Sunday, May 7, 2017

Serikali inafanyia kazi vikwazo biashara ya Madini - Kamishna wa Madini

 Kamishna wa Madini Tanzania Mhandisi Benjamini Mchwampaka akizungumza jambo wakati wa Kufunga Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito ya Arusha.
Waziri wa Madini na Maendeleo ya Viwanda wa Nigeria, Abubakar Bwari (katikati) akiangalia ubora wa Madini ya Tanzanite katika banda la kampuni ya Hadjarat Mining and Gemstone Company Limited. Aiiyeshika kifaa cha kupima ubora wa madini  ni Mkurugrenzi wa Kampuni hiyo.

Na Asteria Muhozya, Arusha
Wadau wa Madini nchini wametakiwa kujikita katika shughuli za ukataji na usanifu wa madini badala ya kusanifiwa nje ya nchi ili kuwezesha  adhma ya Serikali ya Tanzania ya Viwanda kupitia  Sekta ya Madini.
Hayo yalisemwa na Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi  Benjamini Mchwampaka wakati wa kufunga Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito yaliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 3-5 Mei,2017.
Aliongeza kuwa, uwepo wa shughuli za ukataji na unga'rishaji wa madini hayo nchini kutawezesha kuyaongezea thamani ikiwemo kupanua wigo wa ajira kupitia sekta ya madini.
" Tanzania ya sasa ni ya Viwanda. Na sisi sekta ya madini tuwe na viwanda vyetu  vya kusanifu madini yetu hapa hapa nchini. Kwanza tutayaongezea thamani madini yetu lakini pia tutazalisha ajira kwa wingi," alisema Mchampaka.
Aidha, Kamishna  Mchwampaka  aliongeza kuwa, tayari Wizara ya Nishati na Madini imewasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri  ya  biashara ya Madini nchini ili kuondoa kero  ambazo ni kikwazo  katika biashara hiyo kwa watanzania.
"Tunataka kuweka mazingira mazuri zaidi kwa wafanyabiashara wa madini wa Tanzania lakini pia tunapenda wafanyabiashara wetu washiriki kwa wingi katika maonesho haya. Ni fursa kubwa ya kibiashara kwao," alisisitiza Mchwampaka.
Akizungumzia Mnada wa Madini ya Tanzanite uliofanyika tarehe 5 , Mei, alisema kuwa,  minada  hiyo  itaendelea kufanywa mara kwa mara kutokana na mchango wake katika sekta husika kwa kuwa pia inasaidia kupata bei halisi ya madini hayo.
Katika mnada wa Madini ya Tanzanite jumla ya kampuni 48 zilishiriki mnada huo ambapo madini ghafi ya  Tanzanite kutoka Kampuni ya TanzaniteOne  yenye jumla ya gramu 691,060.33 ziliuzwa katika mnada huo kwa dola za Marekani 3,161,860, sawa na asilimia 100 ya madini yote yaliyowasilishwa kwa mauzo.
Pia, alizungumzia ujumbe wa Serikali ya Nigeria iliyoshiriki Maonesho hayo na kueleza kuwa, ujumbe huo ulifika kwa lengo la kujifunza namna Tanzania inavyoongeza thamani madini yake ikiwemo pia kubadilisha uzoefu na kuongeza kuwa, lengo ni kuifanya Afrika inufaike na rasilimali zake za madini.
Ujumbe wa Serikali ya Nigeria uliongozwa na Waziri wa Madini  na  Maendeleo ya Viwanda, Abubakar Bwari aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Abbas Mohamed pamoja na ujumbe wa wafanyabiashara wa Madini kutoka nchini humo.

No comments: