Tuesday, June 6, 2017

Bilioni 16.9/- kunufaisha sekondari 1696

Frank Mvungi- Maelezo
Serikali imetumia shilingi bilioni 16.9 kununua vifaa vya maabara na vile vya wanafunzi wenye mahitaji maalum vitakavyonufaisha shule za sekondari 1696 ambapo shule 1625 ni za Kata na 71 ni kongwe ambazo kwa sasa zipo katika ukarabati.

Akihutubia wakati wa hafla ya kuzindua  mpango wa  kusambaza vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum leo Jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa inaboresha sekta ya elimu  ili azma ya ujenzi wa Tanzania ya Viwanda itimie kwa kuwa Taifa litaweza kuzalisha wanasayansi kulingana na mahitaji.

“Tunatoa vifaa hivi kwa awamu ya kwanza kwa shule zilizokamilisha ujenzi wa maabara, hivyo ni matumaini yangu kuwa wale ambao hawajakamilisha watafanya hivyo ili awamu ijayo nao wapate vifaa hivi.” Alisisistiza Majaliwa.

Aliongeza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha zaidi ya shule 4,000 nchini zinakuwa na vifaa vya maabara, walimu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia na mazingira rafiki ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bora itakayowasaidia kushiriki katika ujenzi wa Taifa.

Pia Waziri Mkuu ameonya kuwa Serikali itachukua hatua kali dhidi ya mtu yoyote atakaye sababisha mwanafunzi wa kike kupata ujauzito na kushindwa kuendelea na masomo ambapo atakabiliwa na adhabu ya kwenda jela miaka thelathini.

“Awe baba au mama au mtu yoyote ambaye itathibitika kuwa amemsababishia ujauzito mwanafunzi, adahabu yake ni kifungo cha miaka thelathini jela.” Alisisitiza Majaliwa.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali imetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kuendelea kununua vifaa hivyo lengo likiwa kuendelea kuinua kiwango cha elimu kwa kushirikisha wadau wa maendeleo.

“Vifaa hivi vinakidhi mahitaji ya wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na upatikanaji wa vifaa hivi ni utekelezaji wa ahadi ya serikali ya Awamu ya Tano kwa wananchi katika kuboresha sekta ya elimu na vitawaongezea wanafunzi kasi ya kudadisi na  kujifunza.” Alisisistiza Prof. Ndalichako.

Akifafanua kuhusu upatikanaji wa vifaa hivyo Prof. Ndalichako aliwashukuru wadau wa  Maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia, Uingereza, Denmark na wengine kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua kiwango cha elimu nchini ili kuchochea maendeleo kwa kuwa ufaulu wa masomo ya sayansi utaongezeka.

Kwa Upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa  kazi ya kupokea vifaa hivyo imefanyika kwa ufanisi na  kuahidi kuwa watatekeleza jukumu la kusambaza vifaa hivyo kama ilivyopangwa kupitia Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Vifaa hivyo vya maabara na vile vya wanafunzi wenye mahitaji maalum  vyenye thamani ya shilingi bilioni 16.9 vitasambzwa katika Kanda 11 na baadhi ya mikoa itakayonufaika katika Kanda hizo ni Dar es Salaam, Katavi, Kagera, Rukwa, Pwani, Tanga, Mwanza, Singida, Dodoma.
 Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya walimu na wanafunzi wa shule za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa zoezi la  usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum  mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
 Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (mwenye tai nyekundu) akipata maelekezo toka kwa moja ya mwalimu wa masomo ya sayansi wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum  mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
 Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (mwenye tai nyekundu) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
  Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (kulia) akikabidhi moja ya kifaa cha kufundishia masomo ya sayansi kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Juhudi wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum  mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum  mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya wanafunzi  wa shule za Mkoa wa Dar es Salaam wakimsikiliza Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum  mapema hii leo katika viwanja vya hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.



Picha zote na Eliphace Marwa - Maelezo

No comments: