Sunday, June 11, 2017

MTOTO WA MIAKA 12 AIBUKA KIDEDEA MASHINDANO YA KUHIFADHI QURAN


  Waziri Mkuu, Kasssim Majaliwa akizungumza katika kilele cha Mashindano  ya 11 ya Afrika ya Kuhifadhi Qur-an Tukufu yaliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Juni 11, 2017. 
Waziri Mkuu, Kasssim Majaliwa akizungumza katika kilele cha Mashindano ya 11 ya Afrika ya Kuhifadhi Qur-an Tukufu yaliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Juni 11, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi , Mohammed Abdullah Aden (12) wa Somalia hundi ya shilingi milioni 15, 750,000/= mshindi wa kwaza wa mashindano ya 18 ya Afrika ya Kuhifadhi Qur-an Tukufu yaliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Juni 11, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi , Mohammed Abdullah Aden (12) wa Somalia hundi ya shilingi milioni 15, 750,000/= mshindi wa kwaza wa mashindano ya 18 ya Afrika ya Kuhifadhi Qur-an Tukufu yaliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Juni 11, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mh. Paul Makonda akizungumza katika mashindano hayo yaliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam leo. 
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili na Mlezi wa Taasisi ya Al- Hikma Foundation, Alhaj Ali Hassan Mwinyi akizungumza katika kilele cha Mashindano ya 18 ya Kuhifadhi Qur-an Tukufu yaliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Juni 11, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally (kulia) na Sheikh Sharif Abduqadir Mohamed Ahmed Al Ahdar ambaye ni Rais wa Taasisi ya Al – Hikima Foundation na Mlezi Mwenza wa Taasisi hiyo , katika Mashindano ya 18 ya Afrika ya Kuhifadhi Qur-an Tukufu yaliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Juni 11, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mufti na Sheikh Sharif Abduqadir Mohamed Ahmed Al Ahdar ambaye ni Rais wa Taasisi ya Al – Hikma Foundation na Mlezi Mwenza wa Taasisi hiyo, katika Mashindano ya 18 ya Afrika ya Kuhifadhi Qur-an Tukufu yaliyofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Juni 11, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…………………………………………………………

*Waziri Mkuu amuagiza Meya wa Temeke kesho atoe maamuzi ya kiwanja

MTOTO wa miaka 12 kutoka Somalia, Mohammed Abdullahi Aden ameibuka kidedea na kitita cha dola za Marekani 7,000 (sawa na sh. milioni 15.75) katika mashindano ya 18 ya Afrika ya kuhifadhi Quran kwenye kundi la washiriki wa juzuu 30.

Mohammed ambaye ni miongoni mwa washiriki wadogo zaidi wawili kuliko wote (mwenzake anatoka Burundi), amejishindia pia IPAD, cheti, kompyuta iliyotolewa na Balozi wa Kuwait, ahadi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na ahadi ya kwenda nchi yoyote aitakayo kutoka kwa kampuni ya Sky Bus Travel Agency ya jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na maelfu ya waumini na Watanzania waliofurika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo mchana (Jumapili, Juni 11, 2017), Waziri Mkuu Kassim Majaliwa waandaaji wa mashindano hayo ambayo ni Taasisi ya Al-Hikma waangalie uwezekano wa kuboresha zawadi kwa kutoa scholarships (udhamini) kwa washindi au washiriki, hususan kwa washiriki wa Tanzania.

“Ongeeni na nchi marafiki kama Saudi Arabia, waone uwezekano wa kutoa zawadi za ufadhili kwenye masomo ya sekta za kimkakati kama vile mafuta na gesi, ili kuongeza hamasa na chachu ya vijana walioko kwenye sekondari zetu nao waone fursa hii na kuichangamkia, badala ya mashindano kujikita kwenye madrasa peke yake,” amesema.

Waziri Mkuu amewataka wazazi wafuatilie nyendo za vijana wao ili wasijiingize kwenye matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine viovu vinavyoweza kuhatarisha maisha yao na ustawi wa nchi yetu lakini akasisitiza pia waisaidie Serikali katika mapambano yake dhidi ya rushwa na ufisadi.

“Endeleeni kushirikiana na Serikali katika mapambano yake dhidi ya rushwa na ufisadi na kuwafichua wakwepa kodi. Kila mmoja wetu ahakikishe analipa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria. Hii itasaidia Serikali kuboresha huduma kwa wananchi ili waweze kufanya ibada zao vizuri zaidi,” amesema.

Washindi wengine kwenye kundi hilo na umri wao kwenye mabano ni Abdulkarim Ahmed Farhina (22) wa Sudan ambaye ameshinda dola za Marekani 5,000, cheti, IPAD, kompyuta iliyotolewa na Balozi wa Kuwait, ahadi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Wa tatu ni Mahamoud Ali Chamfi wa Comoro (18) na Seif Ramadhani Zombe (18) kutoka Taasisi za Tanzania ambao wote wamepata dola za marekani 3,000, cheti, IPAD, kompyuta iliyotolewa na Balozi wa Kuwait, ahadi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Wa nne ni Khalil Mussa Hussein (17) kutoka Tanzania Bara ambaye amepata dola za marekani 1,500, cheti, IPAD, na ahadi ya sh. milioni moja kutoka kwa  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Wa tano ni Ismail Issa Qasim (17) kutoka Tanzania Visiwani ambaye dola za marekani 1,000, cheti, IPAD, na ahadi ya sh. milioni moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,

Washiriki wengine kwenye kundi la juzuu 30 walitoka nchi za Nigeria, Kenya, Uganda, Djibouti, Afrika Kusini, Rwanda, Ghana, Ethiopia, Congo DRC, Burundi na Msumbiji. Umro wao ulikuwa ni kati ya miaka 12 na 26.

Washiriki wengine waliopewa zawadi ni wale walioweza kuhifadhi Juzuu tatu (washindi watano), Juzuu tano (washindi watatu); Juzuu 10 (washindi watatu) na Juzuu 20 (washindi watatu).

Viongozi wengine waliohudhuria kilele hicho ni Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Mohammed Gharib Billal, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Mhe. Mohamed Bin Mansour Al Malek. Wengine ni wawakilishi wanne wa Imam Mkuu wa Mskiti Mtakatifu wa Makkah, Sheikh Abdul Rahman Ibn Abdul Aziz as-Sudais; Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Meya wa Temeke, Bw. Abdallah Chaurembo kesho (Jumatatu, Juni 12, 2017) afuatane na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bw. Nassib Mmbaga hadi kwenye kiwanja kilichopo eneo la Matumbi na kukagua kama kuna uwezekano wa kuliongeza kwa taasisi ya Al-Hikma na wampe majibu Jumanne kwani limekaa wazi kwa muda mrefu licha ya kuwa walishaliomba na hawakupata majibu.

“Mstahiki Meya wa Temeke na Mkurugenzi wako, kesho Jumatatu nendeni mkaangalie eneo husika kama linafaa kuongezwa na mfanye maamuzi. Eneo hilo limekaa wazi kwa muda mrefu, na hawa wanataka wanataka kujenga zahanati. Jumanne asubuhi nipate taarifa ya maamuzi yenu,” alisema Waziri Mkuu na kushangiliwa na maelfu ya waumini waliokuwepo kwenye hafla hiyo.

No comments: