Sunday, June 25, 2017

Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka wazidi kushika kasi jijini Dar es salaam

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare akiwasili katika Kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka cha Kimara Mwisho. Mhandisi Rwakatare alipokewa na Kaimu Meneja Usafirishaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dkt Philemon Mzee (kushoto).
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare akipita sehemu ya ukaguzi wa tiketi na kadi zitumiwazo na Mabasi Yaendayo Haraka. Mhandisi Rwakatare alipata fursa ya kutembelea vitengo mbalimbali vya Kituo Kikuu cha Kimara mwisho na kujionea huduma za usafiri zinavyofanyika katika kituo hicho.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare akizungumza na mmoja wa abiria wa Mabasi yaendayo haraka katika Kituo Kikuu cha Mabasi hayo katika eneo la Kimara Mwisho.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare (kulia) akitembelea vitengo mbalimbali vya kutoa huduma katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo haraka kilichopo Kimara mwisho. Mhandisi Rwakatare aliambatana na Kaimu Meneja Usafirishaji wa DART Dkt Philemon Mzee, na Kushoto ni Afisa Habari Mkuu wa DART bwana Mathew Kwembe.
Sehemu ya daraja linalotumiwa na wananchi pindi wanapoingia na kutoka katika Kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka kilichopo Kimara Mwisho. Daraja hili ni miongoni mwa miundombinu iliyojengwa na Serikali kwa ushirikiano na Benki ya Dunia.



Na Mathew Kwembe

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare ameeleza kuwa mradi huo umepata mafanikio makubwa katika kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es salaam hususani katika barabara ya Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea kituo kikuu cha Kimara mwisho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma, Mhandisi Rwakatare alisema kuwa katika kipindi hicho cha mpito, Mabasi yaendayo haraka yameweza kusafirisha watu 200,000 kila siku kutoka watu 50,000 iliyokuwa ikisafirisha mwaka jana, wakati mradi unaanza.

Mhandisi Rwakatare alieleza kuwa Mradi huo umeweza kuokoa muda wa wananchi ambao kabla ya mradi kuanza walikuwa wakitumia usafiri mwingine uliokuwa ukichukua kutoka masaa mawili, wakati sasa wanatumia dakika 45 tu kwa safari ya kutoka Kimara hadi Posta kwa kutumia mabasi yaendayo haraka.

Alifafanua kuwa huduma hiyo mbali na kuwapunguzia mzigo wa nauli watumiaji wa kawaida wa mabasi ya daladala, mradi wa mabasi yaendayo haraka imeokoa gharama ya usafiri kwa wenye magari binafsi ambapo wengi wao wamekuwa wakiutumia zaidi usafiri huo.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma Mhandisi Rwakatare alisema kwa wakala umeona ni vyema kutumia maadhimisho hayo kusikiliza kero na maoni ya wananchi hasa watumiaji wa huduma hiyo ili kuona namna nzuri ya kuiboresha.

“Watumishi wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka wamekuwepo katika vituo vya Gerezani na Kimara mwisho kwa siku hizi mbili ili kusikiliza kero na maoni kutoka kwa wananchi wetu, na tunafurahi kuona huduma hii ikizidi kushika kasi, hasa kwa kuzingatia kuwa tupo katika kipindi cha mpito,” alisema.

Hata hivyo alisema kuwa maoni na ushauri walioupata kutoka kwa wananchi wataufanyia kazi na kurekebisha kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika kipindi cha mpito ili kuhakikisha kuwa huduma hiyo inakuwa bora zaidi.

Aisema kuwa Wakala upo mbioni kumpata mtoa huduma ya ukusanyaji mapato ambapo ndiye atakuwa na jukumu la kushughulikia suala la kadi ili kuondokana na changamoto mbalimbali za usafiri zinazowakabili watumiaji wa mabasi hayo.

“Natambua kuwa kadi zimeisha na wakala unalishughulikia jambo hili na tutahakikisha kuwa tunaongeza kadi, nawasihi wananchi watambue kuwa tupo katika kipindi cha mpito, mapungufu mengi yaliyojitokeza tutayarekebisha,” alisema.

Mhandisi Rwakatare alibainisha kuwa suala la kadi limechukua muda mrefu kwa vile mchakato wake unahusisha mfumo wa kibenki na hivyo kuwataka wananchi wa jiji la Dar es salaam kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha mpito kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza hususani suala la kadi ambapo aliahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo mapema iwezekanavyo.

Mhandisi Rwakatare alisema kuwa Mradi huo unatekelezwa kwa ubia baina ya Serikali na Kampuni binafsi ya UDART ambayo ndiyo iliyopewa jukumu la kutoa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka katika kipindi hiki cha mpito

Alisema Serikali kwa upande wake imeshirikiana na Benki ya Dunia kujenga miundombinu mbalimbali inayotumiwa na mabasi hayo ambapo katika awamu ya kwanza ujenzi wake umehusisha barabara zenye jumla ya kilometa 20.9 ambazo ni Kimara – Kivukoni, Magomeni – Morocco na Faya – Karikaoo.

Pia alisema kuwa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka upo mbioni kumpata mtoa huduma kamili baada ya kipindi cha mwaka mmoja cha mpito. Alisema kuwa Wakala unatarajia kuongeza mabasi mengine 165 kwa ajili ya kutoa huduma zaidi za usafiri katika jiji la Dar es salaam.

Alisema kuwa wakala unatarajia kuongeza njia za mrisho katika maeneo ya Mwenge, Kawe na Mabibo.

Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ulianza rasmi tarehe 16 Mei, 2016, ambapo umekwishatimiza mwaka mmoja katika kipindi cha mpito tangu kuanza kutolewa kwa huduma hiyo ambapo zimepangwa awamu sita za ujenzi wa miundombinu ya mradi huo katika maeneo mengine ya jiji la Dar es salaam huku awamu ya kwanza imekwishakamilika.

No comments: