Thursday, May 18, 2017

IKUNGI WAANZISHA MFUKO WA ELIMU ILI KUONDOA CHANGAMOTO KATIKA SEKTA HIYO.

Mkuu wa Wilaya Ikungi Miraji Mtaturu katikati akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya mfuko wa elimu wilaya ns viongozi wa halmashauri baada ya kumaliza kikao nao. 
Mjumbe mwakilishi wa madhehebu ya dini sheikh Salum Ngaa akichangia hoja wakati wa kikao kilichoongozwa na mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu pichani wakiwa na wajumbe wa kamati ya mfuko wa elimu wilaya. 
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi Haika Massawe akichangia hoja wakati wa kikao cha wajumbe wa kamati ya mfuko wa elimu wilaya. 
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akitoa maelekezo wakati alipokutana na kamati ya mfuko wa elimu ya wilaya. 

…………………………….. 

MKUU wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu amekutana na kamati ya mfuko wa elimu wilaya na kuwaomba kuwa wazalendo katika kutafuta njia za kutatua changamoto za elimu wilayani humo. 

Mfuko huo umeundwa baada ya uanzishwaji wake kuridhiwa na kikao cha baraza la madiwani kilichoketi hivi karibuni. 

Akizungumza katika kikao cha kuwapatia majukumu yao Mtaturu amesema mfuko huo utakuwa na jukumu la kuratibu masuala yote yatakayosaidia kuboresha utoaji wa elimu katika shule za msingi na sekondari. 

“nawapongezeni kwa heshima mliyopewa ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa kamati hii,naimani kuwa mtafanya kazi kwa uzalendo mkubwa ili matunda ya uwepo wenu yaonekane kwa kuitoa elimu yetu hapa ilipo na kuipeleka mbali zaidi,”alisema Mtaturu. 

Alisema wakifanikiwa kuondoa changamoto zilizopo watakuwa wameboresha mazingira ya utoaji elimu na kuongeza ufaulu wa watoto jambo ambalo waliazimia walipokutana wadau wa elimu. 

Akitoa taarifa kwenye kikao hicho katibu wa mfuko huo Salum Athuman alisema ili kutatua changamoto za elimu zilizopo katika wilaya hiyo zinahitajika jumla ya shilingi bilioni 26 kwa ajili ya miundombinu ya elimu ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa,nyumba za walimu,maabara,matundu ya vyoo na mabweni. 

Aidha mwenyekiti wa kamati hiyo Hamis Maulid kwa niaba ya wajumbe alisema wamepokea kazi hiyo na wataifanya kwa uadilifu mkubwa ili malengo yaliyokusudiwa yatimie. 

Disemba mwaka jana mkuu wa wilaya huyo alikutana na wadau wa elimu ili kubaini changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ambapo waliweka maazimio yapatayo 37 yenyek ulenga kuboresha elimu wilayani humo na moja ya mkakati waliouweka ndio umezaa wazo la kuanzishwa kwa mfuko huo wenye wajumbe 15 ambao wameanza kazi rasmi ili kutafuta njia ya kutatua changamoto za elimu wilayani humo. 

Wilaya hiyo ina jumla ya shule za sekondari 30 ikiwemo za kidato cha sita 3 na shule za msingi 108.

No comments: