Tuesday, May 9, 2017

Balozi Seif akutana na Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar

Na Othman Khamis Ame, OMPR
Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa  Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi imekutana Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kutathmini Mvua za Masika na muelekeo wa kukabiliana na changamoto zilizoanza kuibuka.
Tathmini hiyo imekuja kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika Maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba na kuathiri Nyumba 325 Mkoa Kusinin Pemba, Nyumba 667 kuhamwa  ndani ya Mkoa Mjini Magharibi pamoja na kubomoka kwa miundombinu ya Bara bara na baadhi ya Madaraja hasa Kisiwani Pemba. 
Akitoa Taarifa za awali za athari ya mvua zilizojitokeza kwa mwaka wa 2017 tokea kuanza kwa msimu wa Mvua za  Masika, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad alisema athari ya Mvua hizo zimesababisha maporomoko ya ardhi yaliyosababisha kufukia  kwa baadhi ya Nyumba na Bara bara.
Nd. Ali alisema ziara za Viongozi wa Serikali zimegundua athari kubwa ya uharibifu wa miundombinu ya Bara bara na nyumba kutokana na mvua hizo hasa katika Mkoa wa Kusini Pemba na kusababisha kifo cha Mtoto Mmoja Ramadhan Mohamed baada ya kuangukiwa na ukuta wa Madrasa Chanjani Chake Chake Pemba.
Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar Nd. Mohamed Khamis Ngwali  alisema bado Visiwa vya Unguja na Pemba viko katika msimu wa mvua hali ambayo wananchi wanapaswa kufuatilia Taarifa zainazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Nd.Ngwali  alisema viwango vya mvua katika visiwa vya Zanzibar  viongezeka kama vilivyotangazwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania mnamo Tarehe 28 Mwezi uliopita na kuanza kunyesha mara moja siku iliyofuata.
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Kinga Wizara ya Afya  Dr.Fadhil Abdulla  alieleza kwamba Wizara ya Afya tayari imeshajiandaa na changamoto yoyote inayoweza kujitokeza endapo kutaibuka kwa maradhi ya mripuko katika kipindi hichi cha msimu wa mvua za masika.
Dr. Fadhil  alisema udhibiti wa vyakula vinavyouzwa katika maeneo ya wazi bado mgumu na ndio uliochangia kuibuka kwa maradhi ya Kipindupindu mwaka jana kwa asilimia 16%.
Alisema katika kukabidhiana na udhibiti wa mfumko wa maradhi ya kuambukiza Wataalamu wa Afya tayari wameshapima wagonjwa  22 walioonyesha ishara ya kusumbuliwa na maradhi ya matumbo ya kuharisha.
Akiahirisha  Kikao hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ipo haja ya kuandaliwa mikakati ya muda mrefu ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kila mwaka wakati wa msimu wa mvua za Masika.

No comments: