Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Mfuko wa Kukuza Sekta ya Fedha (FSDT) imewakutanisha pamoja wadau kutoka sekta mbalimbali za maendeleo nchini kujadili masuala mbalimbali yatakayosaidia uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo Tanzania.
Akizungumza katika kikao kazi hicho mwenyekiti wa Kikundi Kazi, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Peniel Lyimo alisema kuna haja ya dhamira ya dhati na uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo nchini ili kusaidia juhudi za Serikali za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini.
Mwenyekiti wa Kikundi Kazi, Bw. Peniel Lyimo (Katikati) akizungumza na wajumbe wa Kikundi Kazi (Hawapo pichani) wakati wa mkutano wa wadau wa kujadili uwekezaji katika sekta ya kilimo uliofanyika katika Hoteli ya Court Yard, Dar es Salaam. Wanaomsikiliza Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga na Mkuu wa Kilimo na Fedha Vijijini wa FSDT, Bw. Mwombeki Baregu (Kulia).
Bw. Lyimo alisema kuwa ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa hali inayorudisha nyuma mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini.
“Kuna haja ya kutafuta suluhisho la changamoto za upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya Kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga akizungumza juu ya umuhimu wa wadau katika kuchagiza uwekezaji katika sekta ya kilimo nchini.
Akizungumzia umuhimu wa kikao kazi hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga alisema kikao hicho kinalenga kuwaleta wadau kutoka sekta mbalimbali ili kujadili kwa kina njia sahihi za kuchagiza uwekezaji wenye tija katika kilimo nchini.
Bw. Assenga alisema kuwa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo kutachagiza kusaidia uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Kilimo, na kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.
“Kimsingi Kikao hiki kinalenga kuanzisha mtandao mpana wa majadiliano na wadau mbalimbali, zikiwemo Wizara zinazohusika na Kilimo na Taasisi mbali mbali za Serikali na Binafsi, ili kukubaliana vipaumbele na namna ya kushirikiana katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya TADB katika kuleta mapinduzi ya kilimo nchini,” alisema.
Mkuu wa Kilimo na Fedha Vijijini wa FSDT, Bw. Mwombeki Baregu (Kulia) akizungumza wakati wa mkutano huo. Pichani ni Mwenyekiti wa Kikundi Kazi, Bw. Peniel Lyimo (Katikati) na Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kilimo na Fedha Vijijini wa FSDT, Bw. Mwombeki Baregu alisema kuwa FSDT inalenga kushirikiana na wadau ili kuchagiza ushirikishaji mpana wa washirika mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ili kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo nchini.
“Miongoni mwa vikwazo katika kufikia ushirikishwaji wa fedha nchini Tanzania hasa katika uwekezaji katika kilimo ni pamoja na ukosefu wa miundombinu sahihi ya soko na upatikanaji wa fedha na huduma na bidhaa zake maalum katika kilimo, hivyo tunaamini kwa kushirikiana na wadau tunaweza kutatua changamoto hizi,” alisema Bw. Baregu.
Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha wa TADB, Bw. Albert Ngusaru akiwasilisha malengo ya mkutano huo.
Waumbe wa Kikundi Kazi cha Kuchagiza Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo nchini wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa.
Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya FSDT, Balozi Mwanaidi Maajar (Kulia) akitoa mchango wakati wa Kikao Kazi cha Kuchagiza Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo nchini. Kushoto ni Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha wa TADB, Bw. Albert Ngusaru.
Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya FSDT, Balozi Mwanaidi Maajar (Kushoto) akifurahia jambo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (Kulia) wakati wa Kikao Kazi cha Kuchagiza Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo nchini.
No comments:
Post a Comment