Sunday, May 7, 2017

Rais wa Zanzibar Mh. Dk. Shein apokelewa na Rais wa Djbout Mhe.Ismail Omar Guelleh


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Rais wa Djbout Mhe.Ismail Omar Guelleh alipofika katika Ikulu ya Djbout leo akiwa katika ziara ya kiserikali na ujumbe wake,Picha na Ikulu.07/05/2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akifuatana na Rais wa Djbout Mhe.Ismail Omar Guelleh alipofika katika Ikulu ya Djbout leo akiwa katika ziara ya kiserikali na ujumbe wake,Picha na Ikulu.07/05/2017 

………………………………………………………………………. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Djibouti Ismail Omar Guelleh ambapo katika mazungumzo hayo viongozi hao wamekubaliana kuanzisha uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo hasa katika sekta za maendeleo na uchumi. 

Viongozi walifanya mazungumzo katika ukumbi wa Ikulu ya Djibouti ambapo Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa Rais Guelleh kwa mwaliko wake huo nchini mwake. 

Katika mazungumzo hayo viongozi hao kwa kauli moja walieleza haja ya kuanzisha uhusiano na ushirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo na uchumi kwa manufaa ya pande mbili hizo. 

Rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh kwa upande wake alimuhakikishia Dk. Shein kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta za mawasiliano, utalii, uwekezaji pamoja na usafiri na usafirishaji sambamba na utayari wa kujifunza mambo mbali mbali kutoka Zanzibar ikiwemo sekta ya utalii. 

Rais Guelleh, alieleza kuwa nchi yake inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania ambao una historia nzuri na kueleza kuwa Djibout iko tayari kujifunza mbinu zilizotumika na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii. 

Ambapo pia, kiongozi huyo alieleza utayari wa kushirikiana na Zanzibar kutokana na mafanikio waliyoyapata na njia sambamba na mikakati waliyoitumia katika kufikia mafanikio waliyoyapata na mikakati waliyoitumia kufikia mafanikio waliyonayo hasa katika suala zima la uimarishaji wa bandari, mawasiliano na vitega uchumi. 

Kiongozi huyo wa Djibouti alimkaribisha Dk. Shein pamoja na ujumbe wake nchini humo huku akisisitiza kuwa Tanzania na Djibouti zina ukaribu mkubwa na zimekuwa zikishirikiana katika kupambana na uharamia wa baharini kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Mamlaka ya Serikali ya Kimaendeleo (IGAD). 

Aidha, Rais Guelleh alitumia fursa hiyo kumueleza Dk. Shein mafanikio yaliyopatikana nchini mwake hasa kutokana na uimarishaji wa bandari, mawasiliano na kueleza azma ya nchi yake hivi sasa kujikita katika sekta ya utalii kutokana na baadhi ya vivutio vilivyopo ikiwemo Ziwa Assal ambalo chimbuko lake ni Bonde la Ufa pamoja na mambo mengineyo. 

Hivyo kiongozi huyo alimueleza Dk Shein kuwa pande hizo mbili zina mengi ya kujifunza kwa pamoja kwani kila upande umeweza kupata mafanikio yake. 

Kwa upande wake Rais Dk. Shein, alitumia fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa Rais Guelleh kwa mualiko wake huo aliompa pamoja na mapokezi makubwa aliyoyapata yeye na ujumbe aliofuatana nao na kueleza kuwa ziara hiyo itakuwa ndio kichocheo kikubwa cha mashirikiano kati ya Zanzibar na Djibouti. 

Dk. Shein alimueleza Rais Guelleh kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Djibouti hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo wa kiuchumi inategemea sekta ambazo Zanzibar nayo imeamua kwa makusudi kuziimarisha ili ziweze kuimarisha uchumi na kuleta tija. 

Alizitaja miongoni mwa sekta hizo ambazo Djibouti imepata mafanikio ni uendeshaji wa Bandari,mawasiliano na Maeneo Huru ya Kiuchumi ambayo yamekuwa ndio kichocheo kikubwa cha uchumi wa nchi hiyo. 

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa ziara hiyo ni kielelezo cha urafiki, heshima na udugu baina ya Serikali zote mbili pamoja na wananchi wake ambapo itasaidia sana kuimarisha uhusiano na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano. 

Katika maelezo yake, Dk. Shein alimueleza Rais Guelleh kuwa Zanzibar katika ziara hiyo ina hamu kubwa ya kufahamu maendeleo makubwa yaliyofikiwa na Djibouti tokea mwaka 1977 ilipopata uhuru wake kutoka kwa Koloni la Kifaransa. 

Dk. Shein alieleza kuwa ana hamu kubwa kuona maendeleo yaliofikiwa na nchi hiyo katika sekta muhimu za kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya bandari, kuendeleza maeneo Huru, mawasiliano, uvuvi, viwanda, usafiri na usafirishaji, afya, elimu na sekta zote muhimu za utoaji wa huduma kwa wananchi wa nchi hiyo. 

Alipongeza juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya nchi hiyo chini ya uongozi wa Rais Guelleh ambazo zimepelekea Djibouti kuwa ni mfano mzuri kwa nchi za Afrika ambazo zinatafuta maendeleo ya haraka, demokrasia pamoja na kuimarisha hali ya utulivu na usalama wa nchi. 

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumueleza Rais wa Djibouti mafanikio yaliopatikana kwa upande wa kisiasa na kimaendeleo na kupelekea kuimarika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni Muungano wa mfano kwa bara la Afrika na kutoa salamu za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa kiongozi huyo. 

Aidha, Dk. Shein alimuhakikishia Rais huyo utayari wa Zanzibar kushirikiana na Djibouti na kutoa uweledi wake katika sekta ya utalii kwa nchi hiyo kutokana na Zanzibar kupata mafanikio makubwa katika sekta ya Utalii. 

Pamoja na hayo, Dk. Sheuin alimuelkeza Rais huyi wa Djibout hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Bandari mpya ya Mpiga Duri, mradi ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uingizaji wa mizigo na makontena na kuipunguzia mzigo Bandari ya Malindi. 

Aidha, alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuifanya Zanzibar kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020, huku akitumia fursa hiyo kumualika kiongozi uyo wa Djibouti kutembelea Zanzibar kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa pande mbili hizo. 

Dk. Shein yupo nchini Djibouti kwa ziara ya siku tatu kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Ismail Omar Guelleh. 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

No comments: