Sunday, May 14, 2017

TFDA: DAWA ZILIZOPO SOKONI ZINA UBORA WA ASILIMIA 98

Frank Mvungi-Maelezo

Serikali imewahakikishia wananchi kuwa dawa zilizopo katika soko zina ubora kwa asilimia 98 na itahakiksha zinaendelea kukidhi vigezo vya ubora kama zilivyokuwa wakati zinasajiliwa kwa mujibu wa sheria, kanuni,miongozo na taratibu za udhibiti.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliolenga kueleza mikakati ya Mamlaka hiyo katika kudhibiti ubora na usalama wa chakula,dawa,vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya za wananchi.

“Katika maabara ya TFDA inayokidhi ithibati ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kati ya sampuli za dawa 199 za Binadamu zilizochunguzwa,sampuli 184 sawa na asilimia 92.5 zilikidhi vigezo vya ubora na sampuli za dawa 10 aina ya Ergometrine ya sindano ambayo ni sampuli 5 sawa na asilimia 2.5 hazikufikia ubora kwa kuwa na kiasi cha kiambata hai chini ya kiwango kinachokubalika.”Alisisitiza Sillo

Akifafanua Sillo amesema kabla ya dawa kusajiliwa na TFDA na hatimaye kuruhusiwa kuingia katika Soko,zinafanyiwa tathmini ya Ubora,Usalama na ufanisi sanjari na ukaguzi wa mifumo ya utengenezaji bora Kiwandani na hizo ni hatua za awali za mifumo ya udhibiti wa dawa duniani.

Pia Sillo aliongeza kuwa dawa zinapokuwa katika soko zinafuatiliwa na TFDA kuona kama zinaendelea kukidhi vigezo vya ubora hadi tarehe ya mwisho ya matumizi (expiry date) ambapo utaratibu huu hujulikana kama Post- Marketing Surveillance au Market Control kwa mujibu wa mwongozo wa shirika la Afya Duniani (WHO) na ulianza kuwekwa na TFDA tangu mwaka 2007.

Katika utaratibu huo kila mwaka sampuli za dawa za aina tofauti zinachukuliwa na wakaguzi kutoka katika soko Zahanati,Vituo vya Afya, Hospitali,maduka ya dawa na maghala ya kuhifadhia dawa ya umma na binafsi na kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara.

Vigezo vinavyotumika kuchagua dawa zinazofanyiwa ufuatiliaji ni pamoja na dawa zenye matumizi makubwa,dawa za kutibu magonjwa ya makundi maalum kama watoto na akina mama wajawazito,dawa zenye historia ya kushindwa kustahili mazingira mbalimbali ya usafirishaji na utunzaji (unstable products)

Kwa kipindi cha mwaka 2012/2015 Sillo alibainisha kuwa dawa zilizofanyiwa ufuatiliaji ili kuona ubora wake ni pamoja na dawa za kutibu malaria,dawa aina ya vijiua sumu (Antibiotics) Dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi,dawa za kupunguza maumivu,dawa za kutibu kisukari,dawa za kutibu magonjwa ya moyo,dawa za kuzuia kutoka damu nyingi wakati wa kujifungua aina ya misoprostol.

Katika kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi machi 2017, TFDA ilifuatilia katika soko,ubora wa dawa za binadamu aina ya Albendazole vidonge,mchnaganyiko wa dawa ya vidonge aina ya Diclofenac na paracetamol,dawa ya macho yenye mchanganyiko wa Dexamethazone na Neomycin,dawa za mifugo aina ya Oxytetracycline 10% na 20 ambazo uchunguzi wake uko katika hatua za mwisho na matokeo yatatolewa mara yatakapokuwa tayari.

Aidha Sillo amesema kuwa mfumo wa kufuatilia usalama wa dawa katika soko unafanya kazi vizuri hapa nchini tangu mwaka 1989 na umeendelea kuboreshwa ambapo oktoba 2016 tulianzisha mfumo wa utoaji taarifa za madhara ya dawa kielekroniki kwa kutumia simu ya kiganjani.

Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania(TFDA) kwa mujibu wa Sheria ya Chakula,Dawa na Vipodozi,sura ya 219 ina jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa chakula,dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda Afya za wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) Hiiti Sillo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi yake leo Jijini Dar es Salaam.
: Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) Hiiti Sillo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi yake leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja Majaribio ya Dawa na Ufuatiliaji kutoka Mamlaka hiyo Bi. Kissa Mwamwitwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) Hiiti Sillo (katikati) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari wakati wa mkutano wake na waandishi wahabari( hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi yake leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Meneja wa Kanda ya Mashariki wa TFDA, Emmanuel Alphonce na Meneja Majaribio ya Dawa na Ufuatiliaji kutoka Mamlaka hiyo Bi. Kissa Mwamwitwa.Picha zote na: Frank Mvungi – MAELEZO.

No comments: