Na MatukiodaimaBlog
SERIKALI wilaya ya kilolo mkoa wa Iringa imewataka wananchi wa wilaya hiyo wanaojishughulisha na kilimo cha mazao mbali mbali kuacha kuuza mazao yao kwa vipimo visivyo sahihi marufu kwa jina la Lumbesa na badala yake kuuza mazao kwa kutumia vipimo sahihi kama mizani .
Akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Irindi na Magana kata ya Mahenge wilayani Kilolo mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdala leo wakati wa ziara yake ya kukagua miundo mbinu ya elimu na uhamasishaji wananchi kushiriki shughuli za uzalishaji mali ,mkuu huyo alisema kuwa iwapo wananchi hao watakubali kuuza mazao yao kwa ujazo batili hatua kali itachukuliwa kwa muuzaji na mununuzi .
Hivyo aliwataka viongozi wa serikali za vijiji na kata zote kuwasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa faida na kuwabana walanguzi wa mazao wanaowapunja wakulima hao kwa kununua mazao kwa vipimo ambavyo vinawanyonya wakulima.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wilaya hiyo imejaliwa kwa kuwa na ardhi nzuri inayokubali mazao ya kila aina kama vitunguu,mahindi ,maharage ,njegere ,nyanya na mazao mengine mengi hivyo jukumu kubwa la mabwana shamba ni kuwasimamia wakulima hao dhidi ya walanguzi wa mazao yao na kuona kila mkulima ananufaika na kilimo na sio kuishia kuwanufaisha wafanyabiashara .
Alisema kuwa chini ya serikali ya Rais Dkt John Magufuli serikali inayowajali wananchi wake wote pasipo kuwabagua asingependa kuona Kilolo wafanyabiashara wakiwanyonya wakulima na kuwa kama walizoea kipindi kabla ya Dkt Magufuli hajaingia Ikulu basi ni vema watambue kuwa mwisho wa mkulima Kilolo kumnufaisha mfanyabiashara ama dalali wa mazao mwisho wake ulikuwa ni mwaka 2015 ila serikali hii ya awamu ya tano ipo kwa ajili ya watanzania wote .
Hivyo aliwataka wakulima wilaya ya Kilolo kuuza mazao yao kwa utaratibu na kwa kuzingatia vipimo sahihi vinavyotambuliwa na serikali na sio vinginevyo .
Meneja wa vipimo mkoa wa Iringa Zainabu Kafungo aliwaeleza wananchi hao kuwa kutokana na elimu mbali mbali ambayo imeendelea kutolewa na ofisi yake na viongozi wa serikali mkoani Iringa kasi ya wananchi kuuza mazao yao kwa vipimo visivyo sahihi imeendelea kupungua na hata wafanyabiashara hasa madalali wa mazao wameendelea kuogopa kuwaibia wakulima .
Alisema kuwa ofisi yake ni wakala wa serikali inayosimamia vipimo vyote nchini Tanzania bara lengo ni kuhakikisha kunakuwepo na usahihi wa bidhaa zinazofungashwa kwa ajili ya kumlinda mlaji asipunjwe kutokana na vipimo apate huduma kulingana na pesa yake .
Pia kumlinda mlaji kwa kufanya kaguzi za bidhaa zilizofungashwa mashambani toka kwa wakulima kuwa zinakuwa kwenye vipimo sahihi na sio lumbesa
Aidha alisema ufungashaji batili ni ufungashaji kinyume na sheria ya vipimo sura 340 mapitio ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake japo alisema kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya viongozi maeneo kuhamasisha wananchi kutotii sheria na baadhi ya taasisi kuandaa kanuni zao bila kurejea sheria ya vipimo .
Sheria inataka kiasi cha ufungashaji kwa uwele ,karanga ,ufuta,wimbi ,mtama ,maharage na jamii yake kilo 90 tu wakati alizeti kilo 40,mkaa kilo 30, viazi ,mazao mengine ambayo hayajatajwa ni kilo 100,korosho kilo 80 na kuwa faini mbali mbali zipo wazi kwa wakiukwaji wa sheria kwa Yule atakayekiuka sheria ya vipimo hufikishwa mahakamani faini yake si chini ya 300,00 na si zaidi ya shilingi 50,000,000 au kifungo kisichozidi miwiliau vyote kwa pamoja .
Mkuu wa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa Asia Abdalah akiwataka wananchi wa kijiji cha Irindi na Magana kata ya Mahenge kuachana na uuzaji mazao kwa vipimo batili |
Wananchi wa wakiendelea kusoma vipeperushi vya elimu sahihi ya vipimo wakati mkutano wa DC ukiendelea |
Mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdalah akiwahutubia wananchi mwenye kilembe cha madoa mekundu ni meneja wa vipimo mkoa wa Iringa Zainabu Kafungo. |
No comments:
Post a Comment