Thursday, April 27, 2017

SONGWE WAJIPANGA KUPAMBANA NA MAAMBUKIZI MAPYA YA UKIMWI



Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Mhe. John Ernest Palingo akifungua kikao cha wadau wa afya Mjini Songwe kilicholenga kutambulisha mradi unatoa huduma mbalimbali za kupunguza maambukizi ya ukimwi ujulikanao kama SAUTI unaofadhiliwa na shirika la Misaada ya Kimataifa ya Maendeleo la Marekani(USAID) na kutekelezwa na shirika la Jhpiego.
Mkurugenzi wa mradi wa SAUTI Dkt. Albert Komba akiwasilisha mada kuhusu Mradi wa Sauti ambao ni Mradi wa miaka mitano unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kupitia Mpango wa dharura wa raisi wa Marekani kwa ajili ya UKIMWI (PEPFAR) katika kikao cha wadau wa afya kwa lengo la kuutambulisha mradi huo.
Mratibu wa kudhibiti Ukimwi kutoka TACAIDS katika Mkoa Songwe Ndg. Emanuel Petro akiwasilisha mada kuhusu mikakati ya Mkoa katika mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI, Mafanikio na changamoto katika kikao hicho
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tunduma ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ukimwi akichangia mada katika kikao hicho
Mdau wa Afya akifafanua jambo wakati wa kikao hicho
Mtaalamu kutoka Mpango wa Taifa wa kuzuia Ukimwi (NACP) akitoa mada nae kuhusu makundi hatarishi na mwongozo mpya wa serikali wa 2017 unaosimamia huduma za VVU na Ukimwi kwa makundi maalum



Serikali ya Mkoa wa Songwe imeanza kuchukua hatua madhubuti kwa lengo la kupambana na changamoto zinazotokana na maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi ili kuweza kufikia malengo ya taifa baada ya kuanza kutekeleza mwongozo mpya wa matibabu kwa wote wanaogundulika na VVU kuanzia Oktoba 2016.


Hayo yamesemwa leo na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Ndg. Eliya Ntandu katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Mhe. John Ernest Palingo kwenye kikao cha wadau wa afya kilicholenga kutambulisha mradi unatoa huduma mbalimbali za kupunguza maambukizi ya ukimwi ujulikanao kama SAUTI unaofadhiliwa na shirika la Misaada ya Kimataifa ya Maendeleo la Marekani(USAID) na kutekelezwa na shirika la Jhpiego.

Akielezea Mradi wa SAUTI katika Mkoa wa Songwe, Mhe. Palingo amesema anatambua malengo ya mradi huu kuwa ni kusaidia jitihada za serikali katika kuboresha afya za wananchi na kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ambapo mkoa wa Songwe ni wanufaika wakubwa kupitia wilaya mbili za Mbozi na Tunduma ambako mradi huu unatekelezwa.

“Mradi huu utasaidia sana kupunguza hatari za maambukizi ya Ukimwi katika makundi maalum yenye hatari zaidi ya kuambukiza au kuambukizwa VVU hususani wanawake wanaoanya biashara ya ngono, Vijana wa Kike nje ya shule walio katika mazingira tete kama ilivyoanishwa katika mwongozo mpya wa serikali wa 2017 unaosimamia huduma za VVU na Ukimwi kwa makundi maalum” alisema Mhe. Palingo

Mapema akiwasilisha mada kuhusu mikakati ya Mkoa katika mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI, Mafanikio na changamoto, Mratibu wa kudhibiti Ukimwi kutoka TACAIDS katika Mkoa Songwe Ndg. Emanuel Petro amesema kwa bahati mbaya bado mkoa wa Songwe unashika nafasi ya tatu katika orodha ya mikoa yenye kiwango kikubwa cha maambukizi Nchini ukiwa na asilimia 9.0.

Kiwango hiki kwa mkoa wa Songwe kinatokana na changamoto mbalimbali zilizopo kama vile uwepo wa baadhi ya Kamati za UKIMWI zisizotekeleza majukumu yake ipasavyo hususan katika ngazi za chini (Zisizokuwa HAI), Uhaba wa rasilimali fedha za utekelezaji wa Afua za VVU na UKIMWI Nchini (Haswa kutoka vyanzo vya ndani – OS), Ushamiri wa Tabia hatarishi miongoni makundi maalum, hususan Vijana wakiwemo wasichana (Ikiwemo na Rushwa ya Ngono/Ngono ya Rushwa) nk.

“Nimatumaini yangu baadhi ya changamoto hizi zitapatiwa ufumbuzi kupitia mradi huu wa SAUTI ambao unafadhiliwa na USAID na kutekelezwa na wenzetu hawa Jpiego ambao kwa kweli umelenga kusaidia juhudi za mkoa wetu katika vita hii ya kuhakikisha maambukizi yanapungua na mkoa wetu unaondoka katika nafasi hiyo. Alisema Ndg. Petro

Awali akiwasilisha malengo ya mradi katika kikao hicho cha wadau wa afya, Mkurugenzi wa mradi wa SAUTI Dkt. Albert Komba alisema kuwa Mradi wa suti ni Mradi wa miaka mitano unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kupitia Mpango wa dharura wa raisi wa Marekani kwa ajili ya UKIMWI (PEPFAR) na ulianza mnamo tarehe 9 Februari 2015 [Songwe ulianza rasmi mwezi Agosti 2015 (Wilayani Mbozi ikiwa ni sehemu ya Mkoa wa Mbeya)]

Katika mkoa wa Songwe mradi una malengo ya kuhakikisha kuwa kuna upatikanaji na utumiaji wa huduma za kukinga ili kupunguza maambukizi ya VVU na kuhakikisha kuwa uzazi wa mpango unaongezeka. Pamoja na malengo hayo pia unakusudia kuhakikisha kuna mabadiliko chanya ya tabia hatarishi na taratibu za kijamii zinazochochea maambukizi ya VVU, Kupungua uhatarishi wa maambukizi ya VVU katika kundi la wasichana walio katika umri balehe na wanawake wenye umri kati ya miaka 15 – 24 pamoja na wanawake wanaofanya biashara ya ngono kwa kutumia njia za kimuundo zenye ubunifu wa hali ya juu.


Pamoja na kutambulisha mradi wa SAUTI, kikao hicho pia kililenga kuwafahamisha wadau mbalimbali wa mkoa wa Songwe na halmashauri zake kuhusu mradi wa Sauti hususan namna unavyochangia jitahada za serikali na mipango mbali mbali ya mkoa, na kutengeneza mikakati ya pamoja ya jinsi ya kushirikiana kwa karibu ili kudhibiti maambukizi mapya ya VVU katika mkoa wa Songwe pamoja na kukubaliana kuhusu majukumu ya kila mdau katika kuhakikisha malengo ya mradi huu yanafanikiwa.

No comments: