Thursday, May 18, 2017

Ben Paul Ndani Ya Miss Ustawi Ijumaa

Mwanamuziki nyota wa kizazi kipya nchini, Ben Paul atatumbuiza katika mashindano ya kumsaka mrembo wa Chuo cha Ustawi wa Jamii (Miss Ustawi) yaliyopangwa kufanyika Ijumaa (Mei 19) kwenye ukumbi wa King Solomon uliopo Namanga jijini.

Mratibu wa mashindano hayo, Catherine Boniface alisema kuwa Paul ambaye anatamba na wimbo wa Moyo Machine, Phone na nyinginezo nyingi, pia atatambulisha wimbo wake mpya aliomshirikisha mwanamuziki nyota nchini, Darasa.

Mashindano hayo yamedhaminiwa na kinywaji cha Windhoek, yatashirikisha jumla ya warembo 12 ambao walikaa kambini kwa muda wa wiki mbili wakijifua chini ya mwalimu wao, Clara Michael na matron, Catherine Boniface.

Warembo ambao wamepitishwa na kamati ya mashindano hayo ni Fatma Kivea, Elice Mwakajila, Melody Thomas, Diana Mwaibula, Hapifania Shedoekulu, Careen Kileo. Wengine ni Angelina Michael, Ruth Deogratius, Consolator Samwel, Loyce Jeck na Elizabeth Julius.

Washindi watatu wa mashindano hayo watapata nafasi ya kushindana katika shindano la warembo wa elimu ya juu (Miss Higher Learning Institution) ambapo warembo watatu wa kwanza watafuzu katika mashindano ya Miss Tanzania mwaka huu.

Mratibu wa mashindano hayo, Catherine Boniface alisema kuwa warembo watapanda jukwaani wakiwa wanashindania vazi la ubunifu, ufukweni na usiku na warembo watano watakaopita katika mchujo wa kwanza watajibu maswali.

“Morali ya warembo ipo juu, kila mmoja ni mshindi, lengo letu ni kushinda taji la vyuo vya elimu ya juu na kutwaa taji la Miss Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano ya urembo nchini,” alisema Catherine.

Msemaji wa kampuni ya Mabibo Beer inayodhamini shindano hilo, Andrea Missama amesema kuwa wameamua kudhamini shindano hilo kama sehemu ya kampuni yao kukuza vipaji na kazi za jamii.

Missama amesema kuwa warembo wengi wamejitokeza kushindania taji hilo ambalo mshindi wake atakiwakilisha chuo hicho katika mashindano ya urembo ya vyuo vya elimu ya juu.

Rais wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Yohana Mabena akizungumza wakati wa  kuwatambulisha warembo wao kwa wadhamini wakuu, kampuni ya Mabibo Beer. Kulia ni msemaji wa kampuni ya Mabibo Beer, Andrea Missama na kushoto kwa Mabena ni Waziri wa Michezo wa Ustawi, Ashura Jingu. Nyuma ni warembo wa miss Ustawi 2017. 
Mwanamuziki wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ben Paul akizungumza akizungumza wakati wa kutambulishwa kuwa msanii wa kutumbuiza katika mashindano Miss Ustawi 2017 yaliyopangwa kufanyika Ijumaa (Mei 19) kwenye ukumbi wa King Solomon uliopo Namanga, jijini.

Miss Ustawi anayemaliza muda wake Evelyn Andrew akizungumza wakati wa utambulisho wa warembo hao kwa wadhamini wakuu. Evelyn anavua taji hilo, Ijumaa (Mei 19) wakati wa mashindano ya kumsaka mrembo wa chuo hicho kwenye ukumbi wa King Solomon uliopo Namanga.


Warembo wakiwa katika picha ya pamoja na Miss Ustawi anayemaliza muda wake, Evelyn Andrew. Warembo hao watapambana Ijumaa (Mei 19) wakati wa mashindano ya kumsaka mrembo wa chuo hicho kwenye ukumbi wa King Solomon uliopo Namanga. 

No comments: