Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Mh. William Lukuvi amefanya ukaguzi wa mfumo wa kodi ya
ardhi katika manispaa ya Musoma Mjini mkoa wa Mara ambapo amebaini wananchi 231
wanadaiwa Kodi ya Pango la Ardhi kiasi cha shilingi milioni 271.
Mhe Lukuvi amemtaka
Afisa Ardhi wa manispaa ya Musoma bwana Joseph Kamonga kuwasilisha majina ya
wadaiwa hao katika Mahakama ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni
pamoja na kupiga mnada majengo na mali zao kawa wakikaidi kulipa kodi hiyo.
“nimeagiza kesi za
madai ya kodi zitolewe hukumu ndani ya siku moja tu ili wadaiwa waweze
kuchukuliwa hatua ya kuuzwa kwa mali zao haraka” Mhe Lukuvi aliyasema hayo
wakati alipo fanya ziara ya kukagua mfumo wa kodi wa manispaa ya Musoma mjini
ili kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi nchini wanalipa kodi kwa hiari kabla ya
hatua za kisheria hazijafuata dhidi yao.
Aidha, Waziri Lukuvi
amefanya uzinduzi wa mpango kabambe (Master Plan) wa Manispaa ya Musoma na
kuwapongeza viongozi na watendaji wa manispaa ya Musoma kwa kuwa manispaa ya
kwanza nchini kuweza kuzindua mpango kabambe wa mji wao. Pia aliwapongeza kwa
uzalendo wao wa kutumia kampuni za ndani katika utekelezaji wa mpango huo.
Manispaa ya Musoma
ilitoa tenda kwa kampuni zalendo ijulikanayo kama CRM ambayo ilithibitisha
uzalendo wake kwa kumaliza kazi waliyopewa kwa wakati. Kutokana na hilo,
Mheshimiwa Waziri alizitaka manispaa zingine kutumia kampuni za ndani ya nchi
ambazo zimesajiliwa na wizara.
Mbali na hayo, Mh.
Lukuvi aliiagiza manispaa ya Musoma kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa
mpango kabambe kwa kutumia wataalam wao (wa serikali) au Makampuni ya ndani.
Pia, aliiagiza manispaa ya Musoma kutoa nakala za kutosha ili mpango huo
uwafikie wadau wote, na kutaka mpango huo utafsiriwe kwa Kiswahili ili madiwani
na wenyeviti wa serikali za mitaa waweze kuwafikishia wananchi kwa urahisi.
Maagizo mengine ni
pamoja na kwataka viongozi wa manispaa zote nchini kusimamia suala la ujenzi
unaofuata mipango miji na kupiga marufuku wananchi wanaojenga bila kupewa vibali
vya ujenzi katika maeneo ambayo yamekamilisha mipango kabambe na kuagiza nyumba
itakayojengwa bila kibali ivunjwe.
Pia aliwataka maafisa
ardhi wa manispaa kutoa elimu ya masuala ya Ardhi kwa kwa maafisa watendaji wa
Mitaa ili elimu na utekelezaji wa masuala ya ardhi ngazi ya wananchi uwe ni kwa
urahisi na wenye kueleweka.
No comments:
Post a Comment