Wednesday, May 24, 2017

RAIS ABBAS: UHURU WA PALESTINA NDIO UFUNGUO WA KUPATIKANA KWA AMANI NA UTULIVU

Rais mahmuud Abbas  na mwenzake Donald Trump,wakiwa katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Beit Lehem

Rais Mahmuud Abbas wa Palestina amesema kwamba,Matakwa ya wafungwa wa kipalestina walio katika jela za Israeli ni ya haki na ni wajibu wa Israli kuyatekeleza, vilevile kupatikana kwa uhuru wa taifa lake ndio ufunguo wa amani na utulivu katika ukanda huo wa Mashariki ya Kati na Dunia nzima kwa ujumla.

Rais Abbas ameyasema hayo jana Jumanne Ikulu mjini Beit Lehem, alipokuwa na mkutano wa pamoja na mgeni wake Rais Donald Trump wa Marekani, huku akitilia mkazo dhamira yake ya kushirikiana nae katika kufanikisha mpango wa amani wa kihistoria na Waisraeli,pia kushirikiana nae Rais Trump kama washirika katika suala zima la kupiga vita Ugaidi duniani.

Mheshimiwa Rais Mahmuud Abbas pia ametilia mkazo msimamo wa Palestina unaotegemea utatuzi wa uwepo wa dola mbili chini ya mipaka ya mwaka 1967, ambazo ni dola ya Palestina ikiwa na mji mkuu wake Jerusalemu ya Mashariki na dola ya pili ni Israeli,huku ukipatikana utatuzi wa mwisho kabisa wa masuala yote husika, kwa misingi ya maazimio ya kisheria za kimataifa na makubaliano ya pande mbili za Palestina na Israeli.

Aidha Rais Abbas ametilia mkazo pia kwamba mzozo uliopo sio wa kidini,kwani kuheshimu dini zote na mitume yake ni sehemu ya imani ya taifa la Palestina, bali tatizo lililopo ni uvamizi, ujenzi wa makazi ya walowezi na kutokubali Israeli uwepo wa dola ya Palestina.

Rais Abbas pia amezungumzia usumbufu wanaoupata wafungwa wa kipalestina wanaoendelea na mgomo wa kula uliofikisha siku 37 mfululizo katika jela za Israeli,huku akitilia mkazo ya kwamba madai yao  ni ya kibinaadamu na ya haki,ni wajibu wa Israeli kuyatekeleza.
Kwa upande mwingine,Rais Abbas amelaani vikali shambulio baya  la kigaidi, lililotokea hivi karibuni mjini Manchester Uingereza lililopelekea vifo kadhaa na majeruhi,huku akitoa rambirambi zake za dhati kabisa kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo na familia za wahanga hao.

Rais Abbas pia amemsifu Rais Trump kwa mapokezi mazuri ya hivi karibuni katika Ikulu ya Marekani na yaliyojiri katika mazungumzo yao, kwani yamewapa Wapalestina matarajio mapya ya kufikia ndoto yao ya muda mrefu,nayo ni kufikia  katika amani ya kudumu iliyo katika misingi ya haki na usawa. Pia amesifu umuhimu wa kufanyika mkutano wa pamoja wa wakuu wa kiarabu,kiislamu na kimarekani,kilichofikia maazimio kadhaa hivi karibuni.

Mwishowe Rais Abbas amemkaribisha tena Rais Trump wa Marekani na ujumbe wake kuitembelea Palestina,huku akiwaombea ufanisi katika ziara yao itakayowafikisha kuonana na Papa Francis,ambae tunathamini sana mchango wake wa kuleta amani.Rais amemalizia kwa kutamani historia imuandike Rais Donald Trump kuwa ndiye Rais wa Marekani aliyeweza kuleta amani na utulivu kati ya Palestina na Israeli.

Nae Rais Trump kwa upande wake, amesema anatarajia kufanya kazi kikamilifu na Rais Abbas  ili kuleta amani na utulivu Mashariki ya Kati,kuinua uchumi wa Palestina na kupiga vita ugaidi. Ameongeza kuwa,mchakato wa kuleta amani ni lazima ufanyike katika mazingira yasiyo na vurugu,huku nchi yake itasaidia pande mbili hizo ili kufikia ufumbuzi wa kudumu.



Amesisitiza kuwa wamekuja mjini “Beit Lehem” ambao ni mji wa amani ili kushirikiana katika kuleta dunia iliyo na amani, wanaamini kuwa Palestina  na Israeli zinaweza kufanya hivyo,huku akimpongeza Rais Abbas kwa kuhudhuria Mkutano wa mjini Riyadh Saudi Arabia, ulioshirikisha viongozi wa kiarabu,kiislamu na Marekani kwa lengo la kupiga vita Ugaidi na misimamo mikali ya kiitikadi.

No comments: