Tuesday, May 23, 2017

RAS TABORA AAGIZA JENGO LA UPASUAJI LA ZAHANATI YA ILOLANGURU WILAYANI UYUI KUKARABATIWA UPYA .

Na Tiganya Vincent-RS-Tabora

Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora kuhakikisha wanakarabati upya Jengo la utoaji wa huduma ya Upasuaji katika Zahanati ya Ilolanguru lilojengwa chini ya kiwango na Mradi wa Mbola Melenia.Hatua hiyo inalenga kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kwa mgongwa wakati anapata huduma ya upasuaji kutoka madaktari.

Dkt. Ntara ametoa agizo hilo jana Wilayani Uyui wakati alipokwenda kukagua vifaa vya kisasa vya upasuaji ambavyo vipo katika Zahanati hiyo toka mwaka 2013 lakini havijaanza kutumika kwa sababu mbalimbali ikiwemo ubovu wa jengo lililojengwa na Mradi wa Mbola na ambalo halina ubora kwa mujibu wa Madaktari.

Alisema kuwa wajenzi wa jengo hilo waliamua kujenga hata bila kuwashirikisha Wataalamu wa Afya na Wahandisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wala Mkurugenzi wa Wilaya ya Tabora na hivyo majengo yao mengi kuwa mabovu na ambayo yana nyufa kabla hayajaanza kutumika.

Dkt. Ntara aliongeza kuwa haiwezekani kwa muda mfupi baada ya kujengwa jengo liwe limeshapasuka na madirisha kuruhusu vumbi kuingia katika Chumba cha upasuaji , jambo ambalo ni hatari kwa mgongwa kupata maambukizi mengine.

Kufuatia udhaifu wa jengo hilo Katibu Tawala huyo wa Mkoa amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kulifanyia maboresho na ukarabati katika sehemu zenye mapungufu ili lianze kutumika wakati taratibu nyingine za kisheria dhidi ya mjezni zikiendelea kufuatiliwa.

“Siwezi kukabali kuwa ujenzi wa jengo hilo umegharimu milioni 90 ,wakati lina mapungufu mengi.… hakuna maru maru wala madirisha ya aluminia, sakafu imeshaanza kupasuka wakati jengo halijaanza kutumia ni vema kitu kinachojengwa kikalingana thamani ya fedha halisi” alisema Katibu Tawala Mkoa.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Tabora Hadija Makuwani alitoa ufafanuzi kwa Katibu Tawala Mkoa alisema kuwa alishindwa kulipokea jengo hilo baada ya kugundua kuwa limejengwa chini ya kiwango na wakati wa ujenzi ukiendelea hakuna mtaalamu wake hata mmoja alishirikishwa ili kuhakikisha linakuwa imara na bora kwa matumizi ya Zahanati hiyo.

Alisema kuwa alipokuwa akimwita Meneja Mradi huo wa Mbola Melenia Dkt. Greyson Nyadzi kuja mara nyingi amekuwa akipiga chenga na kumtuma mwakilishi,jambo linaloonyesha kuwa hata yeye anatambua kuwa mradi huo uko chini kiwango.

Mkurugenzi huyo Mtendaji aliongeza kuwa viongozi wa mradi huo wameshindwa hata kukabidhi vyombo vya usafiri kama vile pikipiki 25, magari madogo na gari kubwa la kubebea mchanga na kuvitumia kwa matumizi binafsi bali ya kuvitoa ili visaidie watendaji wa Halmashauri yake kutoa huduma kwa wananchi.

Akijibu hoja hiyo Katibu Tawala huyo Mkoa amemwagiza Mkurugenzi Mtandaji wa Wilaya ya Tabora kuwaambia viongozi wa Mbola kurejesha mara moja vyombo vyote vya usafiri ili kuwasaidia Watendaji wa Halmashauri kuwahudumia wananchi.“Haiwezekani watu wachache wang’ang’anie magari ya umma wakati nyie hamna magari ya kutosha …nakuagiza DED mwambie huyo Meneja wa Mbola arudishe magari yote na pikipiki”alisisitiza Dkt. Ntara.

Aidha ,Katibu Tawala Mkoa wa Tabora ameunda timu ya Wataalam kutoka Mkoani na Katika Halmashauri ya Wilaya ya Tabora kwa ajili kukagua ubora wa majengo yote , vifaa vya upasuaji alivyoweka katika jingo la upasuaji ili kuandaa taarifa kwa ajili ya kupeleka mbele kwa hatua zaidi.

Alisema kuwa hadi kufikia Ijumaa ya wiki hii taarifa iwe tayari kwa kuwa wananchi wanahitaji sana huduma ya upasuaji kwa karibu kuliko hivi sasa wanapata tatizo na ukimbili katika Hospitali ya Rufaa Kitete.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Gunini Kamba alisema kuwa jengo linabidi baadhi ya sehemu zivunje ili kupanua mlango wa kuingizia na kumtoa mgonjwa katika chumba cha upasuaji kuliko ilivyo sasa ambao mlango uliojengwa ni mdogo sana haurusu Kitanda cha mgonjwa kupita.

Aliongeza kuwa ni vema dirisha yakawekwa vizuri na yawe ya aluminia na sio yaliopo sasa ambayo yanaruhusu vumbi kuingia katika chumba cha upasuaji na hivyo kuweza kumsababishia maambukizi mapya mgonjwa wakati madakitari wakiendelea na zoezi la upasuaji.

Dkt. Kamba aliueleza Uongozi wa Halmashauri hiyo kufanyia maboresho ya mapungufu hayo ili kiweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa eneo hilo.

No comments: