Wednesday, June 21, 2017

RC WA TANGA MH MARTINE SHIGELLA AFUNGU MAFUNZO YA KUMALIZA MAFUNZO YA AWALI

Mkuu wa mkoa wa Tanga Mh. Martine Shigella amewataka wahitimu wa mafunzo  ya awali ya kijeshi ya vijana operasheni Magufuli awamu ya pili wa kujitolea kutumia mafunzo waliyoyapata kwa kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa niaba ya Taifa la Tanzania.

Hayo ameyazungumza wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya kumaliza mafunzo ya awali ya kijeshi ya vijana operesheni Magufuli awamu ya pili  wa kujitolea yaliyofanyika kwenye  Kituo namba  835KJ Mgambo JKT  kilichopo Kata ya Kabuku Wilayani Handeni.

Mkuu wa Mkoa amesema kuwa mafunzo ya ukakamavu wa mwili, uzalishaji mali, masuala mazima ya ulinzi na usalama na mafunzo ya kijeshi yatumike kwa uzalendo na kuwa mfano bora kwa jamii itanayowazunguka.

“ Nendeni mkawe mfano bora wa kuigwa  kwenye familia zenu na wazazi wenu wamekuja hapa kuwashuhudia, Sisi kama Serikali tunawaamini” alisema Shigella.

Ameongeza kuwa Mh. Rais alipoamua kurudisha mafunzo haya alitambua umuhimu mkubwa kwa Taifa letu sababu anajua mahitaji ya sasa na ya baadae wakati lengo kuu likiwa ni kuleta usawa na uzalendo kwa wasomi na wasio wasomi.

Amewataka wakatimize wajibu wao wa kuwa raia wema na kuwa walinzi wa Taifa kwa kupitia mafunzo ya ulinzi na usalama waliyoyapata huku akieleza kuwa Serikali inapambana na changamoto za kukabiliana na wahalifu  ambao hawataki kuwa kama wanadamu wengine.

 “ Nina imani kubwa na nyinyi kwamba mtaendelea kuwa waadilifu, waaminifu na kuendelea kupiga vita vitendo vya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma na kwamba mtakuwa kimbilio la wanyonge na watu wenye matatizo makubwa” alisema Shigella.

Amewasisitiza kuendelea kujiendeleza kielimu ili waweze kupata ajira zinazolingana na hadhi zao. Waje wafanye kazi kwenye viwanda na kwamba rasilimali watu isitegemewe kutoka nje ya Tanga na Tanzania.

Ameeleza kuwa watakaofanya kazi kwenye viwanda watoke Tanzania kwa maana Tanga kuna viwanda vingi vinatarajiwa kuwepo na hivyo nguvu kazi itahitajika ya kutosha na angependezwa kuona miongoni mwao wanatoka JKT Mgambo.

Mwisho amewataka wahitimu kuongeza jitihada za uzalishaji mali hasa kwa kipindi hiki tunachoendea kua Tanzania ya Viwanda  kwani  ili Viwanda viwe na thamani,  wasomi na upatikanaji wa bidhaa zitakazohitajika viwandani hazinabudi kuwepo wakati wote na kwa wingi.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutenga muda wake kuweza kujumuika pamoja katika kufunga mafunzo hayo. Alieleza kuwa kuhusu suala la maji atalishughulikia kwa pamoja na Viongozi wa Halmashauri na kwamba atahakikisha maji yanafika Wilayani Handeni .

 Mafunzo ya awali ya Kijeshi kwa Vijana wa kujitolea Operesheni Magufuli yalifunguliwa tarehe 2Jan 2017 yakiwa na jumla ya Vijana 1083 kati yao wasichana 270 na wavulana 813 idadi ya vijana 5 hawakuweza kumaliza mafunzo  kutokana na kijana 1 kufariki, 3 kutorokaa wenyewe na 1 aliahirisha mafunzo hivyo kufanya idadi kubaki 1078.

Mafunzo waliyoyapata ni  uzalishaji mali, huduma za jamii , michezo, mafunzo ya kijeshi ya (Ulinzi na usalama wa Taifa na mafunzo ya kijeshi ya mbinu za kivita,elimu ya mapigano, matumizi ya silaha ndogondogo, usalama na utambuzi, uokoaji, huduma ya kwanza, usomaji ramani, sheria  za kijeshi) n.k.

Alda Sadango
Afisa Habari
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh Martin Shigella akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.
 Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe akizungumza na wakati wa kufunga Mafunzo.
 Wahitimu wa Mafunzo wakiwa kwenye Gwaride

 Picha ya pamoja na Baadhi ya wahitimu.
 


Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh Martin Shigella akitoka kukagua gwaride

No comments: