Saturday, April 29, 2017

WAZIRI MUHONGO AWATAKA WATAALAM KULISAIDIA TAIFA

Na Veronica Simba – Dodoma

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametoa wito kwa wataalam nchini, hususan walioko katika sekta za mafuta na gesi kulisaidia Taifa kuepukana na mikataba mibovu kwa kutumia utaalam wao badala ya wao kuendelea kulalamika kama wananchi wa kawaida.

Profesa Muhongo alitoa wito huo jana, Aprili 27, 2017 wakati akizindua Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA) katika hafla iliyofanyika makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.

Akizungumza na wajumbe wa Bodi hiyo, Profesa Muhongo alisema kwamba, kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wananchi kuhusu Taifa kuibiwa rasilimali mbalimbali na makampuni ya kigeni kutokana na mikataba mibovu iliyoingiwa awali.

“Ni kwa sababu hiyo, uteuzi wa wajumbe wa Bodi hii ya PURA, umezingatia sifa za hali ya juu za kitaaluma mlizonazo, ili pamoja na mambo mengine muweze kulisaidia Taifa kunufaika ipasavyo na rasilimali hizi adhimu za mafuta na gesi, kwa kuhakikisha mikataba inayoingiwa, inakuwa yenye manufaa kwetu.”

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Bodi ya PURA ina wajumbe watano ambao wamebobea katika taaluma za sheria, fedha, uhasibu na mazingira; sifa ambazo zinaifanya Bodi hiyo kuwa miongoni mwa Bodi bora kabisa hapa nchini.

Aliwataka wataalam hao kuachana na kasumba ya kulalamika kuwa Taifa linaibiwa badala yake watumie utaalam na ubobezi wao kuhakikisha changamoto hiyo inabaki kuwa historia nchini hususan katika sekta wanayoisimamia.

Sambamba na rai hiyo kwa wajumbe wa Bodi ya PURA, aliwataka wataalam wengine mbalimbali nchini, kujitokeza na kulisaidia Taifa katika sekta mbalimbali walizopo.

“Watanzania wajue kuwa, hivi vilio tunavyotoa, haimaanishi kwamba hatuna wataalam hapa nchini, Wataalam wapo. Sasa wataalam wajitokeze, siyo na wao wabaki kulalamika tu kama wananchi wa kawaida wasio na utaalam. Haitatusaidia,” alisisitiza Waziri.

Aidha, akizungumzia majukumu ya Bodi hiyo, Profesa Muhongo alisema kwamba, Bodi inawajibika kuishauri Wizara katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na masuala ya lesni, utafutaji wa rasilimali, kuhusu mikataba, mambo ya kodi na tozo mbalimbali na mengine ya aina hiyo.

“Kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) hapo awali. Hivyo, kama kulikuwa na mapungufu, nyie myarekebishe. Tunategemea mtoe majibu ya kitaalam kwa kilio cha watanzania.”

Vilevile, Waziri Muhongo aliitaka Bodi hiyo kuhakikisha inasimamia ushiriki wenye tija wa watanzania katika miradi mbalimbali ya sekta husika. Alieleza kuwa, mmoja wa wajumbe wa Bodi hiyo aliteuliwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, sehemu inayosimamia uwezeshaji, ili aweze kutekeleza jukumu hilo ipasavyo.

Waziri Muhongo pia aliwataka wajumbe wa Bodi hiyo kufanya kazi kwa uadilifu pasipo kuegemea upande wowote. Aliwataka kuepukana na vishawishi vya rushwa kutoka kwa Kampuni kubwa za Mafuta na Gesi na badala yake watangulize maslahi ya Taifa.

“Msinunuliwe na makampuni husika. Siyo kwamba nawazuia msionane nao, hapana. Suala ni mnaonanaje! Wekeni mipaka. Lazima ujue mipaka yako. Siyo unaenda huko unalishwa vitu unakuja unaipigania kampuni husika kama vile wewe siyo mjumbe wa Bodi. Hilo hatutakubali,” alisisitiza Waziri.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Bodi Dk. Adelardus Kilangi alimhakikishia Waziri Muhongo kuwa, watatekeleza majukumu yao kwa uaminifu na weledi ili kuleta manufaa kwa Taifa kama ilivyokusudiwa.

“Tumesikia maelelekezo yako, tunatambua uzito na umuhimu wa kazi iliyoko mbele yetu. Tunafahamu Imani ambayo Taifa limetupatia katika kusimamia Sekta ya Petroli-Mkondo wa Juu. Kwa niaba ya wenzangu, nikuahidi kuwa tutafanya kazi kikamilifu.”

Aliongeza kuwa, Bodi inatambua changamoto iliyopo mbele yao na kwamba wako tayari kukabiliana nayo.

Wajumbe wengine wa Bodi ya PURA ni Dk. Josephat Lotto, Bw. Yona Killaghane, Bibi Beng’l Issa na Mhandisi Ramadhan Suleiman.

Uhai wa kipindi cha kutumikia Bodi hiyo kwa wajumbe husika unatofautiana kuanzia miaka mitatu hadi mitano. 

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akisisitiza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA) iliyofanyika Aprili 27, 2017 makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.
 Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Habass Ng’ulilapi (kwa niaba ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa James Mdoe), akiwasomea majukumu yao, wajumbe wa Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA), katika hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo, iliyofanyika makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akizungumza, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA) iliyofanyika Aprili 27, 2017 makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akiwakabidhi vitendea kazi baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA), mara baada ya kuizindua rasmi katika hafla iliyofanyika makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.

 Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA), wakielezea wasifu wao kitaaluma, mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo, iliyofanyika makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.

 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA), Charles Sangweni, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo, iliyofanyika makao makuu ya Wizara mjini Dodoma.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA), baadhi ya wafanyakazi wa PURA, Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Habass Ng’ulilapi (wa pili kutoka kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi (wa pili kutoka kulia), mara baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.

No comments: