Saturday, July 29, 2017

DC HAPI ASHUSHA PRESHA KWA WANANCHI KUNDUCHI, AHITIMISHA MGOGORO WA ARDHI WA MUDA MREFU


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Salum Hapi amefanya maamuzi magumu leo Jijini Dar es Salaam Kata ya Kunduchi Mjimwema baada ya kuumaliza mgogoro uliokuwepo kati ya wachimbaji wa kokoto na wananchi wapatao 3000 wa eneo hilo, mgogoro ambao umedumu kwa muda wa zaidi ya miaka 20.
DC Hapi ameagiza wananchi wa eneo hilo kuendelea kukaa maeneo hayo baada ya leseni ya uchimbaji kokoto eneo hilo kufutwa kutokana na uharibifu wa miundombinu.
"Hatuwezi kuhatarisha maisha ya wananchi 3000, tutawapeleka wapi, kwani wao siyo wanakinondoni, kwani wao siyo watanzania" Alisema DC Hapi.
DC Hapi ametoa maagizo kwa watendaji kuhakikisha kuwa wananchi hao wanamilikishwa maeneo hayo kwao kufuata taratibu na sheria ambapo itabidi maeneo hayo yapimwe na wananchi hao wawe wavumilivu maana kuna baadhi ya maeneo yatatengwa kwa huduma za kijamii, ikiwemo vituo vya Afya, Polisi na barabara.
Hata hivyo DC Hapi amewatoa hofu wananchi wa maeneo hayo kuhusu kulipia gharama za upimaji wa ardhi ambazo itabidi wachangie, huku akieleza kuwa wataiandikia barua mamlaka ya chuo cha Ardhi ili waweze kutoa baadhi ya wanafunzi ambao watafanya upimaji katika eneo hilo bure na kuwaondolea wananchi gharama za ziada.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Benjamini Sitta amesisitiza kuwa serikali itakuwa bega kwa bega na wananchi wanyonge kuhakikisha haki yao haipotei, huku Diwani wa Kata hiyo akihimiza ushirikiano katika shughuli za maendeleo kwani maendeleo hayana chama, hvyo ni vyema kuondoa itikadi.
Wananchi wa maeneo hayo wameonesha kuridhishwa na uamuzi huo wa serikali na kuhaidi kutoa ushirikiano wa hali na mali, huku wakimpongeza Rais Magufuli kwa serikali yake kujali maslahi ya wanyonge.

Mkuu wa Wilaya ya Kindoni Mhe Ally Hapi akishangiliwa na wananchi mara baada ya kuzungumza nao na kumaliza mgogoro wa muda mrefu wa ardhi katika eneo la Kunduchi Mecco na mji mpya Kata ya Kunduchi ambao hapo mwanza ilidaiwa na Manispaa ya Kinondoni kuwa wamevamia kwakuwa eneo hilo lilikuwa limepangwa kwa ajili ya Machimbo ya Kokoto.


Mkuu wa Wilaya ya Kindoni Mhe Ally Hapi leo ametangaza msimamo wa serikali ya wilaya ya Kinondoni kuwa wananchi wa Kunduchi Mecco na mji mpya Kata ya Kunduchi waliokuwa na hofu ya kuondolewa kuwa hawataondolewa na kwamba badala yake makazi yao yatapimiwa viwanja na watamilikishwa rasmi.

Uamuzi huo umekuja baada ya mvutano wa miaka mingi baina ya manispaa ya Kinondoni na wananchi hao waliovamia eneo hilo ambalo awali lilitengwa kwa ajili ya machimbo ya kokoto. Katika mvutano huo ulioibua kesi mbili zilizoendeshwa kwa muda mrefu na hatimaye manispaa kushinda kesi hizo, uamuzi umefikiwa kuwa Manispaa ya Kinondoni haitawavunjia na kuwaondoa wananchi hao wapatao zaidi ya 3000 waliojenga eneo hilo. Badala yake eneo hilo litapimwa ili kupanga vema mji na kuruhusu maeneo ya huduma za msingi za jamii kama barabara, shule, afya na zahanati kutengewa maeneo.

Akiambatana na Meya wa manispaa hiyo Benjamin Sitta pamoja na Kaimu Mkurugenzi, Mh. Hapi ameeleza kuwa serikali ya wilaya itaendelea kumaliza migogoro ya ardhi wilayani humo na kwamba wananchi waendelee kuiunga mkono na kuipa ushirikiano.Uamizi huo umepokewa kwa shangwe kubwa na wananchi wa Kunduchi walioamua kumuamuru dereva azime gari la DC HAPI na kulisukuma huku wakina mama wakilifuta vumbi kwa kanga kama ishara ya kufurahia uamuzi huo.

“Leo natangaza rasmi uamuzi wa serikali ya wilaya kuwa hamtaondolewa hapa.Badala yake mtapimiwa na kumilikishwa kihalali ili mpewe hati.”
Alisema DC Hapi.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi wake, diwani wa kata hiyo Mh. URIO ameishukuru serikali kwa uamuzi huo na kwamba wananchi wake wataendelea kuiunga mkono.

No comments: