Monday, May 29, 2017

MEJA JENERALI (MSTAAFU) KIJUU: CHANGAMKIENI MIKOPO YA BENKI YA KILIMO

Na Mwandishi wetu, Bukoba
Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu amewaasa wakulima na wafugaji wa mkoa wa Kagera kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kujikwamua katika shughuli zao za kilimo mkoani humo.
Meja Jenerali (Mstaafu) Kijuu alitoa wito huo alipotembelea Banda la TADB wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa inayofanyika kitaifa mkoani Kagera.
Mkuu wa mkoa huyo alisema kwa kuzingatia malengo ya uanzishwaji wa Benki ya Kilimo unalenga kutimiza dhamira ya Serikali ya kuwasaidia wakulima nchini kote kukabiliana na mapungufu kwenye kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo.
“Nawaomba wakulima na wafugaji wa Kagera kuchangamkia mikopo nafuu ya Benki yetu ya Kilimo ili muongeze tija katika kilimo chenu maana Benki ipo kwa ajili ya kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na kuchagiza mapinduzi katika  kilimo nchini,” Meja Jenerali (Mstaafu) Kijuu alisihi.
Kwa mujibu wa TADB, sekta za kilimo na mifugo ni sekta za kipaumbele ambazo zinazopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao na mifugo hasa katika uongezaji wa thamani wa sekta hizo nchini.
Benki hiyo inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2 hadi Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka Kumi na Mitano (15)).
TADB ni taasisi ya serikali ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kutatua ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini ambao ulikuwa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa; riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo; mikopo ya muda mfupi; masharti magumu ya kukopa bila kuzingatia hali halisi ya sekta ya kilimo  na mazao ambayo inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
 Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu (aliyevaa Kaunda suti) akiwasili katika Viwanja vya Kyaikarabwa kutembelea na kukagua shughuli zinazoendelea wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa inayofanyika kitaifa mkoani Kagera.
 Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu akikaribishwa katika Banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Afisa Mahusiano na Masoko Mkuu wa TABD, Bw. Saidi Mkabakuli.
 Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu (aliyeshika kipaza sauti kulia) akizungumza wakati alipotembelea Banda la TADB. Anayemsikiliza kushoto ni Afisa Mahusiano na Masoko Mkuu wa TABD, Bw. Saidi Mkabakuli.
 Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu akimsikiliza Afisa Mahusiano na Masoko Mkuu wa TABD, Bw. Saidi Mkabakuli wakati alipotembelea Banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwenye Viwanja vya Kyaikarabwa yanapofanyika Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa mkoani Kagera.
Afisa Mahusiano na Masoko Mkuu wa TABD, Bw. Saidi Mkabakuli akisisitiza jambo wakati Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu (hayupo pichani) alipotembelea Banda la TADB.
 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bukoba, Bibi Mwantum Dau (kulia) akifurahia jambo na  na Afisa Mahusiano na Masoko Mkuu wa TABD, Bw. Saidi Mkabakuli wakati wakimsubiri Mkuu wa mkoa wa Kagera.

No comments: