Wednesday, June 7, 2017

MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI-IRINGA NA KASI YA UONDOSHAJI MASHAURI

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya
Hakimu Mkazi-Iringa, Mhe. David Ngunyale

Na Mary Gwera, Mahakama, Iringa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa imefanikiwa kuondosha Mashauri/kesi kwa zaidi ya asilimia tisini (90) na kuifanya Mahakama hiyo kuendana na azma ya Mahakama ya Tanzania ya kutoa haki kwa wakati ili kuondokana na mlundikano wa mashauri katika Mahakama zake nchini.
Akizungumza ofisini kwake katika mahojiano maalum na Mwandishi wa taarifa hii aliyepo Kanda ya Iringa, mapema Juni 6, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi-Iringa, Mhe. David Ngunyale alisema hali ya uondoshaji wa Mashauri katika Mkoa wa Iringa inaridhisha na kufafanua kuwa kwa upande wa Mahakama za Mwanzo ambazo jumla yake zipo 21, hakuna kesi inayozidi miezi sita (6) katika Mahakama hizo.
Akiongelea katika ngazi ya Mahakama za Wilaya, Mhe. Ngunyale alisema kuwa Mahakama hizo zina jumla ya kesi 12 za mlundikano (ambazo zimezidi umri ya miezi 12 Mahakamani), huku kesi 8 zikiwa ni za Jinai na nne (4) zikiwa ni kesi za Madai.
Hata hivyo; Mhe. Ngunyale alidai kuwa kuna sababu kadhaa ambazo zilipelekea kuwa na mlundikano huo akitaja kuwa ni pamoja na kutopatikana kwa mashahidi kwa wakati, upelelezi kutokamilika kwa wakati na kadhalika.
“Hata hivyo tunaweza kusema kuwa suala la umalizwaji wa kesi kwa wakati lipo vizuri kwa Kanda hii, na tumefanikiwa kwa asilimia 95, na hivyo kwenda sawia na Mpango Mkakati wa Mahakama wa kuhakikisha kuwa Mahakama zake zinatoa haki kwa wakati,” alisisitiza Mhe. Ngunyale.
Akiongelea juu ya upatikanaji wa nakala za hukumu, Mhe. Ngunyale alisema kuwa Wateja hupatiwa nakala za hukumu ndani ya siku 21 tangu kuamriwa kwa shauri/kesi husika.
Akizungumzia kuhusiana na Programu maalum ya uondoshaji mlundikano wa Mashauri Mahakamani linalohusisha mahakama zote nchini, Mhe. huyo alisema kuwa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa ni miongoni mwa Mahakama zilizotekeleza wito huo.
“Mahakama ya Hakimu Mkazi-Iringa ilianza Program hii kwa mara ya kwanza Machi, 27 mwaka huu kama ilivyopangwa na Makao makuu ya Mahakama, na katika awamu hii ya kwanza iliyokamilika Aprili 30, mwaka huu, tulifanikiwa kumaliza jumla ya mashauri 8 kati ya mashauri 9 yaliyokuwa yamepangwa kusikilizwa katika Programu hiyo,” alifafanua Hakimu Mkazi huyo.
Kwa upande mwingine Hakimu huyo Mfawidhi aliongeza kuwa, wamekuwa pia wakifanya kaguzi za mara kwa mara katika Mahakama za chini za mkoani humo (Mahakama za Wilaya na Mwanzo), lengo likiwa ni kufuatilia kwa karibu zaidi hali ya utoaji haki katika Mahakama hizo na endapo kuna madhaifu kuyafanyia kazi ili Mahakama zote katika Mkoa wa Iringa ziendane na kasi moja ya kumaliza mashauri kwa wakati.
Akizungumzia juu ya uhifadhi wa kumbukumbu za kesi za miaka ya nyuma na zinazoendelea, Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Iringa, Bw. Elvin Mwakajinga, alisema kuwa Kanda yake imefanikiwa katika kuhifadhi kumbukumbu zake za kesi.
“Mafaili ya kumbukumbu za kesi/mashauri ya miaka ya nyuma na zinazoendelea zimewekwa katika Maboksi maalum, mafaili hayo ya kumbukumbu za kesi yapo yaliyomalizika kati ya mwaka 1982 na 2005 yamepangwa kulingana na mwaka wa kesi husika kukamilika,” alifafanua Bw. Mwakajinga

Uhifadhi sahihi wa kumbukumbu za kesi hurahisisha upatikanaji wa haraka wa kumbukumbu hizo zilizomalizika kwa rejea endapo kuna uhitaji.

No comments: