Saturday, May 13, 2017

BENKI YA NMB YAIKABIDHI SERIKALI GAWIWO LA SHILINGI BILIONI 1.7



Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Tanzania Bw. Edward Marks, akizungumza jambo wakati wa maadhimisho ya Benki yake kutimiza miaka 50, tukio lililofanyika Mjini Dodoma Jana usiku.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NBC, Bw. Nehemiah Mchechu, akitaja mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Benki hiyo, wakati wa uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya Benki hiyo kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, tukio lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Morena, Mjini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Josephat Kandege, akipokea tuzo kwaniaba ya wabunge, tuzo iliyotolewa na NBC kutambua mchango wa Bunge katika kuanzishwa kwa Benki hiyo miaka 50 iliyopita.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akionyesha alama ya dole! akifurahia gawiwo la shilingi bilioni 1.7 zilizotolewa na NBC kwa Serikali, ambayo inamiliki asilimia 30 za hisa katika Benki hiyo
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akishukuru baada ya kupokea gawiwo la shilingi bilioni 1.7 zilizotolewa na NBC kwa Serikali, ambayo inamiliki asilimia 30 za hisa katika Benki hiyo

Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee Samwel Malecela, akitoa neon la shukurani kwenye hafla ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, sherehe zilizofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Morena mjini Dodoma.(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)







Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa mara ya kwanza imetoa gawiwo la shilingi bilioni 1.7 kwa Serikali ambayo inamiliki asilimia 30 ya hisa za Benki hiyo.

Hundi kifani ya kiasi hicho cha fedha alikabidhiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), kwaniaba ya Waziri Mkuu, katika tukio la Benki hiyo kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, tukio lililofanyika katika Hoteli ya Morena Mjini Dodoma.

Hii ni Mara ya kwanza kwa Benki hiyo kutoa gawiwo kwa wanahisa wake katika kipindi cha miaka 9 baada ya kuanza kupata faida ya uwekezaji wake hapa nchini.

Dkt. Mpango aliishukuru Benki hiyo kwa kuanza kutoa gawiwo kwa wanahisa wake baada ya ukame wa muda mrefu na kuelezea matumaini yake kwamba kiasi cha gawiwo kitaongezeka zaidi miaka ijayo.

Hata hivyo alizitaka Benki zote hapa nchini kupunguza riba za mikopo inazotoza kwa wateja wao hasa baada ya Benki Kuu ya Tanzania-BOT kupunguza riba za mikopo kwa mabenki kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12.

Alizitaka pia taasisi za fedha nchini, kuwekeza fedha katika kutekeleza Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo kwa njia ya mikopo kwa wateja wao kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vitakavyosisimua uchumi na kukuza ajira nchini.

Alipongeza pia juhudi zilizofanywa na Benki hiyo kufanya uwekezaji mkubwa kwenye mtandao wa malipo ya kielektroniki ikiwa ni maagizo ya Serikali kwamba malipo yote ya Serikaloi yafanyike benki au kupitia miamala ya kielektroniki

“Nimefurahi kuthibitishiwa kwamba, kutoka tarehe 1 Julai 2016 hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2017, NBC imekusanya fedha za Serikali na kuzituma kielektroniki katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jumla ya Shillingi Billioni 991” aliongeza Dkt. Mpango.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Nehemiah Mchechu, alieleza Mkakati wa Benki hiyo ya tatu kwa ukubwa hapa nchini ikitanguliwa na Benki za NMB na CRDB, huku ikiwa imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 1, kwamba imejipanga kusogeza huduma zake kwa wananchi na wafanyabiashara wa kati na wa chini kabisa.

“Mwaka jana Benki yetu imepata faida ya zaidi ya shilingi bilioni 13 na katika mkutano Mkuu wa wanahisa tuemekubaliana kutoa gawiwo kwa wawekezaji” aliongeza Bw. Mchechu.

NBC inamilikiwa na wabia watatu, wakiwemo kundi la Mabenki ya Barclays (ABSA Group ltd) ya Afrika Kusini, inayomiliki hisa nyingi zaidi, Serikali ya Tanzania yenye hisa asilimia 30 huku Benki ya Dunia kupitia Taasisi yake ya Fedha ijulikanayo kama The International Finance Corporation (IFC), ikiwa na hisa asilimia 15.

No comments: