kuliko za kwetu bali ukoloni mamboleo ndio umetufikisha hapa”

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ambaye ameishi na kusoma Tanzania, anafahamu lugha ya Kiswahili na mara zote anapokuwa Tanzania mara nyingi hutumia lugha adhimu na pendwa ya Kiswahili kuonyesha ubora na umuhimu wa lugha hiyo katika masuala ya serikali, siasa, kijamii, udugu na katika ujirani mwema.

Rais Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pia ni miongni mwa wasomi na walioishi Tanzania kwa miaka mingi, ambapo Kiswahili chake hakina tofauti na Mtanzania yeyote kwa ufupi kama humjui utasema huyu Mtanzania ametoka wapi huku Kongo – DRC.

Rais Kabila amekuwa akipendelea kutumia lugha hiyo adhimu yenye utajiri wa maneno, nyepesi kujifunza na kueleweka kutokana na matamshi yanaelekeza jinsi ya kutamka silabi moja kwa moja tofauti na baadhi ya lugha ambazo matamshi huwa yanapishana na maandiko ya lugha husika.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame ni mtaalamu mzuri wa lugha ya Kiswahili ambaye ameipamba lugha hiyo kwa kuona umuhimu wa elimu itolewayo nchini kwake, ijumuishe lugha ya Kiswahili kama somo, ili kuwaunganisha Wanyarwanda na wanajumuia ya Afrika Mashariki kwa ukaribu zaidi.

Kagame anastahili pongezi kwa kuweka mitaala ya Kiswahili na kutoa fursa kwa walimu kutoka Tanzania,  kufundisha lugha hiyo tangu shule za msingi, sekondari hadi Chuo Kikuu. Rais huyo ametambua njia rahisi ya kuwaunganisha wana Jumuia ya Afrika Mashariki, aghalabu atumie filosofia ya Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Nyerere kwa kuleta mshikamano, umoja wa wananchi katika kunufaika na soko la pamoja la Jumuia na kuleta maendeleo kwa ujumla. 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila ni mdau mkubwa wa lugha ya Kiswahili ambapo amewezesha wafanyabiashara na wanamuziki wengi kutoka nchini kwake wanaongea lugha ya Kiswahili na kuiimba kwa ufasaha. Kama tujuavyo muziki ni tasnia muhimu sana katika upelekaji wa ujumbe aidha, wa kuunganisha au kubomoa, hivyo lugha ya Kiswahili ikitumika vizuri katika mataifa ya kiafrika kama ilivyo sasa tunafanya biashara na kuendeleza tasnia ya muziki kwa faida ya nchi zetu.

Kwa kuwa nimeitaja tasnia ya muziki japo sio kiongozi wa nchi, ni vema nikaeleza umuhimu wake katika matumizi ya lugha yetu ambaye ni mwana Diplomasia wetu kupitia muziki Naseeb Abdul au kwa jina maarufu Diamond Platnum. Mwanamuziki huyu ni miongoni mwa wasanii wanaopenyeza lugha ya Kiswahili katika nchi zote ambazo muziki wake unapigwa. Mfano nitapenda kuwa shuhuda kwa kuonyesha wanamuziki kutoka nchini Nigeria anaoshirikiana nao katika kuimba nyimbo zake au zao na kufanya Kiswahili kitumike sana katika muziki wa Afrika Magharibi.

Binafsi nimekutana na Wacameroon waliofika nchini kwa masuala ya utalii nikashangaa wanapenda sana nyimbo za Naseeb Abdul na kupata wasaa wa kuchambua maneno anayoimba kwa Kiswahili na wanaelewa maana yake, hivyo ni vema balozi huyu akatambua mchango wake  wa lugha kwa ufasaha na usahihi katika uimbaji na kufika ujumbe utakaochangia kuleta umoja, mshikamano na maendeleo barani Afrika. Hii ina maana Naseeb Abdul atakuwa ni mwalimu mzuri wa lugha ya Kiswahili.

Msumari wa mwisho katika wapiganaji na viongozi wa lugha ya Kiswahili katika makala yangu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli anavyoithamini na kuijali kwa hali ya juu lugha ya Kiswahili. Rais ameleta msisimko wa pekee na kuwafanya hata viongozi wengine barani  Afrika ambao walikuwa wanaona lugha ya Kiswahili “si mali kitu iwe mali kitu”.

Pengine viongozi hao wametambua filosofia ya Mwalimu Nyerere ya kuleta umoja na kuunganisha wananchi kwa kutumia lugha, kuwa na uelewa wa pamoja na masikilizano katika nchi, pia katika kunufaika na soko la pamoja la Jumuia na kuleta maendeleo kwa wananchi, ambapo Rais Magufuli amelitambua hilo mapema.

 Magufuli amekuwa akitumia muda wake wote katka kuwatumikia wananchi wa Tanzania, kila mara  afanyapo chochote kile, huwaita wanahabari na kuhakikisha tukio hilo analiwasilisha kwa lugha ya Kiswahili ili kueleweka kwa Watanzania wote. Hii inafanya Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ya uwazi    zaidi pia, kueleweka kwa wananchi wote nini anafanya, hili ni suala muhimu sana katika uongozi bora.

Hakika mwenye macho haambiwi tazama, utakubaliana nani Rais amepaisha lugha ya Kiswahili kitaifa na kimataifa kwa uamuzi wake wa kutumia lugha ya Kiswahili, kila anapokwenda iwe kwenye mikutano ya taifa au ya kimataifa, hivi karibuni pale Addis Ababa Ethiopia alihutubia kwa Kiswahili.

Aidha, kutokana na utendaji wa Rais na  Serikali ya Awamu ya Tano uliotukuka, kazi zote anazofanya husambaa dunia nzima na kila kiongozi anayeifikiria Tanzania kwa sasa anaona umuhimu wa kujua lugha ya Kiswahili kwa kuwa Rais ameishikia bango na ndiyo anayoitumia kuwafafanulia jambo wananchi.

Matokeo ya bango la Rais Magufuli kutumia lugha ya Kiswahili imezaa ajira lukuki za kufundisha lugha hiyo nchini Ethiopia, Rwanda, Afrika ya Kusini, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambazo ni rasmi. Pia kuna ajira za kufundisha lugha ya Kiswahili sehemu mbalimbali duniani kwenye vyuo vya kimataifa ambapo Watanzania wako huko hizi ni zile ambazo sio rasmi.

Huu ni uthibitisho tosha kuwa Mwalimu Nyerere alilitambua hili na hakika amepata wapiganaji sahihi wakiongozwa na Dkt Magufuli, hakika wanastahili pongezi na daima wanakuenzi,   “Pumzika kwa Amani Mwalimu”.
Lugha ya Kiswahili kwa sasa inatumika katika nchi zote za Afrika Mashariki, Kati na Pembe ya Afrika, yaani Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Malawi, Burundi, Somalia, Msumbiji, Zambia, visiwa vya Comoro na Mashariki mwa Kongo. Hivyo zaidi ya  watu milioni 150 kwa sasa wanaongea Kiswahili hii ni neema kwa Tanzania.

Azimio la kuteuliwa kwa Lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi na ya kazi ya Umoja wa Afrika lilifanyika huko Durban, Afrika Kusini tarehe 9 – 11 mwezi Julai mwaka 2002 wakati wa kikao hicho chini ya Uenyekiti wa Rais Levy Mwanawasa (aliyekuwa Rais wa Zambia)

No comments: