Wachimbaji wadogo wa madini nchini wametakiwa kuepuka ajali zisizo za
lazima kwani tangu mwaka 2008 hadi Mei 2017 zimetokea ajali 125 kwenye
migodi yenye leseni na vifo ni 213.
Ajali zilizotokea kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wasio na leseni
nchini (maeneo ya mifumuko ya uchimbaji madini) katika kipindi hicho
ni 56 na kusababisha vifo vya wachimbaji 140.
Kamishna
wa madini nchini, mhandisi Benjamin Mchwampaka aliyasema hayo wakati
akizungumza na mameneja na wamiliki wa migodi mji mdogo wa Mirerani,
wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Mhandisi Mchwampaka alisema ajali nyingi kwenye migodi ya wachimbaji
wadogo zinasababishwa na uzembe, kwani kwa mwaka huu pekee hadi Mei 15 ajali zilizotokea ni 11 na kusababisha vifo 26.
Alisema kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani,
ajali zilizotokea kwa wachimbaji wadogo kwa kipindi cha 2008/2017 ni
31 na wachimbaji wadogo waliopoteza maisha ni 40.
Alisema uchambuzi wa takwimu za ajali hizo unaonyesha kuwa vyanzo
vikubwa ni kuangukiwa na vifusi kwa kukatika kwa ngema, kulipukiwa na
baruti, kukosa hewa, kuteleza na kuangukia mgodini.
Alisema hawatafumbia macho ajali za uzembe kwenye migodi na
wataifungia mara moja na kumchukulia hatua meneja na mmiliki,
haitafunguliwa hadi mkaguzi mkuu wa migodi atakapojiridhisha.
“Tunapaswa kuhakikisha uchimbaji unafanyika kwa usalama na kauli mbiu
ya wachimbaji wadogo nchini iwe usalama kwanza, familia zetu
zinatuhitaji na Taifa linatuhitaji,” alisema mhandisi Mchwampaka.
Mkaguzi mkuu wa migodi nchini, mhandisi Ally Samaje alisema lengo la
mafunzo hayo ni kupunguza matukio ya ajali zinazoweza kuepukwa na
wachimbaji wadogo hivyo mafunzo hayo yatawajengea uwezo.
Mhandisi Samaje alisema kila mmiliki wa leseni ya madini anazingatia
maelekezo yote waliyoyatoa kwa kufanya kazi zao kwa usalama, kwani
ajali hizo zimesababisha vifo na vilema vya maisha.
“Kamishna wa madini ameshatoa maelekezo ya kuimarisha masuala ya
usalama, afya na utunzaji mazingira hivyo wamiliki wa migodi wawape
majukumu mameneja wayasimamie hayo,” alisema Samaje.
Mmoja kati ya wamiliki wa migodi Hamis Juma aliishukuru wizara ya
Nishati
na Madini kwa kuendesha mafunzo hayo kwa mameneja na wamiki wa migodi
kwani elimu hiyo itasaidia kupunguza ajali mgodini.
“Kupitia elimu hii tumekumbushwa wajibu wetu na pia mameneja na
tunatarajia watatekeleza hayo kwa faida ya wachimbaji wenyewe na jamii
inayoishi maeneo yanayozunguka migodi yetu,” alisema Juma.
Viongozi
wa Wizara ya Nishati na Madini, Chama cha wachimbaji wadogo wa Madini
Mkoani Manyara, (Marema) na wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mji mdogo
wa Mirerani Wilayani Simanjiro, wakiwa kwenyemafunzo ya usalama
migodini.
Kamishna
wa madini Tanzania, mhandisi Benjamin Mchwampaka akizungumza na
wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani
Simanjiro Mkoani Manyara, kuhusiana na usalama kwenye migodi yao.
Viongozi
wa Wizara ya Nishati na Madini, Chama cha wachimbaji wadogo wa Madini
Mkoani Manyara, (Marema) na wachimbaji wa madini ya Tanzanite Mji mdogo
wa Mirerani Wilayani Simanjiro, wakiwa kwenye
mafunzo ya usalama migodini.
No comments:
Post a Comment