Tuesday, June 6, 2017

SEKTA YA HABARI NCHINI ITAHESHIMIKA IWAPO WANAHABARI WATAJIWEKEA MALENGO YA KUFANYA KAZI KWA AJENDA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,Balozi Seif Ali Idd  akimsikiliza  Mkurugenzi Mkuu wa  Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania { Tanzania Media Foundation – TMF } Bwana Ernest Sungura alipokuwa akizungumza nae jambo ofisini kwake.

 Mkurugenzi Mkuu wa  Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania { Tanzania Media Foundation – TMF } Bwana Ernest Sungura  amesema hadhi ya Sekta ya Habari Nchini itaheshimika na kuaminika zaidi endapo wanahabari wenyewe watajiwekea malengo ya kufanya kazi kwa agenda katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Alisema mfumo wa agenda kwa Wanahabari ndio njia pekee itakayosaidia  kuamsha ari sambamba na kuibua changamoto zinazokwaza Jamii na kuzipa nguvu za uwajibikaji Taasisi za Umma na hata zile binafsi katika kuwahudumia kwa umakini Wananchi.

Nd. Ernest Sungura  Alisema hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa TMF uliokuwepo Zanzibar  kwa ziara maalum ya kukagua  Maandalizi na Mikakati  ya mradi wa kuwapatia Mafunzo Wanahabari wa Zanzibar.

Alisema kupitia Mfuko wa Vyombo vya Habari zipo agenda zilizowahi kuibuliwa na Wanahabari wa Vyombo tofauti Nchini akizitolea mfano  vita dhidi ya Dawa  za Kulevya, Udhalilishaji wa Kijinsia na ubalozi wa Usalama barabarani ambazo zimesaidia kuleta faraja kwa Jamii na kuzipunguzia matumizi mabovu yasiyo na msingi Serikali zote mbili.

Alieleza kwamba yapo mambo mengi na mazuri ya kujivunia  kutokana na kuanzishwa kwa mfumo huo wa agenda  jambo ambalo limeziletea sifa Taasisi za Habari kwa Taifa na Wananchi jambo ambalo lilisaidia kuibua changamoto zinazokwaza Serikali na Jamii kwa ujumla.

Bwana Sungura alimueleza Balozi Seif  kwamba katika kuwajengea uwezo uliobobea Waandishi wa Habari katika utekelezaji wa kazi zao.

Alisema kuwa tangu kuanzishwa kwake, TMF tayari imeshatoa ruzuku kwa   Wanahabari  binafsi zaidi ya 600 na taasisi za  kutoka kihabari 120 nchini.

Alisema mkazo zaidi wa mafunzo hayo utawekwa kwa wale waandishi na Vyombo vya Habari visivyo na uwezo wa kufanyakazi vizuri  ili navyo viweze kupiga hatua itakayokwenda sambamba na wenzao wenye nguvu za uwezeshaji kifedha.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliushukuru Uongozi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania { TMF } kwa uamuzi wake wa kuwafinyanga Wanahabari katika misingi ya kuwajibika Kitaaluma zaidi badala ya kukurupuka katika Uandishi wao.

Balozi Seif alisema kitendo cha Taasisi hiyo cha kuwajengea uwezo wa Kitaaluma Wana Tasnia hao wa Habari kitawawezesha kuzalisha zao litakalopokewa vyema tena kwa Heshima kutoka kwa Jamii.


Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

5/6/2017

No comments: