Wednesday, May 17, 2017

NAIBU KATIBU MKUU CCM BARA ZIARANI JIMBO LA TEMEKE, ASEMA HANUNULIWI KWA 'JERO'


Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Rodrick Mpogolo, akizungumza na wanachama na Viongozi wa CCM Kata ya Mtoni, wakati akiwa katika mfululizo wa ziara zake za kuimarisha Chama, kwa Mkoa wa Dar es Salaam,jana.



Na Ripota wa Mafoto Blog, Dar

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM (Bara) Rodrick Mpogolo,amesema hakuna mtu anayeweza kukinunua Chama Cha Mapinduzi, kwa kuwa ni Chama kikubwa kilichoanzishwa na waasisi makini.

Amesema waasisi walizingatia misingi ya haki umoja na mshikamano ,wakaondoa dhulma, chuki na ubaguzi wa kila aina hivyo si rahisi mtu kufanya biashara na CCM.

Mpogolo alisema hayo jana alipozungumza na viongozi na wanachama wa CCM katika majimbo ya Temeke na Mbagala jijini Dar es Salaam,ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kuimarisha Chama.

Alisema CCM inaendesha shughuli zake kwa uhuru na itahakikisha uchaguzi wake unafanyika kwa haki pasipo kuingilia na wanachama wenye tabia ya kununua madaraka.

Mpogolo aliwaagiza watendaji wa Chama na jumuiya kusimamia uchaguzi unaendelea kufanyika kwa haki bila kuwashinikiza wanachama kwa kuwa wanawafahamu viongozi wanaowataka.

"Hatutaki vurugu CCM, tunapenda amani,umoja na mshikamano. Wenye ni ya kutumia uchaguzi huu kupanga mitandao yao, wataambulia patupu,watatumia fedha na uongozi hawatapata,"alisema.

Aliwaonya wenye nia ya kuwagawa wanachama kwa misingi ya udini na ukabila kuacha mara moja kwa kuwa CCM haina dini wala kabila na wanachama wako huru kuchagua kiongozi anayefaa bila kujali dini wala kabila yake.

Akizungumzia mabadiliko ndani ya Chama, Mpogolo alisema yanalenga kurejesha nguvu ya Chama kwa wanachama ,kwa kujenga mashina yenye nguvu huku balozi akiwa jukumu kubwa kuisimamia serikali.

Alisema mabadiliko hayo yanataka kwenye shina kuwe na wanachama 50 hadi 150 ili kuongeza nguvu ya Chama . Aliwataka wanachama na viongozi kujenga umoja,upendo ili wawe kivutio kwa wengine wajiunge na CCM.

"Katika ziara yangu nilifika Namtumbo nikakaribishwa nyumbani kwa balozi, akiwa na wanachama wake 50,akanieleza kwamba wana kero ya maji ,nikamsimamisha diwani aeleze mipango ya kutatua kero hiyo.Pale ndio niliona nguvu ya balozi,"alisema.

Wakizungumza baada hotuba hiyo ,baadhi ya wanachama na viongozi walimshukuru Mpogolo kwa ziara hiyo iliyosheheni mikakati ya kukijenga Chama na kuwaonya watendaji jambo ambalo.

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Saad Kusilawe, alisema Chama kimejipanga vizuri kukomboa majimbo yote ya mkoa huo, hivyo ziara yake imeongeza nguvu kwenye mikakati inayoendelea kutekelezwa.

Alisema kutokana na ziara hiyo ,anaamini uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu bila malalamiko wala upendeleo na kila ngazi itapata viongozi bora watakaoshirikiana na wanachama kukivusha Chama kwenye uchaguzi ujao.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dar es Salaam,Janneth Masaburi, alisema ziara hiyo itasaidia kuwajenga kisiasa ili waendane na kasi ya mabadiliko ya ujenzi wa Chama na kasi ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli.

Alisema Mpogolo amegusa mambo muhimu, ambayo yatasaidia wanachama kufanya uchaguzi huru na viongozi wa mkoa wataendelea kuelimisha wana CCM ili kujiimarisha zaidi.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam Mariam Kisangi, alisema Naibu Katibu Mkuu Mpogolo, anatoa elimu muhimu juu ya dhamira ya Chama ya kujenga mashina na kuongeza wanachama.

Alisema ziara hiyo imejenga hamasa na wanachama wameelimishwa kuepuka chuki na kujenga upendo miongoni mwao jambo ambalo ni muhimu hususan kwa kipindi cha uchaguzi. 
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Rodrick Mpogolo, akiwasili kwenye Ukumbi wa Kijichi Mbagala kwa ajili ya kuzungumza na wanachama na Viongozi wa CCM.
Naibu Katibu Mkuu, Rodrick Mpogolo akiwasili ukumbini (kushoto) ni Mkubwa Fela akiwa ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliohudhuria mkutano huo.
Wanachama wa CCM wakiimba wimbo maalum
Akipokelewa na wanachama wa Kijichi
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Rodrick Mpogolo, akisalimiana na baadhi ya Viongozi wa CCM Kata ya Mtoni, wakati akiwa katika mfululizo wa ziara zake za kuimarisha Chama, kwa Mkoa wa Dar es Salaam,jana. 
Vijana wa Kikundi cha Hamasa cha CCM Kata ya Mtoni, wakisebeneka wakati wa mapokezi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Rodrick Mpogolo, alipokuwa katika ziara ya kuimarisha Chama Mkoa wa Dar es Salaam. 
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Rodrick Mpogolo, akizungumza na wanachama na Viongozi wa CCM Kata ya Mtoni, wakati akiwa katika mfululizo wa ziara zake za kuimarisha Chama, kwa Mkoa wa Dar es Salaam,jana. 
Baadhi ya Wanachama wa CCM Kata ya Mtoni wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Rodrick Mpogolo.

Wazee wa CCM wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Rodrick Mpogolo, katika Ukumbi wa CCM Mtoni.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Rodrick Mpogolo, akiwasili kwenye Ukumbi wa CCM Mtoni kwa ajili ya kuzungumza na wanachama na Viongozi wa CCM Kata ya Mtoni, wakati akiwa katika mfululizo wa ziara zake za kuimarisha Chama, kwa Mkoa wa Dar es Salaam,jana.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva (kushoto) akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Rodrick Mpogolo, wakati alipomtembelea ofisini kwake alipokuwa katika ziara yake ya kuimarisha Chama katika Jimbo la Temeke jijini Dar es Salaam jana.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo, akizungumza kutoa shukrani zake kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala (hawapo pichani) kwa mapokezi, wakati akiwa katika ziara yake ya kuimarisha Chama kwa Jimbo la Temeke jana. 
Picha ya pamoja baada ya mazungumzo
Naibu akiagana na baadhi ya Viongozi ofisini kwa Mkuu wa Wilaya

No comments: