Monday, June 19, 2017

VIGOGO WA ESCROW NA IPTL WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA MAKOSA YA KUHUJUMU UCHUMI



Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii.
Mkurugenzi wa kampuni ya VIP Engendering na mmiliki mwenzangu wa zamani wa IPTL James Rugemalira na Habinder Seth Sigh, Mwenyekiti mtendaji wa PAP wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka sita.
Watuhumiwa hao wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma uhujumu uchumi na kula njama, kughushi, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuisababisha hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
Washtakiwa hao wote wamesomewa mashtaka yao na mwendesha mashtaka, wakili wa serikali, Paul Kadushi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi. Hata hivyo, wamerudishwa rumande hadi Julai 3 mwaka huu kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza wala kutoa dhamana kwa kesi ya uhujumu uchumi.

Wawili hao wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18 ,2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Imedaiwa kuwa, katika shtaka la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18,2011na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam wakiwa siyo watumishi wa umma na wakisaidiana na watumishi wa umma walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la nne mtuhumiwa Sethi anadaiwa kuwa Oktoba 10,2011 katika mtaa wa Ohio Ilala DSm akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 a ya usajili wa makampuni na kuonesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua si kweli.

Seth anadaiwa kutoa nyaraka hiyo ya usajili wa kampuni kwa ofisa msajili wa kampuni, Seka Kasera kwa njia ya kuonesha kwamba yeye ni Mtanzania na Mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Aidha katika shtaka jingine, Washtakiwa wote, wanadaiwa kuwa kati ya Novemba 28/29, 2011 na Januari23,2014 makao makuu ya benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi tawi St Joseph zote za Dar es salaam, kwa ulaghai, walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), USD 22,198,544.60 na shilingi 309, 461,300,158.27. 

Iliendelea kudaiwa kuwa katika shtaka la kusababisha hasara, washtakiwa hao wanadaiwa kwamba mnamo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati Kinondoni kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya USD 22, 198, 544.60 na Tsh 309,461,300,158.27.

Baada ya kumaliza kusomewa mashtaka yao, wakili wa utetezi Respicius Didas kwa niaba ya mawakili wenzao aliomba mahakama iwapatie wateja wao dhamana kwa sababu Mashtaka yanayowakabili yanadhaminika.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga vikali hoka hizo na kuiomba mahakama kuyatupilia mbali maombi ya utetezi ya kuwapatia dhamana washtakiwa hao.

Akiwasilisha hoja zake, Wakili Kadushi amesema mahakama ya Kisutu haina mamlaka si tu ya kutoa dhamana bali hata kusikiliza maombi ya dhamana. Amesema mahakama pekee yenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Mahakama Kuu na ndiyo maana washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote wakati wakisomewa mashtaka yao.

Ameongeza mazingira pekee ambayo yangeifanya mahakama ya Kisutu iweze kusikiliza maombi hayo na kesi kwa ujumla wake ni pale ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) angetoa cheti maalum cha kuipa mamlaka mahakama ya Kisutu kuisikiliza kesi hiyo.

" Maombi ya dhamana yameletwa katika mahakama isiyoweza kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria" amesema Wakili Kadushi.

Naye Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alisisitza na kuomba mahakama kutupilia mbali hoja zote za maombi ya dhamana zilizotolewa na upande wa utetezi na ijielekeze kwa Jinsi inavyoona inafaa washtakiwa waende mahabusu wakati wakisubiri taratibu za kesi zinazoendelea. 

Akijibu hoja hizo, Hakimu Shaidi amesema sheria inaelekeza kwamba kesi za uhujumu uchumi zinazozidi shilingi milioni 10 Mahakama hiyo  haina mamlaka ya kuisikiliza wala kutoa dhamana isipokuwa kwa Cheti maalum kutoka kwa DPP kinachoiwezesha mahakama kufanya hivyo.

Kesi hiyo itatajwa Julai 3,2017 na watuhumiwa wameenda kulala mahabusu gereza la Segerea.
 Mmiliki wa VIP Engineering and Marketing, James Rugemalila na Mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Seth Sigh wakiwa  Ndani ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam leo.
 Mmiliki wa VIP Engineering and Marketing, James Rugemalila na Mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Seth Sigh  wakipandishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu jijini Dar es Salaam



Mmiliki wa VIP Engineering and Marketing, James Rugemalila na Mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Seth Sigh  wakitoka katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mara baada ya kukosa dhamana na kutakiwa kupelekwa mahabusu.


  Mmiliki wa VIP Engineering and Marketing, James Rugemalila na Mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Seth Sigh wakisindikizwa kwenye gari tayari  kupelekwa rumande mara baada ya kukosa Dhamana kutokana na Makosa yanayo wakabili
   Mmiliki wa VIP Engineering and Marketing, James Rugemalila na Mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Seth Sigh wakipakiwa kwenye gari kwa ajili ya kupelekwa Rumande mara baada ya kukosa Dhamana kutokana na Makosa yanayo wakabili

   Mmiliki wa VIP Engineering and Marketing, James Rugemalila na Mmiliki wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Seth Sigh wakiwa kwenye gari kwa ajili ya kupelekwa rumande mara baada ya kukosa Dhamana kutokana na Makosa yanayo wakabiri.



No comments: