Friday, May 19, 2017

Wizara ya Mambo ya Nje yatoa elimu ya Mtangamano Pemba

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Issa Gavu akisoma hotuba ya kufunga semina kuhusu elimu ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zake. Semina hiyo iliandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilifanyika Pemba kuanzia tarehe 15 - 18 Mei 2017. Wengine katika picha, kushoto ni katibu wa Wizara hiyo, Bw. Salum Salum na Mkurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Eliabi Chodota. 
Kulia ni Mbunge wa Wete, Mhe. Ali Mbarouk akifuatilia kwa makini semina ya mtangamano. 
Washiriki wa semina hiyo ambao wengi wao walikuwa wajasiriamali wakisikiliza hotuba ya kufunga semina. 
Washiriki wengine wakifuatilia hotuba ya Mhe. waziri wa Nchi. 
Mhe. Waziri wa Nchi akiendelea kuwahutubia wana semina na watu wengine waliohudhuria sherehe za ufungaji. 
Picha ya pamoja kati ya Mhe. Gavu na washiriki wa semina. 
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Bi. Mindi Kasiga akiwasilisha mada kuhusu Diplomasia ya Umma kwa wana semina hiyo. 
Wajumbe wa semina wakisikiliza mada kuhusu Diplomasia ya Umma. 
Bi. Mindi akiendelea kuwasilisha mada. 
Prof. Ammon Mbelle kutoka Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam akiwasilisha mada kuhusu Sera ya Mambo ya Nje kwenye semina hiyo. 
Mchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Elly Chuma akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika Diplomasia yaUchumi. 
Wajumbe wa Semina wakifuatilia mada. 
Mjumbe wa Semina akichangia mada. 
Watoa mada wakipongezwa na wajumbe wa semina. 





Serikali ya Zanzibar imeahidi kuwa itaendelea na jitihada za kuimarisha huduma za kiuchumi kwa madhumuni ya kuweka mazingira mazuri ya kibiashara ili wananchi waweze kunufaika na fursa zinazopatikana kwenye Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Issa Gavu alipokuwa anafunga semina ya siku nne kuhusu mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zake iliyofanyika Pemba kuanzia tarehe 15 hadi 18 Mei 2017.

Mhe. Gavu alitoa wito kwa wanasemina hao ambao wengi wao walikuwa ni wajasiriamali kutengeneza bidhaa zenye ubora kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia ya ulimwengu wa sasa ili ziwe na uwezo wa kushindana na bidhaa nyingine katika soko la EAC.

Aidha, Mhe. Gavu aliahidi kuwa Serikali itasaidia wajasiriamali washiriki makongamano, semina, maonesho na warsha mbalimbaili zinazofanyika nchini na nje ya nchi ili iwe fursa kwao kujifunza mambo mapya yanayoendana na ulimwengu wa sasa kwa lengo la kuboresha biashara zao.

Mhe. Gavu aliwasihi wote waliopata na watakaopata fursa za mafunzo kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ili kwa pamoja watumie mbinu, ujuzi na uzoefu wanaoupata kukabili changamoto za ushindani wa soko kulingana na mahitaji ya sasa.

Alisisitiza umuhimu wa nchi zote wanachama wa EAC kuwahudumia raia wa nchi zote kwa usawa bila ubaguzi. Alisema endapo nchi moja ikiwa na tabia ya kunyanyasa raia wa nchi nyingine inaweza kusababisha dhana ya kulipiza kisasi hatimaye vurugu na kuleta mkanganyiko katika Jumuiya. 

Vile vile, Waziri wa Nchi alitoa wito kwa nchi zote wanachama kushirikiana kwa pamoja kudhibiti biashara ya magendo. "Sio sahihi kwa nchi moja kufumbia macho biashara ya magendo kwa kutochukua hatua dhidi ya wanaoingiza na kununua bidhaa za magendo". Mhe Gavu alisema. Zanzibar inakabiliwa na biashara ya magendo ya zao la karafuu ambayo inasafirishwa kwa njia za panya kwenda nchi za jirani.

Kwa upande wao wajasiriamali wameahidi kuwa watatumia mafunzo waliyopata kulikabili Soko la EAC bila khofu yeyote kama ilivyokuwa hapo awali.

Semina hiyo ya siku nne ilifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga na ilitolewa na wataalamu wa Wizara kwa kushirikiana na Prof. Ammon Mbelle kutoka Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 

Dar es Salaam, 18 Mei, 2017 

No comments: