WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba amewataka viongozi wa miradi ya kilimo inayofadhiliwa na serikalipamoja na mashirika ya misaada kuzingatia malengo ya kuanzishwa miradi hiyo ili kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.
Akizungumza katika skimu ya umwagiliaji ya Dakawa mkoani Morogoro hivi karibuni Dkt. Tizeba alisema wakulima hawana sababu ya kuwa na hiyari kwani fedha zinazotolewa ni nyingi na wahisani pamoja na serikali wanataka kuona matokeo ya misaada hiyo.
“Naomba unisikilize ndugu mwenyekiti, waliopewa pesa kwa ajili ya kilimo wasiwe na hiyari ya kulima, hatuwezi kuendelea kusikia tu wenzetu wanavuna tani nyingi katika mataifa mengine ikiwa sisi bado tunaendelea hivi hivi,” alisema Dkt. Tizeba na kusisitiza:“Anayetaka kukaa hapa kwenye skimu akae kwa kufuata masharti na asiyetaka aondoke apishe wengine.
USAID (Shirika la misaada la watu wa Marekani) kiasi walichotoa kinafikia Sh bilioni 29, tukizigawa kila mmoja anapata Sh milioni 60. Naombeni make halafu mkubaliane kuwa suala la kufanya kilimo cha hiyari katika maeneo tuliyofadhili hatutaki kusikia. Msimu ujao tunataka tuvune tani 12 katika skimu hii.”
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo, Dkt. Filimini Mizambwa amesema ili taasisi zinazosaidia wakulima ziendelee kuwepo lazima wakulima hasa wadogo waonyeshe tija katika shughuli wanazofanya ikiwemo kuonyesha matokeo mazuri wakati wa mavuno.
“Ili sisi tuendelee kuwepo lazima wakulima hasa mkulima mdogo fanikiwe, wito wangu wakulima wajifunze kilimo chenye tija na kufanya kazi kwa juhudi ili kuwaonyesha wafadhili fedha zao hazipotei bure kwa uzembe.
“Kazi yetu ni kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na kuongeza tija katika uzalishaji mazao, tunafanya kazi na sekta binafsi na sekta za umma, majukumu yetu ni kuongeza uzalishaji mbegu bora,” alisema Dkt. Mizambwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Bwana Geoffrey Kirenga alisema malengo ya ziara hiyo katika skimu ya umwagiliaji ya wakulima wadogo Mkondo na skimukubwa ya Dakawa yenye ukubwa wa Hekta 2000 inalenga kuangalia shughuli zinazofanyika na kuangalia changamoto zilizopo.
“Huu ni mfano mzuri wa utekelezaji wa dhana ya SAGCOT, ambayo ni ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma. Katika ziara hii kuna watu wa serikali na sekta binafsi, wakulima ni sehemu ya sekta binafsi,” alisema na kuongeza:
“Nawashauri wakulima wadogo wafuate kanuni bora za kilimo ili kuonyesha tija, zamani suala hili ilikuwa ni utashi wa mkulima lakini kwa sasa si suala la hiyari tena. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wa Kilimo asiyetaka atupishe ili tulete watu wengine.
Tumwekeza fedha nyingi za walipa kodi na fedha za wahisani lengo ni kuona mkulima anapata faida, ikiwa kinyume chake haitakuwa na maana hiki tunachokifanya.”Ziara hiyo ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa skimu hizo za umwagiliaji mkoani Morogoro utakaofanywa hivi karibuni na Rais Dkt. John Magufuli.
Miongoni mwa wafadhili wa shughuli za SAGCOT ni Serikali ya Tanzania, Ubalozi wa Norway, USAID, UKAID, Benki ya Dunia, UNDP na AGRA.
No comments:
Post a Comment