Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.
Kamishana wa usimamizi wa mipaka idara ya Uhamiaji Tanzania, Samwel Magweiga, amepiga marufuku Mawakala wanaojihusisha na shughuli za uhamiaji na kuwataka waache mara moja kufanya hivyo.
Badala yake amewataka wananchi wanaohitaji huduma hiyo kufika ofisi husika ya Uhamiaji.
Kamishana Magweiga ametoa wito huo leo, wakati akizungumzia ukamatwaji wa watu watano wenye umri wa kati ya miaka 55 na 64 ambao walikutwa wakimiliki ofisi na mitambo wa kughushi nyaraka mbalimbali ikiwamo ya kughushi miradi ya maendeleo ya Serikali na machine za risiti za kielektroniki (EFDs).
Kufuatia ukamataji huo, Kamishna Magweiga amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa idara ya Uhamiaji ili kudhibiti mianya ya watu wanaojihusisha na kughushi nyaraka za aina mbalimbali kwa kuwa zinapelekea uhujumu wa uchumi.
Mapema wiki hii, makachero kutoka ofisi za uhamiaji baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasalimia wema kuhusu kuwepo kwa hujuma hiyo, walifanya msako na kuwakamata wazee watano ambao ofisi yao ipo eneo la BibiTiti Mohammed kiwanja namba 16/47 lililopo Wilaya ya Ilala mtaa wa Mtendeni.
Wazee waliokamatwa ni Hemed Ali Mchepe(56), Edga Samson Mwafongo(55), Huruma Mwakidete(57), David Tumpange (64),At human Mohammed (61) na Simon Joseph Veso (62).
Amesema, “kuna magenge ya wahalifu huko mitaani ambao wanafanya kazi kwa niaba ya serikali, hawa ni wahujumu uchumi, ni lazima wafichuliwe.” Amesisitiza Kamishna Magweiga.
Ameongeza kuwa, nyaraka hizo za mara nyingi zimekuwa zinatumika kuchukua hati za kusafiria, mikopo benki na kupelekea benki husika kupata hasara na serikali kukosa mapato.
Amesema, upelelezi dhidi ya watuhumiwa hao umekamilika na siku yoyote watapelekwa mahakamani ila badoa wanahitaji kujua mtandao wao ni mkubwa kiasi gani na upo hapa nchini pekee ama na nje ya nchi.
Wakielezea jinsi walivyokamatwa mbele ya Kamishana mzee David Tumpange alikubali kuwa yeye ni mmiliki wa ofisi iliyokutwa na nyaraka hizo za kughushi iliyopo eneo la barabara ya Bibi Titi Mohammed na kwamba yeye hashughuliki nayo alimkabidhi ndugu yake Huruma Mwakidete.
Aliongeza kuwa, kwa sasa yeye anajishughulisha na masuala ya ujenzi na siku ya tukio, alikwenda kwenye ofisi yake hiyo kwa ajili ya kumsalimia ndugu yake huyo aliyemkabidhi ofisi na vyote vilivyokutwa humo havitambui.
Huruma Mwakidete ambaye ni mstaafu wa Kampuni ya Bia ya TBL na ndiye alikabidhiwa ofisi hiyo na David, yeye alikubali kuendesha ofisi hiyo na kwamba ofisi hiyo ni ofisi huru na inashughulika na mambo mbalimbali ikiwamo ujenzi.
Aliongeza kuwa nyaraka zinazodaiwa za kughushi zilizokutwa ndani ya boxi katika ofisi yao hazitambui na wala hajui zilikopatikana.
Edga Samson alisema ofisi hiyo siyo yake, hausiki nayo ila alipita siku hiyo alipita ofisini hapo kwa ajili ya kumuona rafiki yake Huruma Mwakidete.
Hemed Mchepe yeye ni mstaafu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam yeye alikana kuhusika na ofisi hiyo wala nyaraka zilizokamatwa na kwamba alifika ofisini hapo kwa ajili ya kusalimia marafiki zake na kusoma gazeti.
Watuhumiwa hao walikamatwa na nyaraka mbli mbali za kughushi zikiwamo fomu mbalimbali za Idara ya Uhamiaji Tanzania zikiwemo za kuomba hati za kusafiria, VISA, vibali vinavyowaruhusu raia wa nje kuishi nchini na kufanya kazi, fomu ya shahada ya dharura ETD.
Vingine ni, vyeti vya kughushi vya ndoa na taraka kutoka Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la waislamu Tanzania (Bakwata), Karatasi za EFDs za manispaa, stakabadhi za kutoza ushuru katika halmashauri mbalimbali ikiwamo ya Temeke.
Vingine ni vyeti vya vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi, vyeti vya kumaliza elimu ya msingi, kidato cha nne, vyeti vya elimu ya juu ikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na matokeo yake.
Pia walikutwa na nyaraka za uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma zinaoonyesha ni halali na zimetolewa na Baraza Mitihani Tanzania, nyaraka za kughushi za makubaliano ya miradi mbalimbali ya maendeleo ya Serikali ikiwamo mradi wa Wilaya ya Mafia wenyewe zabuni namba LGA 008/2016/2017/W/15 package II.
Mbali na nyaraka hizo za kughushi pia walikutwa na leseni za utalii za kughushi zinazotolewa na bodi ya Utalii nchini, Tin namba na nyaraka za ulipaji wa kodi zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), vyeti vya kughushi vya kuzaliwa, matangazo ya kuzaliwa ya mtoto yanayotolewa na Idara ya Msajili Mkuu wa Vizazi na vifo, Stakabadhi za halmashauri za kukusanya ushuru, vitambulisho vya Mkazi, hati mikiliki, nyaraka za utambulisho wa utumishi wa umma wa halmashauri ya Manispaa ya Temeke, nyaraka za kupotelewa na kitu zinazotolewa na kes jeshi la polisi.
Pia walikutwa na mihuri ya kughushi ya benki ya Exim tawi la mnara wa saa na tawi la Namanga, muhuri wa mkuu wa Shule ya sekondari ya Jamuhuri Dodoma, makampuni mbalimbali na mihuri ya Halmashauri mbalimbali na Kata ikiwamo ya Mtendeni.
1 comment:
Aisee!hao jamaa ni hatari yaani wamejipanga utadhani ndio serikali yenyewe.
Post a Comment