Tuesday, June 6, 2017

MWILI WA HALILA TONGOLANGA WAAGWA

Halila Tongolanga amefariki jana usiku katika hospitali ya Muhimbili. Alikuwa mwanamuziki wa siku nyingi na alifahamika kwanza kwa wengi baada ya kuanza kusikika kibao chake cha lugha ya Kimakonde cha Kila munu ave na kwao, chenye tafsiri ya ‘Kila mtu ana kwao’ ambacho alikirekodi akiwa bendi ya jeshi ya CTU Monduli, iliyojulikana kama Les Mwenge.
 
 Kwa kifupi ni kuwa baada ya hapo aliitwa kujiunga na bendi iliyokuwa mali ya Dr Alex Khalid, iliyokuwa ikiitwa Makondeko Six. Wakati huo Dr Khalid alikuwa na sehemu kubwa ya burudani iliyokuwa pia na ukumbi na ilikuwa inaitwa Makondeko ikawa na bendi ya watu sita hivyo bendi hiyo ikaitwa Makondeko Six. 
 
Bendi hii awali ilikuwa ikipiga muziki kwa kufuata nyayo za bendi ya Tatu Nane, lakini Dr Khalid baada ya kuona bendi haina umaarufu kutokana na aina ya muziki iliyokuwa ikipiga, ndipo alipomuita Halila Tongolanga nae akaja na baadhi ya wanamuziki wakajiunga na kuanzisha kundi lililoendelea kutumia jina la Makondeko Six japo wanamuziki walikuwa wengi zaidi ya sita. 
 
Na ndipo katika kundi hili lilikuwa na wanamuziki wengine kama Innocent Nganyagwa, Anna mwaole wakaweza kurekodi tena wimbo wa Kila Munu Ave na kwao na kundi kupata umaarufu mkubwa mpaka baada ya kusambaratika kwa Makondeko baada ya kifo cha Dr Alex Khalid, lakini Tongolanga aliendelea kutumia jina la Makondeko. 

Tongolanga amefanya kazi nyingi za muziki ikiwemo kuwa mmoja wa kundi lililoundwa na wanamuziki wengine mahiri kama Moshi William, Muhidin Mwalim, Huluka Uvuruge, Kandaya na wengine lililojulikana kama Bana mwambe, ambapo waliweza kutoka nyimbo nyingi nzuri sana wakati biashara ya kuuza album ilipokuwa ina faida. 
 
Tongolanga ameagwa na wapenzi wa muziki ndugu na marafiki, lakini kulikuwa na uhaba mkubwa wa wanamuziki wenzie katika kundi lililokuja kumuaga mwanamuziki huyu. Waliojitokeza hasa ni wanamuziki wale tu ambao waliwahi kupiga nae katika kundi la Makondeko na Bana Mwambe na wanamuziki wengine wachache wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Muziki John Kitime, Katibu Mkuu wa Chamudara Hassan Msumari. 
 
Serikali iliwakilishwa na Katibu Mtendaji wa BASATA. Katika jambo moja kubwa lililotokea wakati wa kuaga mwili ni kujitokeza kwa balozi wa Msumbiiji Bi Monica Patricio Clemente aliyefika Muhimbili kuaga mwili wa Tongolanga akiwa amesindikizwa na maafisa wengine, na pia Balozi huo alitoa rambirambi zake kama Balozi na alitoa rambirambi kutoka kwa Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji. 
 

Hili lilikumbusha usemi wa wahenga ‘Nabii hathaminiwi kwao.’ Taarifa zilizopatikana pale ni kuwa Tongolanga alikuwa mtu maarufu sana nchini Msumbiji, na aliyekuwa ni msanii muhimu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini humo. 
Balozi wa Msumbiji Bi Monica Patricio Clemente akiaga sanduku lililokuwa na mwili wa Halila Tongolanga 

Baadhi ya wanamuziki waliowahi kufanya kazi na Tongolanga katika kundi la makondeko Six, wakiwa wanasubiri kusafirisha mwili wa mpendwa wao.Toka kushoto, Innocent Nganyagwa, Meneja wa bendi, mpiga solo, Waninga 


John Kitime, wanamuziki wa Makondeko Six, Mngereza, Kumburu


Toka kushoto Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Nyangamale, Balozi wa Msumbiji nchini, Katibu Mtendaji wa BASATA, Mbunge wa Tandahimba Mhe Katani Katani, afisa wa Ubalozi wa Msumbiji ,Tongolanga anategemewa kuzikwa kijijini kwao Mchichila kesho Junanne 6 Juni 2017.
Mungu Amlaze Pema Halila Tongolanga 



Nilipokutana nae kwa mara ya mwisho akiwa kitandani Tongolanda kwa sauti ya uchovu alinambia alikuwa na mengi ya kunambia, wakati tunasubiri taratib kukamilika za kuanza kusafirisha mwili, Innocent Nganyagwa ambaye alikuwa mmoja ya wanamuziki waliotengeneza kundi la Makondeko Six alinambia Tongolanga alikuwa amepanga kufanya onyesho la ‘Usiku wa Makondeko’ na alikuwa na mipango mingine mikubwa ya kufanya kupitia kipaji chake. Pengine ndiyo hayo aliyotaka kunambia Mungu pekee anajua.

Shukrani za pekee zimfikie Mbunge wa Tandahimba Mheshimiwa Katani Ahmed Katani, kwani kwa juhudi zake Tongolanga alisafirishwa akiwa hai kutoka Ndanda hadi Dar es Salaam kwa matibabu, na pia ndie aliyeusafirisha mwili wa mwanamuziki huyu kwenda Mchichila kwa ajili ya mazishi. 
Mpiga Kinanda Geophrey Kumburu, Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza, Katibu Mkuu wa CHAMUDATA Hassan Msumari 
Sanduku alilolazwa Halila Tongolanga likitayarishwa kuingizwa kwenye gari la kusafirisha kuelekea Mcjichila 


Sanduku likiingizwa kwenye gari 
Imetayarishwa na John Kitime wa www.tanzaniarhumba.blogspot.com

No comments: