Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dr. Idrisa Muslim Hija amelishauri
Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) na Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuangalia uwezekano wa kuanzisha taasisi
maalum itakayoshughulikia tafiti za kitaalamu juu ya zao la karafuu.
Alitoa ushauri huo wakati akizungumza na Wakulima na Wadau wa zao la
karafuu katika mkutano maalum ulioandaliwa na Shirika la ZSTC kwa
Wakulima na wadau wa zao hilo Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema kutokana na zao la karafuu kuendelea kuwa uti wa mgongo wa
uchumi wa nchi na wananchi wake ambapo wananchi wengi wanaonyesha nia
na ari ya kulima zao hilo hivyo wanahitaji msaada mkubwa wa kitaalamu
juu ya ukulima wa zao hilo.
Alisema endapo itaanzishwa taasisi hiyo ya utafiti itatoa majibu ya
changamoto zinazokabili zao hilo mashambani ikiwemo udongo unaokubali
kuota mikarafuu, njia bora za upandaji, mbegu bora, maradhi na tiba
yake.
Alisema pamoja na kuwepo kwa Wizara ya kilimo na Shirika la ZSTC
ambazo zinatoa huduma za uimarishaji wa zao hilo la karafuu lakini
taasisi hizo zina majukumu mengine zaidi hivyo itakuwa ni busara
endapo itaanzishwa taasisi maalum itakayohusika moja kwa moja kufanya
utafiti na kuja na majibu ya kitaalamu.
Akizungumza na Wakulima na Wadau wa zao la karafuu wa Mkoa wa Kusini
Pemba kwa nyakati tofauti Mkuu wa Mkoa huo Bi. Mwanajuma Majid
Abdalla, aliwakumbusha Wakulima wa zao hilo la karafuu kuendelea
kulinda ubora, kuacha kabisa magendo na kuuza karafuu zote Serikalini
kupitia vituo vya ununuzi vya ZSTC.
Alisema Sheria ya Maendeleo ya Karafuu Na. 2 ya mwaka 2014 ipo kwa
ajili ya kulinda zao la karafuu kwa maslahi ya nchi na wananchi wake
ambapo aliwataka Masheha kuwafahamu wakulima wa zao la karafuu katika
shehia zao ili kuimarisha ulinzi.
Aliwataka Masheha kuhakikisha karafuu hazihamishwi kutoka sehemu moja
kwenda nyengine kinyume na utaratibu uliowekwa wa kuomba kibali ambapo
alifahamisha kuwa uhamishaji kiholela unaweza kupelekea watu waovu
kutumia nafasi hiyo kusafirisha magendo.
Aidha Bi. Mwanajuma aliwasisitiza Wakulima na Wadau wa zao la karafuu
kujisajili haraka kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Shirika la ZSTC
ili kunufaika na huduma za uendelezaji wa zao la karafuu.
Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali
Mohamed Shein anaonyesha imani kubwa na wakulima wa zao la karafuu
hivyo huduma kwa wakulima hao zitaendelea kutolewa hivyo ni vyema
wakulima wote na wadau wa zao la karafuu wakajisajili ili wafahamike
rasmi na kupatiwa huduma.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar Khamis Othman alisema hataki
kuona mkoa wake ukichafuliwa kwa biashara za magendo ya karafuu wala
kuwepo kwa viwanda vya kuchafua karafuu kwa makusudi.
Akizungumza na Wakulima na Wadau wa zao la karafuu kwa nyakati
tofauti, alisema Mkoa huo wa Kaskazini unazungumzwa sana kwa magendo
ya karafuu kutokana na bahari yake kupakana na nchi za jirani hivyo
inawezekana waovu wanatumia kama njia ya kutoroshea karafuu, alisema
hatokubali vitendo hivyo viendelee kutokea katika Mkoa wake.
Aliwataka Wakulima katika Mkoa huo kufuata maagizo wanayopewa na
wataalamu juu ya kulinda ubora wa zao la karafuu na kuacha kabisa
kuanika karafuu barabarani, juu ya mabati, sakafuni na kuchafua kwa
makusudi.
Akiwasilisha tathmini ya manunuzi ya karafuu mwaka 2016/2017 katika
mikutano hiyo Mkurugenzi Fedha wa Shirika la ZSTC Imail Omar Bai
alisema katika mwaka huo wa 2016/2017 hadi kufika tarehe 30/04/2017
Shirika limenunua karafuu kutoka kwa Wakulima jumla ya tani 2,266.2
zenye thamani ya TZS 31.8 bilioni Unguja na Pemba.
Alifafanua kuwa Unguja zimenunuliwa tani 132.5 kwa thamani ya TZS 1.8
bilioni na Pemba zimenunuliwa tani 2,133.7 kwa thamani ya 29.9
bilioni. Manunuzi hayo ni sawa na asilimia 81 ya makadirio
yaliyowekwa na Shirika la ZSTC kwa mwaka wa 2016/2017.
Alifahamisha kuwa makadirio kwa mwaka wa 2016/2017 ilikuwa ni kununua
tani 2,810, Unguja tani 160.0 na Pemba 2,650.0 ambapo aliwapongeza na
kuwashukuru Wakulima na Wafanyabiashara ya karafuu kwa kuuza karafuu
zao Serikalini kupitia vituo vya ununuzi vya ZSTC.
Kwa upande wao Wakulima na Wadau wa zao la karafuu waliendela
kuipongeza na kuishukuru Serikali kwa namna wanavyoshirikiana na
Wakulima katika kulihudumia zao la karafuu.
Pamoja na pongezi hizo Wakulima hao waliendelea kuiomba Serikali kuwa
karibu na kuzidisha huduma zaidi kwa Wakulima wa zao hilo la sekta ya
karafuu kwa jumla kwa vile uimarishaji wa zao hilo ni kazi ngumu.
Walifahamisha kuwa kumekuwa na kipindi kirefu cha jua na joto
limeongezeka kunakosababisha uotaji na ukuaji wa mikarafuu kuwa mgumu
hivyo kuhitaji jitihada zaidi za wakulima. Waliomba Serikali kuangalia
uwezekano wa kusaidia huduma za maji katika mashamba ya mikarafuu
ikiwemo kuwachimbia visima.
Wakibainisha changomoto nyengine kubwa katika ukulima wa zao hilo la
karafuu wakulima hao walisema kuwa wafugaji wamekuwa tatizo kubwa kwao
kutokana na tabia zao za kuingiza mifugo yao katika mashamba ya
mikarafuu na kuathiri zao hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dr. Idrisa Muslim Hija akimkabidhi kitambulisho cha ukulima wa zao la karafuu Mmoja kati ya wakuliwa wa zao hilo.
Baadhi ya Wakulima wa zao la karafuu Mkoa wa Kusini Unguja
wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mkoa huo.
No comments:
Post a Comment