Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema iwapo Mpango wa Huduma ya Afya ngazi ya
Jamii utatumika vizuri utasaidia kuokoa Afya na maisha ya wananchi wengi Mkoani humo.
Mtaka ameyasema hayo katika kikao kilicho wahusisha Viongozi ngazi ya Mkoa,Wilaya, watendaji wa
Kata, Mitaa na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya Bariadi, Itilima na Mji wa Bariadi, ambacho kililenga
kutoa elimu kuhusu utekelezaji wa mpango wa huduma ya Afya ngazi ya Jamii mkoani humo.
Mtaka amesema mwamko wa kupata huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa
wananchi katika maeneo mengi mkoani humo uko chini, hivyo mpango huu wa kutoa huduma ngazi ya
kaya utasaidia kuhamasisha wananchi kutafuta huduma za afya katika vituo hivyo badala ya kutegemea
tiba za kienyeji.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani humo.
“Tukitumia huduma hii ya Afya Majumbani vizuri itasaidia sana, tukifika mahali ambapo jamii yetu
itapata mwamko wa kupata matibabu katika vituo stahiki vya afya tutakua tumeokoa jamii yetu, kwa
sababu bado wapo wanaoamini kupata matibabu katika tiba za kienyeji; tungehitaji wananchi wetu
huduma ya kwanza kwenye afya iwe vituo vyetu kutolea huduma za afya na siyo tiba mbadala” amesema
Mtaka.
“........kwa sisi ambao tunatengeneza Mkoa wetu katika Uchumi, Uchumi ni Afya wananchi hawawezi
kufanya kazi wakajenga uchumi kama hawatakuwa na afya njema” alisisitiza.
Aidha, Mtaka amewataka Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji kufanya utambulisho wa kutosha wa
wahudumu wa afya ya Msingi ngazi ya jamii watakaokuwa wakitoa huduma kwa wananchi katika
maeneo yao ili wataalam hao wasije wakapata madhara yoyote wakati wakitekeleza majukumu yao.
Dkt.Ama Kasangala kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, akizungumza na Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani Simiyu.
Mkuu huyo wa Mkoa pia amewataka wananchi kuachana na taratibu za kimila zinazoathiri utendaji wa
watumishi wa Umma ikiwemo kutumia mahakama za kimila (dagashida) na akawataka viongozi hao
kuwasaidia wananchi kubadilika ili wahudumu wa afya ngazi ya Jamii watakaopelekwa katika maeneo
yote ya mkoa huo watekeleze majukumu yao bila vikwazo vyovyote.
Wakati huo huo Mtaka ameomba Shirika lisilo la Kiserikali la AMREF lisaidie katika kuajiri wahudumu
wa afya ngazi ya jamii walipewa mafunzo, ili wasaidie kutoa huduma na kupunguza changamoto ya
upungufu wa watoa huduma wakati Serikali ikiendelea kushughulikia suala hilo.
Baadhi ya Watendaji Kata, Mitaa na Vijiji kutoka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani humo.
Vile vile ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa afya ikiwemo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto kushughulikia suala la upatikanaji wa vifaa ili watoa huduma ngazi ya jamii
watakapowafikia wananchi waweze kutoa huduma stahiki kwa wakati.
Kwa upande wake Afisa wa Mpango wa Huduma ya Afya ngazi ya Jamii kutoka Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt.Ama Kasangala amesema Wizara imetengeneza
miongozo ya kuwafundisha wahudumu hao wanapokuwa kazini ili waimarike na kutoa huduma nzuri.
Naye Kaimu Mratibu wa Mpango wa Huduma ya Afya Ngazi ya Jamii, Dkt. Bahame Ntelemko amesema
mpango umelenga kuwatumia wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kusaidia kuboresha huduma za afya
hususani katika huduma za mama wajawazito na uzazi kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(kushoto) na Dkt.Ama Kasangala kutoka Wizara ya Afya wakizungumza jambo katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani humo.
Dkt. Ntelemko amesema kwa mwaka 2016 wanawake takribani 45 walipoteza maisha kutokana na
masuala ya uzazi ambapo vifo vingi vinatokana na ukosefu wa elimu ikiwemo kutojua umuhimu wa
kuwahi katika vituo vya kutolea huduma, ambapo amesema uwepo wa huduma katika kaya utasaidia
kupunguza idadi ya vifo hivyo.
Mafunzo yanayofanywa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa
kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la AMREF, kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Huduma za
Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoa wa Simiyu, yameshawafikia Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji zaidi
ya 350.
Baadhi ya Watendaji Kata, Mitaa na Vijiji kutoka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima wakimsikiliza
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika
Mjini Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani humo.
Baadhi ya Watendaji Kata, Mitaa na Vijiji kutoka kwa Halmashauri ya Mji Bariadi wakimsikiliza Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka katika kikao cha kutoa elimu kwa viongozi hao kilichofanyika Mjini
Bariadi kuhusu utekelezaji Mpango wa Huduma za Afya ya Jamii ngazi ya Jamii Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(wa tano kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi
ya Watendaji Kata, Mitaa na Vijiji kutoka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(wa tano kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi
ya Viongozi wa Mkoa, Wizara ya Afya na Watendaji Kata, Mitaa na Vijiji kutoka kwa Halmashauri ya Wilaya ya
Itilima.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka(wa tano kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi
ya Viongozi wa Mkoa, Wizara ya Afya na Watendaji Kata, Mitaa na Vijiji kutoka kwa Halmashauri ya Mji wa
Bariadi.
No comments:
Post a Comment