Na Felix Mwagara (MOHA)
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mhandisi Hamad Masauni ameongozana na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mkoani Tanga
kufanya operesheni ya kuwasaka waharibifu
wa chanzo cha maji cha Mto Zigi ambao unapeleka maji Tanga mjini.
Masauni alifika katika eneo hilo la
tukio saa mbili usiku na kujionea maeneo yaliyoharibiwa kwa kuchimbwa mashimo
makubwa na wahalifu hao wakidai kuwa wanatafuta madini ya dhahabu. Hata hivyo,
hakuna mhalifu aliekamatwa katika eneo hilo wakati wa oparesheni hiyo.
Akizungumza katika eneo hilo lililopo Tarafa
ya Amani, wilayani humo jana, Masauni ambaye pia aliambatana na Mbunge wa Jimbo
la Muheza, Balozi Adadi Rajabu, alisema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya
oparesheni katika eneo hilo usiku na mchana kwa kushirikiana na walinzi wa msitu
ili kuwaondoa wahalifu hao haraka
iwezekanavyo.
Masauni alisema licha ya Polisi
kuendelea kufanya doria katika eneo hilo lakini wanatarajia kufungua kituo cha
polisi ili kuongeza ulinzi zaidi katika eneo hilo muhimu ambalo ndio chanzo cha
maji kwa sehemu kubwa ya wakazi wa Mji wa Tanga.
“Tumepanga kuimarisha ulinzi zaidi katika
eneo hili kwa kujenga kituo cha polisi ambapo askari wetu watashirikiana na
walinzi wa misitu kufanya doria ya kupambana na wahalifu,” alisema Masauni na
kuongeza;
“Kwa habari zisizo rasmi tulizozipata
katika vyanzo vyetu, hawa wahalifu wanamtandao mkubwa wakishirikiana na watu
mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na hata baadhi ya watumishi wa umma,
tutaendelea kufanya uchunguzi huu kwa kina kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa
wilaya ili kuwabaini wahalifu wote haraka iwezekanavyo.”
Hata hivyo, Masauni alifafanua kuwa, watafanya
uchunguzi wa kina kuwachunguza wale wote waliohusika kuwaficha wahalifu iwe
askari polisi, iwe mamlaka yoyote nyingine, iwe hakimu au watu wa aina yoyote watachunguzwa.
Watanzania tunapaswa tulinde rasilimali za Taifa pamoja na kusimamia ipasavyo.
Masauni alitarajia kwenda mkoani
Kilimanjaro kuendelea na ziara yake lakini mara baada ya kupewa taarifa kuhusu
uharibifu mkubwa unaofanywa na wahalifu katika msitu huo wa asili, ndipo
akaelekeza safari ya kwenda eneo hilo kwanza kuangalia hali halisi pamoja na
kuwasaka wahalifu hao ambao inasemekana wana watu hao wanapoona msafara unakuja
katika eneo hilo, wanaambizana na utoweka haraka katika eneo hilo.
Katika ziara yake ya siku moja mkoani
humo, kwa kutembelea mjini Tanga, Wilaya ya Pangani na baadaye akamalizia
Wilaya ya Muheza, Masauni alitoa maelekezo mbalimbali kwa Taasisi zilizochini
ya Wizara yake hasa Jeshi la Polisi na
Uhamiaji kuakikisha wanaongeza nguvu kubwa ya kuchunguza na kuzidi kuwasaka wahamiaji
haramu mkoani humo, na pia aliamuru ujenzi wa Gereza la Muheza kuanza mara moja
ili kupunguza msongamano mkubwa uliopo katika Gereza Kuu la Tanga pamoja na
mengineyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya
Muheza, Mhandisi Mwanaasha Tumbo
alimshukuru Naibu Waziri huyo kwa kufanya ziara katika wilaya yake, na pia
alishukuru kwa kuamuru ujenzi wa Gereza Muheza kuanza mara moja na kuahidi
kuyafanyia kazi zaidi maelekezo mbalimbali aliyoyatoa wilayani humo.
Hata hivyo, Mhifadhi Msaidizi wa Hifadhi
hiyo ya Asili, Bob Matunda alisema mara kwa mara wanawakamata wahalifu hao na
kuwafikisha katika vyombo vya usalama, na akaahidi kuwa wataendelea
kushirikiana kikamilifu na Jeshi la Polisi katika oparesheni mbalimbali za
kuwaondoa wahalifu hao katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment