Wednesday, May 24, 2017

MKURUGENZI MKUU TIC GEOFFREY MWAMBE AWATAHADHARISHA WAWEKEZAJI WENYE NIA MBAYA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) Geoffrey Idelphonce Mwambe ametoa tahadhari kwa wawekezaji wote wa nje na ndani ambao hawana nia njema na maendeleo ya taifa kuwa hawana nafasi nchini na kwamba hawatapata fursa yoyote Tanzania.

Mwambe ametoa tahadhari hiyo jana jioni katika kikao kifupi kilichoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi kwa ajili ya kumuaga rasmi Mkurugenzi huyo mara baada ya uteuzi wake ambapo hapo awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni.

Amesema kituo cha uwekezaji kitashirikiana na wawekezaji wenye nia njema tu ila wale ambao wanataka kujinuafiasha wao na kuliacha taifa bila faida yoyote hawatapewa fursa yoyote ya kuwekeza nchini.

Mwambe ameongeza kuwa atahakikisha kuwa wawekezaji wenye ubora na ambao uwekezaji wao unamgusa mtanzania moja kwa moja wanapatikana hasa wale ambao watasaidia kutoa ajira kwa wananchi na kukuza uchumi.

“Nina imani na wawekezaji wadogo ambao nitajitahidi kuwaunganisha na wawekezaji wakubwa ili wakue na wajenge uchumi wa taifa itawasaidia pia hao wawekezaji wadogo watapata uzoefu na hivyo kuwa wawekezaji wakubwa”, amesema.

Mwambe ameongeza kuwa hatausahau Mkoa wa Singida kwenye fursa za uwekezaji na kuongeza kuwa mkoa wa Singida una fursa nyingi hasa vitunguu ambavyo vimekuwa vikisafirisha nje ya nchi na kufungashwa kwa jina la nchi hiyo ya jirani.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi amempongeza Mkurugenzi Mwambe kwa kuendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Raisi kutokana na uchapakazi na uadilifu wake.

Dokta Nchimbi amesema Mkoa wa Singida umekuwa ukizalisha bidhaa nzuri na zenye ubora pamoja na kuzalisha watendaji waadilifu na wachapakazi na hivyo uteuzi wake utaendelea kuwapa hamasa vijana na watumsihi wengine waendelee kuwa waadilifu.

Ameongeza kwa Singida ina fursa za kutosha kuleta maendeleo ya Mkoa huu pamoja na taifa kwa ujumla pia unajivunia fursa hizo ambazo baadhi yake ni kilimo cha alizeti, vitunguu na asali bora.

Dokta Nchimbi amemuasa Mkurugenzi Mwambe kuiwakilisha Singida katika majukumu yake na pia kutumia uchapakazi wake katika kuboresha mazingira ya uwekezaji ili yawavutie wawekezaji wa nje na ndani ili kufikia lengo la tanzania ya Viwanda.

Aidha amemkaribisha tena Singida na kumuahidi kuwa Mkoa uko tayari kwa ajili ya uwekezaji wowote wenye tija kwa wananchi na pia Singida iwe sehemu ya viwanda na kuipa nafasi Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.
 Mkurugenzi wa TIC Geoffrey Mwambe (wa kwanza kushoto) akipokea zawadi ya saa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (wa kwanza Kulia) katika kikao cha kumuaga, Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo na Mkuu wa Wilaya Mkalama JacksoN Masaka.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini Geoffrey Mwambe akiwashukuru viongozi wa Mkoa wa Singida kwa ushirikiano katika kikao kifupi cha kumuaga.
 Mkurugenzi wa TIC Geoffrey Mwambe (wa kwanza kushoto) akipokea zawadi ya saa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (wa kwanza Kulia) katika kikao cha kumuaga, Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo na Mkuu wa Wilaya Mkalama JacksoN Masaka.
  Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi na Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo wakifungua zawadi ya saa ambayo ina picha ya mazao ya alizeti na vitunguu ambavyo huzalishwa kwa wingi na ubora Mkoani Singida.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo akimpongeza Mkurugenzi Mpya wa TIC kwa uteuzi bw. Geoffrey Mwambe ambaye alikua Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, kulia kwake ni mkurugenzi Mwambe na kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Injinia Jackson Masaka.

No comments: