Balozi wa mchezo wa mpira wa kikapu nchini, Jokate Mwegelo akikabidhi bendera ya Taifa kwa mchezaji Chipukizi, Jesca Ngaise (katikati) wakati wa hafla fupi iliyofanyika kwenye kituo cha michezo za Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park. Anayeshuhudia zoezi hilo ni Kocha maarufu wa mpira wa kikapu Tanzania, Bahati Mgunda.
Balozi wa mchezo wa mpira wa kikapu, Jokate katika picha ya pamoja na baadhi ya wachezaji chipukizi wa mpira wa kikapu kwenye viwanja vya JMK Park.
Balozi wa mchezo wa mpira wa kikapu, Jokate akisalimiana na wachezaji chipukizi wa mpira wa kikapu kwenye viwanja vya JMK Park.
Baba Mzazji wa Jesca, Julius Ngaise akizungumza
………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu
Balozi wa mchezo wa mpira wa kikapu nchini, Jokate Mwegelo ametoa rai kwa wasichana na wazazi kuwaruhusu watoto wa kike kushiriki katika michezo mbalimbali ili kukuza vipaji na kujiingizia kipato.
Jokate alitoa rai hiyo wakati wa kukabidhi bendera kwa mchezaji chipukizi wa mpira wa kikapu nchini, Jesca Julius Ngaise ambaye anaondoka leo kwenda nchini Afrika Kusini kushiriki katika mafunzo ya juu mchezo huo yatakayoendeshwa na makocha wa kimataifa wa ligi ya NBA ya Marekani.
Amesema kuwa Jesca ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Juhudi ya Ukonga, amepata nafasi hiyo baada ya kuchaguliwa na jopo la makocha na kuweka historia ya kuwa msichana wa kwanza wa Tanzania kuhudhuria mafunzo hayo.
“Hii ni faraja kwa Tanzania, makocha wa kimataifa wameona kipaji cha Jesca ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa ya wasichana ya wachezaji wa chini ya miaka 16, ameiwezesha Tanzania kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya Afrika Mashariki nchini Kenya, sasa tunampa bendera na kuiwakilisha nchi katika kozi hiyo, ni sifa kubwa kwake na kwa Taifa,”
“Michezo ni ajira,wachezaji wengi wa mpira wa kikapu wanalipwa vizuri, hii ni fursa kwa Jesca na wachezaji wasichana, bidii inakuwezesha kufanikiwa, Jesca ni mfano wa kuigwa na sasa anaingia katika vitabu vya kihistoria kwa kuwa msichana wa kwanza kupata mafunzo ya NBA, akifanya vizuri anaweza kwenda Marekani,” alisema Jokate.
Kwa upande wake, Jesca aliwashukuru wote walioshirikiana nao katika mchezo wa mpira wa kikapu na kuahidi kufanya vyema katika kliniki hiyo.
Alisema kuwa hakuamini kupata nafasi hiyo na kuwaomba wasichana wenzake kujishughulisha katika michezo kwani fursa ya kufanikiwa ipo.
“Ni faraja kwangu, wazazi wangu, walimu na wadau wa michezo kwa ujumla, ni heshima kwa Taifa kwani naiwakilisha nchi katika mafunzo hayo, sitawaangusha, nitafanya vizuri na ninaamini makocha wa NBA watavutiwa na kipaji changu na kusonga mbele,” alisema Jesca.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Mwenze Kabinda amempongeza Jesca kwa kupata nafasi hiyo na kuomba kuongeza bidii kwani hiyo ndiyo njia ya mafanikio.
No comments:
Post a Comment