Saturday, May 13, 2017

RC TABORA AONGOZA WAFANYAKAZI WA NBC KUPANDA BARABARA YA URAMBO

Na Tiganya Vincent-Tabora

Uongozi wa Mkoa wa Tabora umeamua kuendesha zoezi la kudumu la kuhamasisha jamii kuanzia ngazi za wanafunzi hadi jamii nzima juu ya zoezi upandaji miti ili kukabiliana na uharibifu mkubwa wa mazingira ulisababishwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu mkoani humo.

Hatua hiyo inalenga kuijengea jamii na wanafunzi katika shule na vyuo tabia ya utunzaji wa mazingira na upandaji miti kwa ajili ya faida yao na kizazi kijacho.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini Tabora na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri wakati akiongoza zoezi la upandaji wa miti zaidi ya 150 katika eneo la Malolo barabara ya zamani ya kutoka Tabora mjini kuelekea Urambo.

Alisema kuwa zoezi hili ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Ofisi ya Makamu wa Rais ambapo kwa kuanzia amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zaote kuhakikisha kila Wilaya inatekeleza agizo hilo kwa miti isiyopungua milioni moja na laki tano kila mwaka.

Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa miti waliyopanda watakikisha inahimili wakati wa kiangazi kwa kuimwagilia kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya umwagiaji kwa matone ya chupa.

Alizitaja baadhi ya sababu zilizosababisha kuwepo ya uharibifu huo mkubwa ni pamoja kilimo cha tumbaku, ulimaji katika vyanzo vya maji na ufugaji usio rafiki wa mazingirana.

Bw. Mwanri aliongeza kuwa hatua nyingine ambazo zimeanza kuchukuliwa katika kudhibiti uharibifu wa mazingira hasa maeneo ya mijini ni pamoja na kukamata mifugo yote inayozurura.

Aidha , aliwashukuru wanyakazi wa NBC tawi la Tabora kupanda miti hiyo na kuahidi kuitunza ili ije iwe ukumbusoa wao wa kufanyakazi katika Mkoa huo.

Bw. Mwanri alisema kuwa kitendo chao cha upandaji wa miti katika Mkoa huo sio tu kwamba watakuwa wanahifadhi mazingira bali watabakiza alama ambayo itakuwa ukumbusho kwao na kwa kizazi chao.

Kwa upande wa Meneja wa NBC wa Kanda (Tabora, Shinyanga, Kigoma na Mara) Daudi Edgar Mfalla alisema kuwa Benki hiyo imefurahishwa na juhudi za Uongozi wa Mkoa huo na kuamua kuunga mkono zoezi linaloendelea kwa sababu ya kutambua bila mazingira mazuri hakuna uhai.

Alisema kuwa upandaji wa miti hiyo ni sehemu ya utaratibu wa Benki hiyo wa kurudisha inachokipata katika jamii. Bw.Mfalla alisema kuwa zoezi linaloendwa na uongozi wa Mkoa wa Tabora ni zuri na litasaidia kuijenga jamii hasa kuanzia watoto hadi wazee kuwa na mazoea ya upandaji miti na utunzaji wa mazingira kwa ya faida yao , jamii, Taifa na dunia kwa ujumla.

Mmoja wa wafanyakazi wa Benki hiyo mkoani Tabora Bibi Grace Mwanri alitoa wito wa kujenga tabia ya kupanda miti na kuitunza kwani inahusika sana na uhai na maisha ya kila ya mwanadamu.

Alisema kuwa jamii kama itakata miti ovyo bila kupanda mingine kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo vyanzo itasababisha ukame na hivyo hakutakuwepo na maji na uhai utakuwa shakani.

Bibi Mwanri alisema kuwa wao kama wafanyakazi na wakazi wa Tabora wanalitambu hilo na ndio maana wameungana na viongozi na wadau wote ambao wamekwishapanda miti kushiriki zoezi hilo. Mkoa wa Tabora kabla ya uharibifu wa mazingira ulikuwa ukipata mvua za wastani wa milimita 1800 lakini kutokana na uharibifu huo hivi unapata wastani wa milimita 650. 

No comments: