Saturday, April 29, 2017

IRAN YAONESHA NIA KUWEKEZA NCHINI


BALOZI MPYA WA IRAN AMTEMBELEA WAZIRI MUHONGO
Aomba Iran ishirikiane na Tanzania sekta za nishati, madini

Na Veronica Simba – Dodoma

Balozi mpya wa Iran hapa nchini, Mousa Farhang amemtembelea Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa ajili ya kujitambulisha na kuzungumzia uwezekano wa nchi za Tanzania na Iran kushirikiana katika sekta za nishati na madini.

Balozi Farhang alimtembelea Profesa Muhongo jana, Aprili 28, 2017 ofisini kwake mjini Dodoma.

Akizungumzia nia ya nchi yake kushirikiana na Tanzania katika sekta ya nishati, Balozi Farhang alimwambia Waziri Muhongo kuwa Iran inazo sifa stahiki katika sekta hiyo kutokana na maendeleo iliyofikia ambapo alieleza kuwa mbali na kuzalisha umeme wa kutosha kwa mahitaji ya nchi, imejenga viwanda vya umeme katika baadhi ya nchi zinazowazunguka.

Aidha, aliongeza kuwa, nchi hiyo huzalisha zaidi ya mapipa milioni nne ya mafuta kwa siku moja.

“Miaka 10 iliyopita, Iran ilikuwa kama nchi nyingine zilizo nyuma kimaendeleo lakini sasa tunazalisha umeme mwingi unaotosheleza mahitaji ya nchi yetu na mwingine tunauza.

Alisema kuwa, kutokana na utafiti alioufanya yeye binafsi, amegundua kuwa, sekta ya nishati ndiyo yenye nafasi kubwa na nzuri zaidi itakayowezesha nchi za Tanzania na Iran kunufaika endapo zitashirikiana.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Iran inavutiwa zaidi kuwekeza Tanzania kutokana na sifa ya uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili ambapo alifafanua kuwa, Tanzania inashika nafasi ya Tatu kwa nchi za Afrika, katika kuwa na uhusiano mzuri na Iran, ikitanguliwa na Afrika Kusini na Misri.

Kwa upande wa sekta ya madini, Balozi Farhang alimweleza Waziri Muhongo kuwa, nchi ya Iran iko tayari kushirikiana na Tanzania katika namna yoyote inayofaa.

Akijibu maombi ya Balozi Farhang, Waziri Muhongo alimweleza kuwa, Tanzania inakaribisha wawekezaji kutoka nchi ya Iran kwa ajili ya kuwekeza katika sekta za nishati na madini.

Akizungumzia maeneo muafaka ya uwekezaji katika sekta ya nishati hapa nchini, Profesa Muhongo alimweleza Balozi Farhang kuwa, kwa sasa Tanzania inahitaji umeme mwingi hivyo wawekezaji kutoka Iran wanakaribishwa kuja kuwekeza katika uzalishaji wa umeme.

Profesa Muhongo alifafanua zaidi kuwa, wawekezaji husika wanaweza kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali vilivyopo nchini ambavyo ni pamoja na gesi asilia, makaa yam awe, maporomoko ya maji, jua, upepo, jotoardhi, mawimbi ya bahari na tungamotaka.

Kuhusu uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, Profesa Muhongo alimweleza Balozi Farhang kuwa, nchi ya Iran inao utaalam zaidi kuliko Tanzania hivyo ni vema timu ya wataalam kutoka Tanzania ikakutana na Timu ya wataalam kutoka Iran ili kujadiliana na kukubaliana maeneo muhimu ya ushirikiano.

Waziri Muhongo pia alieleza kuwa, eneo jingine muhimu linalohitaji uwekezaji mkubwa na makini katika sekta ya nishati hapa nchini ni usambazaji na usafirishaji wa umeme.

Aidha, kwa upande wa sekta ya madini, Profesa Muhongo alisema kuwa, wafanyabiashara kutoka Iran wanakaribishwa kuja Tanzania kununua aina mbalimbali za madini yanayozalishwa nchini, yakiwemo madini ya vito.

Profesa Muhongo na Balozi Farhang, walikubaliana kuunda timu za wataalam kutoka nchi zote mbili, ili wakutane kujadiliana na kukubaliana maeneo yanayofaa kwa ushirikiano wa uwekezaji katika sekta za nishati na madini. 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akifafanua jambo kwa Balozi mpya wa Iran hapa nchini, Mousa Farhang (katikati), wakati Balozi huyo alipomtembelea Waziri ofisini kwake mjini Dodoma hivi karibuni. Kulia ni Ofisa kutoka Ubalozini, Maisarah Ally.
Balozi mpya wa Iran nchini Tanzania, Mousa Farhang (kushoto) akimkabidhi zawadi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Balozi Farhang alimtembelea Waziri Muhongo ofisini kwake mjini Dodoma hivi karibuni.
Balozi mpya wa Iran nchini Tanzania, Mousa Farhang (kushoto) akimkabidhi zawadi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Balozi Farhang alimtembelea Waziri Muhongo ofisini kwake mjini Dodoma hivi karibuni.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akiagana na Balozi mpya wa Iran nchini Tanzania, Mousa Farhang (kulia). Katikati ni Ofisa kutoka Ubalozini, Maisarah Ally.

No comments: