Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akijibu hoja mbalimbali wakati akihitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2017/2018 bungeni mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo makani akijibu hoja mbalimbali wakati wa kuhitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2017/2018 bungeni mjini Dodoma.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, Viongozi wakuu na baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo wakiwa nje ya lango la Bunge mara baada ya kikao cha Bunge kupitisha bajeti ya Wizara hiyo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo makani akijibu hoja mbalimbali wakati wa kuhitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2017/2018 bungeni mjini Dodoma.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, Viongozi wakuu na baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo wakiwa nje ya lango la Bunge mara baada ya kikao cha Bunge kupitisha bajeti ya Wizara hiyo.
Na Hamza Temba - WMU
Serikali inafikiria kuunganisha taasisi zote zinazohusika na
sekta ya uhifadhi wa wanyamapori nchini kuwa chombo kimoja chenye nguvu
kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi hizo pamoja na
kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika sekta hiyo muhimu hapa nchini.
Akizungumza mwishoni mwa wiki bungeni mjini Dodoma wakati
akihitimisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alisema anaunga mkono ushauri
uliotolewa na wabunge mbalimbali ukiwemo wa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashasta Nditiye juu ya umuhimu wa
kuunganisha taasisi hizo za uhifadhi.
"Wakati umefika sasa, tusiwe na makampuni (taasisi) zaidi
ya manne ndani ya sekta hii ya wanyamapori, tuwe na kampuni (taasisi) moja tu
ambayo itapunguza gharama katika uendeshaji, tutaunganisha jeshi la wahifadhi
na jeshi hilo tutakalolitengeneza ni jeshi moja tu ambalo litakua na malezi
chini ya jeshi la wananchi wa Tanzania, ili kujenga nidhamu, kuheshimu haki za
binadamu na kufanya kazi kwa mujibu wa maslahi ya taifa,". alisema
Maghembe.
Aliongeza kusema "Jeshi hilo ambalo tunaliandaa kisasa,
jeshi usu litakua na "chain ya comand" moja na litawajibika kijeshi
kwa makosa ya haki za kibinadamu na usaliti wa taifa au usaliti wa uchumi wa
nchi yetu".
Awali akiwasilisha bungeni hapo hotuba ya makadidirio ya mapato
na matumizi ya Wizara yake, Prof. Maghembe alizitaja taasisi hizo kuwa ni
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la
Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) na
Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) lilianzishwa mwaka 1959 kwa
Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura 282 na kupewa dhamana ya kusimamia na
kuendeleza maeneo yaliyoanzishwa kisheria kuwa Hifadhi za Taifa. Hifadhi hizo
ambazo zipo 16 zina jumla ya kilometa za mraba 57,365.80.
Kwa upande wake, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA)
ilianzishwa kwa Sheria Sura 284 na kupewa jukumu la kusimamia eneo la kilometa
za mraba 8,292 kwa ajili ya kuhifadhi, kuendeleza utalii na wafugaji wenyeji wa
eneo hilo ambapo wakati mamlaka ikianzishwa walikua takriban 8,000 mwaka 1959
na idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia zaidi ya wakazi 90,000 mwaka uliopita,
2016.
Nayo, Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA)
ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Na.135 la tarehe 9 Mei, 2014 chini ya
Kifungu cha 8 cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura 283 ikisomwa pamoja na
marekebisho yake yaliyotolewa katika Tangazo la Serikali Na.20 la tarehe 23
Januari 2015. Mamlaka hiyo ilianza kazi rasmi tarehe 1 Julai, 2016.
Mamlaka hiyo ina jukumu la kusimamia uhifadhi wa wanyamapori
kwenye Mapori ya Akiba 28, Mapori Tengefu 42 na maeneo ya wazi yenye
mazalia ya wanyamapori, mtawanyiko na shoroba. Aidha, Mamlaka inashirikiana na
jamii katika kusimamia maeneo 22 ya jumuiya za hifadhi za wanyamapori na maeneo
manne ya ardhioevu yenye umuhimu wa kimataifa (Ramsar Sites).
Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ilianzishwa
kwa Sheria Sura 260 kwa lengo la kusimamia, kufanya na kuratibu utafiti wa
wanyamapori nchini. Taasisi hiyo ina wajibu wa kutoa ushauri kuhusu uhifadhi
endelevu wa wanyamapori kwa kutumia matokeo ya utafiti wa kisayansi. Aidha,
TAWIRI inawajibu wa kufanya Sensa ya makundi mbalimbali ya Wanyamapori ili
kushauri Wahifadhi na Serikali.
Akizungumzia umuhimu wa uhifadhi wa Wanyamapori, Prof. Maghembe
alisema sekta ya maliasili kwa ujumla inachangia asilimia 21.4 ya pato lote la
taifa, ambapo mchango wa wanyamapori kupitia utalii ni asilimia 17.5 na misitu
asilimia 3.9. Aliongeza kuwa wanyamapori pia husaidia katika tafiti mbalimbali
duniani kwa ajili ya utafutaji wa dawa za kutibu maradhi ya binadamu.
Katika mwaka huu wa fedha 2017/2018, Bunge limeidhinisha Sh.
bilioni 148.597 kwa ajili ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya
Maliasili na Utalii, ambapo Sh. bilioni 96.794 ni kwa ajili ya Matumizi ya
Kawaida na Sh. bilioni 51.803 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment